Header Ads

LWAKATARE KWENDA NJE KUTIBIWA


 Na Happiness Katabazi
 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imempatia ruhusa  Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi,Denis Msacky ya kwenda nje ya nchi kutibiwa.
 
Sambamba na hilo,Hakimu Mkazi Alocye Katemana alitoa  onyo kwa mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo Ludovick Joseph  asiendelee kuiongelea kesi hiyo nje ya mahakama kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwani kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo  na endapo atakaidi onyo hilo mahakama hiyo italazimika kumfutia dhamana.
 
Wakili wa Lwakatare,Nyaronyo Kicheere aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba wanaiomba mahakama  impatie ruhusu mteja wake aende nje ya nchi kutibiwa kwani anasumbuliwa na matatizo ya mgongo na uthibitisho wa kuonyesha Lwakatare anaumwa alitoa nyaraka za matibabu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo inaonyesha Lwakatare ni mgonjwa na ana matatizo ya mgongo.
 
Aidha wakili Kicheree  wanaulaumu upande wa jamhuri kwa kukaa kimya  bila kulalamika wakati kesi ambayo bado haijaisha mahakamani kuandikwa magazetini, akimtuhumua Ludovick kuwa yeye ndiye aliyefanya hivyo.
 
Baada ya kuwasilisha madai hayo , mahakama ilitoa kibali cha Lwakatare kwenda kutibiwa nje, ambapo leo (jana) hakuwepo mahakamani na pia ilitoa onyo kwa Ludovick.Hakimu Katemana aliarisha kesi hiyo hadi  Agosti 21 mwaka huu kitakapokuja kwaajili ya kutajwa.
.
Machi 18 mwaka huu, ilidaiwa na upande wa jamhuri kuwa Lwakatare na  Ludovick wanakabiliwa na kosa moja la kula njama ya kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.

Juni 14 mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aliwasilisha Mahakama Kuu ombi la kusudio la kukataa rufaa uamuzi wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu uliompatia dhamana Lwakatare na Ludovick na hadi sasa bado rufaa hiyo haijapangiwa tarehe wala jaji wa kuanza kuisikiliza.
 
DPP hakukubaliana na uwamuzi ulitolewa Mei mwaka huu na Jaji wa Mahakama Kuu,Lawrence Kaduri ambao ulimfutia mashitaka matatu ya ugaidi washitkiwa hao, hadi sasa bado Mahakama ya Rufaa haija panga tarehe wala jaji wa kuanza kusikiliza ombi hilo la kuomba mahakama hiyo ya juu kabisa nchini ifanyie marejeo uamuzi wa mahakama kuu ambao ulimfutia mashitaka matatu ya ugaidi Lwakatare na Ludovick..
 
Wakati huo huo; kesi ya wizi wa jumla ya Paspoti 26 inayomkabili mwanamuzi wa muziki wa asili, Che Mundugwao na wenzake jana ilitajwa mbele ya hakimu Sundi Fimbo na upande wa jamhuri ulidai upelelezi bado haijakamilika na akaiarisha kesi hiyo hadi kesho na kuamuru washitakiwa warudishwe rumande kwasababu bado mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi bado hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 23 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.