Header Ads

MRAMBA KWENDA KUTIBIWA NJE YA NCHI
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imempatia ruhusa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali harasa ya Sh.bilioni 11.7.
 
Mbali na Mramba washitakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa  Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wizara ya fedha, Gray Mgonja wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Hurbet Nyange, Peter Swai, Profesa Leonard Shahidi na Elisa Msuya.
 
Ruhusa hiyo ilitolewa jana na jaji Sam Rumanyika  ambapo alisema anakubaliana na ombi la wakili wa Mramba, Elisa Msuya  ambaye aliomba mahakama impatie ruhusa Mramba ya kwenda kutibiwa nje ya nchi kwasababu daktari anayemtibia Mramba amependekeza Mramba akatibiwe nje ya nchi.
 
Jaji Rumanyika alisema anakubaliana na ombi hilo na kwamba anamruhusu Mramba aende kutibiwa nje ya nchi na kwamba wakati Mramba atakapokuwa amekwenda nje ya nje kwaajili ya matibabu kesi yake haitaweza kuendelea kwasababu Mramba  hajatoa idhini kesi hiyo iendelee bila ya yeye kuwepo.
 
“Hivyo natupilia mbali ombi la wakili wa Jamhuri Oswald Tibabyekomya lilokuwa linataka kesi hiyo iendelee kusikilizwa hata kama Mramba hayupo….na kwamba nakubali ombi la wakili wa Mramba hivyo mahakama hii inamruhusu Mramba aende kutibiwa nje ya nchi na ninairisha kesi hii hadi Septemba 16 hadi 20 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya Mramba kuendelea  kuhojiwa na mawakili wa upande wa jamhuri’alisema Jaji Rumanyika.
 
Awali wakili Tibabyekomya aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili Mramba kuendelea kuhojiwa lakini ikashindikina kwasababu Mramba anaumwa lakini hata hivyo jana Mramba aliweza kufika mahakamani hapo.
 
Wakati huo huo; mahakama hiyo ilishindwa kutoa uamuzi wa kumuona Johnson Lukaza na Mwesigwa Lukaza kama wanakesi ya kujibu au la kwasabu miongoni mwa wanajopo wanaosikiliza kesi hiyo ni mgonjwa na hivyo hakimu Nyigulile Mwaseba aliarisha kesi hiyo ya wizi wa sh.bilioni sita hadi Julai 15 mwaka huu,  ambapo jopo hilo litakuja kutoa uamuzi wake  wakuona washitakiwa hao ama wanakesi ya kujibu au la.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Ijumaa, Julai 12 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.