MAHAKAMA KUENDELEA KUBORESHA MAHAKAMA ZAKE
Na Mary Gwera, Bukoba
JAJI Mkuu Mohamed Chande Othman amesema mahakama imedhamiria kuboresha miundombinu ya majengo ya Mhimili huo,ili huduma inayotolewa na mhimili huo iwe inatolewa katika mazingira mazuri na yenye hadhi.
Akizungumza na katika uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo katika Kijiji cha Karabagaine, Mjini Bukoba mkoani Kagera juzi, Jaji Othman uu aliainisha kuwa moja kati ya vipaumbele vya Mahakama ni kuwafikia wananchi wa kila Mkoa katika kuhakikisha kuwa huduma za Kimahakama hususani za Mahakama za Mwanzo zinasogezwa karibu na wananchi.
"Moja kati ya ngazi za Mahakama zinazoongoza kwa kupokea kesi kwa wingi ni ngazi ya Mahakama za Mwanzo, hivyo kuna haja kubwa ya kuboresha miundombinu pamoja na huduma za utoaji haki katika Mahakama hizi," alisema.
Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa uzinduzi wa jengo hilo la Mahakama ya Mwanzo ni moja ya Mahakama ambazo zitazinduliwa katika mkoa huo wiki ambapo pia jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba linatarajiwa kuzinduliwa leo asubuhi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
"Mahakama ya Tanzania, tumedhamiria kuleta sura mpya ya Mahakama za Mwanzo, na sura hii iendane na dhamira yetu ya utoaji 'Haki sawa kwa wote na kwa wakati' hivyo basi nawasihi Viongozi na watumishi wa Mahakama hii usiishie katika muonekano mzuri wa jengo bali jengo hili liende sambasamba na kasi ya utoaji haki katika eneo hili," alilisitiza.
Kwa upande wake Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Gad Mjemmas alisema upatikanaji wa jengo hilo la Mahakama ya Mahakama ya Mwanzo Karabagaine kutarahisisha upatikanaji wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi waliopo katika kijiji hicho.
Jaji Mjemmas aliongeza kuwa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Karabagaine umegharimu ujumla ya Sh.Milioni 138, zote zikiwa ni fedha za ndani za Mahakama ya Tanzania, na jengo hilo litahudumia wananchi wa Kijiji cha Karabagaine na vijiji vya jirani.
Mbali ya kuboresha miundombinu ya Majengo ya Mahakama, zipo hatua nyingine kadhaa zinazochukuliwa na Mahakama ikiwemo Upatikanaji wa takwimu sahihi wa kesi za muda mrefu, Utunzaji sahihi wa kumbukumbu ambao unaenda sambasamba na uboreshaji wa Masjala za Mahakama hii yote ni katika kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji inaboreshwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania la Alhamisi, Julai 25 mwaka 2013.
No comments:
Post a Comment