KIKWETE USIWASIKILIZE 'BUSH LAWYER' KATIKA ESCROW
KIKWETE USIWASIKILIZE 'BUSH LAWYER' KATIKA ESCROW
Na Happiness Katabazi
IBARA ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 , inasema hivi: ' Mbali na kuzingatia Masharti yaliyomo katika Katiba hii, na Sheria za Jamhuri ya Muungano Katika Utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na Mtu yeyote , isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na Sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote.
Na Ibara ya 4(2) ya Katiba hiyo inasomeka hivi ; " Vyombo vyenye mamlaka ya Utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano NA serikali ya Mapindunzi ya Zanzibar ; vyombo vyenye mamlaka ya kutekeleza Utoaji haki vitakuwa ni Mahakama na Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , na vyombo vyenye mamlaka ya kutunga Sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma vitakuwa ni Bunge na Baraza la Wawakilishi.
Ibara ya 4(3) ya Katiba hiyo pia inasema; " Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano , na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo vilivyotajwa Katika Ibara hii , kutakuwa na Mambo ya Muungano Kama yalivyoorodheshwa Katika Nyongeza ya kwanza iliyoko mwishoni mwa Katiba hii, na pia kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano , ambayo ni mambo mengine yote yasiyo mambo ya Muungano.
Ibara ya 4(4) ya Katiba hiyo inasema ; " Kila Chombo kilichotajwa Katika Ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake kwa kufuata Masharti mengine yaliyomo katika Katiba hii".
Nimelazimika kuanza na nukuu hizo za Ibara ya Katiba ya nchi yetu kwasababu makala yangu ya Leo itazungumzia kuhusu utekelezaji wa kazi na shughuli za Rais na dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka Katika taifa letu ambayo mambo yote hayo yameanishwa Katika wazi Katika Ibara hizo za Katiba.
Leo nitajadili kuhusu Wimbo Ulianza kuchuja kwa kasi ya Mwendo wa ' Pikipiki ambayo hainaga rivasi' wa ESCROW.
Itakumbukwa Kuwa wiki Tatu zilizopita Wimbo wa Escrow ulshika kasi kila Pembe ya nchi na kusababisha kuacha majeraha Katika mihimili yote mitatu ya nchi yaani serikali, Bunge na Mahakama.
Sakata hili la Escrow lilikuwa na sura nyingi ambazo kwa jinsi lilivyochukuliwa liliweza kulichanganya taifa na kujikuta katika mgongano wa hali ya juu. Katika hali ya kawaida, Tanzania imeshawahi kupita katika kashfa nyingi kama zile za Richmond na Buzwagi na hata EPA, hivyo mambo ya kuwepo ubadhirifu au harufu ya ubadhirifu katika kuta au dari za serikali si jambo geni kwa nchi yetu japokuwa kutokuwa geni huko hakuhalalishi vitendo vyenyewe.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mambo mengine inatoa si haki na wajibu wa raia tu bali pia uwajibikaji wa kisiasa na kiutendaji kwa watu mbalimbali waliopewa dhamana ya kushughulikia masuala ya taifa kwa niaba ya wananchi. Ni wazi kuwa katika serikali kuna dhana ya uwajibikaji wa kiwaziri yaani kwa kiingereza “Ministerial Responsibility”.
Katika dhana hii ya uwajibikaji kuna uwajibikaji wa Waziri Mmoja mmoja (Individual responsibility) na uwajibikaji wa Mawaziri wote kwa ujumla (collective responsibility).
Katika uwajibikaji binafsi, Waziri mwenye dhamana ya jambo Fulani katika wizara yake anawajibika kwa matendo yake na ya watumishi wake katika wizara yake hata kama Waziri huyo hakutenda yeye jambo hilo.
Hivi ndivyo ilivyotokea katika sakata la operesheni tokomeza ambapo tulishuhudia mawaziri wakijiuzulu nyadhifa zao kwa matendo maovu yaliyofanywa na askari au watumishi waliokuwa chini ya Wizara zao. Ni hivyo hivyo hata Edward Lowassa aliwajibika japokuwa hakukuwa na ushahidi wa kuchukua hata senti moja.
