Header Ads

RAIA WA UINGEREZA AUNGANISHWA KESI YA CHE MUNDUGWAO

 
Na Happiness Katabazi
 
RAIA wa Uingereza Ahassan jana aliunganishwa kwenye kesi  ya wizi wa Paspoti  26 inayomkabili  Msanii wa Muziki wa Asili nchini, Chigwele Che Mundugwao na wenzake ambao wanaoendelea kusota gerezani  tangu Mei 3 mwaka huu, kufuatia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi awafungie dhamana.
 
Wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Sundi Fimbo alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa ambao inajumla ya washitakiwa wanne lakini ,upande wa jamhuri unaomba kubadilisha hati ya mashitaka kwasababu inamuunganisha mshitakiwa mwingine ambaye ni raia wa Uingereza na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
 
Wakili Kweka pia aliomba mahakama isitoe masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo kwani upande wa jamhuri utaleta hati ya DPP ya kumfungia pia mshitakiwa huyo dhamana kama washitakiwa wengine walivyofungiwa kwa mujibu wa kifungu cha  148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
 


 Hakimu Fimbo alikubali ombi hilo na kusema sasa hati ya mashitaka itasomeka kuwa ina jumla ya washitakiwa wa tano na akautaka upande wa jamhuri ulete kwa maandishi hati hiyo  ya DPP ya kumfungia dhamana mshitakiwa huyo wa tano na akaiarisha kesi hiyo hadi Julai 22 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa wote warejeshwe rumande.

Mbali na Che Mundugwao ,washitakiwa wengine ni ofisa  Manunuzi  wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius (37) na mfanyabiashara, Ally  Jabir  (34) wanaotetewa na wakili Peter Kibatara.

 Mei 3 mwaka huu, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya  mbele ya Hakimu Mkazi  Aloyce Katemana aliwasomea mashitaka washitakiwa hao na kudai kuwa wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha  384 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.

Wakili Komanya alieleza kuwa kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu , Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma,  katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji aliiba paspoti 26, mali ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Komanya alidai kuwa washitakiwa  Chigwele, Keneth na Ally, Mei 30, mwaka huu, huko Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam ,walikamatwa wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.

Kuhusu  Che Mundugwao,wakili Komanya alidai kuwa mshitakiwa huyo kuwa Aprili 22, mwaka huu alikamatwa akimiliki  paspoti 12  za watu wengine bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi .

Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa Mei , mwaka huu  Che Mundugwao pia alikamatwa na maofisa wanausalama akimiliki pasipoti nyingine mbili  zenye majina ya watu wengine sababu yoyote ya msingi. 
Komanya aliendelea kuwa Aprili 24 mwaka huu, mshitakiwa Ally , alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha kuwa ilikuwa ni halali na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji wakati akijua kuwa si kweli.

Wakili Komanya alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,   Shemweta alighushi nyaraka ya serikali ambayo ni muhuri akijaribu kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na Idara ya Uhamiaji wakati si kweli.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 10 mwaka 2013.
Powered by Blogger.