Uwajibikaji wa kijumla pia ni jambo la kawaida katika nchi nyingi za jumuiya ya Madola hasa zinazofuata mfumo wa kiingereza katika kuendesha serikali zake.
Bunge lina uwezo wa kumwajibisha Waziri Mkuu kwa mujibu wa Katiba ambapo matokeo yake ni kuanguka kwa baraza lote la mawaziri.
Vivyo hivyo Rais anao uwezo wa kuwawajibisha mawaziri wake mmoja mmoja au kuvunja kabisa baraza la Mawaziri kama alivyofanya Rais Ally Hassan Mwinyi mwaka 1994.
Jambo hili ni la kisheria pia kisiasa. Tofauti na ilivyo kwa watumishi wa umma ambao mamlaka zao za nidhamu ni kwa mujibu wa sheria ya utumishi wa Umma ya mwaka 2002, Mawaziri na wateule wengine wa Rais huweza kuwajibishwa bila kuzingatia sheria ya utumishi wa umma kwa kuwa watu hawa hushika na kuendesha nyadhifa zao kwa matakwa ya Rais (at the pleasure of the President).
Hata hivyo, ili Rais amwajibishe mteule wake au ili bunge limwajibishe Waziri Mkuu au kumlamzimisha waziri kujiuzulu au hata waziri mwenyewe binafsi kutangaza kujiudhuru, lazima kuwe na sababu za msingi.
Sababu hizi lazima ziwe za wazi na zenye mashiko na ushahidi ambapo mtu yeyote haitaji kuingizwa darasani kutambua kuwa kuna kosa limefanyika na hivyo mtu Fulani anatakiwa kuwajibika au kuwajibishwa.
Moja ya sababu za kuwajibishwa popote pale inaweza kutokana na kukosa uadilifu kwa mtendaji husika, wizara yake kukiuka sheria au taratibu Fulani, au kuvunja haki za binadamu au kukitokea kashfa kama hii ya escrow, Richmond, epa nk ambazo zinagusa moja kwa moja wizara husika au mtu husika.
Sakata la escrow kama yalivyo masakata mengine yote yaliyowahi kutokea hapa nchini liligusa hisia za watu wengi hasa ukichukulia kuwa nchi bado inakabiliwa na changamoto nyingi za kifedha na umasikini na escrow ilitokea kipindi ambacho hata MSD walikuwa wakilalamikia kutokuwa na Fedha za kununulia na kusambaza dawa mahospitalini.
Hivyo ni wazi kuwa mtu yeyote kusikia bilioni 300 zimetafunwa na wachache lazima apate jazba. Siwezi kusema moja kwa moja kuwa suala la Escrow pengine hakukuwa na ubadhirifu kabisa au hata kama hakukuwepo ubadhirifu basi hakuna watu kwenye ofisi zao ambao hawakutenda kwa makini hivyo kuwezesha baadhi ya taratibu kukiukwa au pesa kutolewa katika utaratibu usiokubalika kisheria.
Vyombo vya uchunguzi vitatueleza zaidi. Waswahili husema, vita ya panzi faida ya kunguru, na penye ugumu penyeza rupia, na pia adui mwombee njaa hata kama shujaa.
Sakata la escrow pamoja nalo limeibua au kuwezesha mambo mengi sana. Limekuwa kama mtego wa panya ambao waliokuwemo na wasiokuwemo wote wanaingia na baadhi ya watu wakauchukulia huu mwanya kutiumiza haja na matakwa yao ya kisiasa.
Hili lilithibitishwa na uchangiaji bungeni na hata ushabiki uliokuwa ukiendelea nchini. Naweza kusema sakata hili limekuzwa sana kuliko uhalisia hasa kutokana na wakati ambao limetokea.
Sakata kwa bahati mbaya sana limeibuka au kupangwa kuibuliwa wakati watu wana nia mbalimbali za kisiasa na tayari makundi mbalimbali yameanza kujipanga kikambi, na kuwekeana mbinu chafu za kuharibiana.
Ugomvi binafsi, wivu na vita kati ya vyama vya siasa vilitawala zaidi kuliko sheria, kanuni na taratibu. Hata kama escrow kweli ingekuwa watu wameiba Fedha bado ushughulikiaji wa watu waliohusika nao unatakiwa kufuata Katiba ya nchi, sheria na taratibu za nchi na sio matakwa ya watu binafsi na kiu tu ya kuona Fulani hayupo kwenye cheo chake.
Baadhi ya watu walijifanya wao Wanaofahamu zogo la Escrow kindakindaki kumbe uzushi mtupu kadri ya uwezo wao waliweza kutumia baadhi ya vyombo vya habari,majukwaa ya kisiasa , bunge kuaminisha umma kupandikiza Chuki kwa wananchi Kuwa baadhi ya viongozi wa serikali akiwemo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhungo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eliachim Maswi , Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema , Jaji Mujulizi, Jaji Luhangisa na wengine Kuwa ni wezi wa Fedha za umma,hawatakii Mema nchi yetu, majambazi sugu na wajiudhuru nyadhifa zao.
Watu hawa walifanya hivi bila kujali haki za watuhumiwa kujieleza na wala kujali ukomo wa kazi wa mhimili mmoja wa dola kwa mwingine.
Haki ya kujieleza ni ya msingi sana kwa binadamu yeyote anayetuhumiwa hata kama kosa lake ni kubwa au linakera kiasi gani na ndio maana kila siku inasisitizwa watu kutochukua sheria mkononi.
Haki hii ya kusikilizwa ina historia ndefu na wanasheria wanaamini kuwa haki hii inatokana na Mungu mwenyewe, kwamba Mungu hatamuadhibu mtu bila kumsikiliza na ndivyo alivyofanya kwa Adam na Eva.
Pale Bustanini Mungu alimwita Adam kwa kumuuliza “ Adam Uko wapi?” Adam akajibu “nilisikia sauti yako nikaogopa na kujificha kwa kuwa niko uchi”.
Mungu akamuuliza nani amekuambia uko uchi? Na kwa nini mmekula tunda la mti wa katikati niliowakataza? Adam akajibu, sio mimi ni huyu Mwanamke uliyenipa.
Kisha Mungu akamuuliza mwanamke maswali. Baada ya kujitetea, Mungu akapitisha adhabu ya kuwafukuza bustanini na kumpa Adam adhabu ya kuilima nchi na kumletea matunda na kwa mwanamke kuzaa kwa uchungu na hatimaye akaweka fitna kati ya nyoka na mwanadamu kwa kusema binadamu watamponda nyoka kila wamwonapo na nyoka atawagonga kisigino wanadamu.
Kwa kufanya hivyo inaaminika kuwa Mungu aliwapa wanadamu wa kwanza nafasi ya kujitetea kabla ya kuwahukumu. Je, sisi ni nani wa kuhukumu kabla ya kuwapa wengine nafasi ya kujitetea?
Siku ile PAC inasoma ripoti yake, kila mtu aliamini kuwa yote yaliyosemwa na PAC yalikuwa ya ukweli na asilimia kubwa ya watu walitamani siku ile ile Muhongo, Sethi, Werema, Pinda wajiuzulu na ikiwezekana kukatwa vichwa vyao.
Lakini hali ilibadilika siku ya pili baada ya Muhongo kuanza kutoa utetezi wake, ambapo aliwabadilisha kabisa kile watanzania walichokiamini kutoka PAC na baadhi wakaanza kuona hana makosa na hata vichwa vya magazeti vilithibitisha hili. Taifa likagawanyika na hata bunge lenyewe.
Utetezi wa Profesa Muhongo ulionekana ni wa kisomi wenye vielelezo na usio wa kubabaisha. Ni kutokana na utetezi huuu majadiliano ya bunge yalichukua sura tofauti kabisa, na ndipo walipojitokeza walioanza kumtetea na wale walioanza kuishambulia serikali bila kujali mgawanyo wa madaraka (separation of powers).
Tuliokuwa tukifuatilia mjadala huu tangu mapema mwaka huu ulivyoanza hadi hadi Novemba 29 Mwaka huu ilipomalizika Bungeni na Bunge lilipotoa maazimio yake kuhusu Wimbo huo wa Escrow kwa kuagiza vyombo vinavyohusika na masuala ya uchunguzi na Maadili vifanyie kazi maazimio hayo ya Bunge ambayo maazimio hayo yalitaka Majina ' yaliyorushwa ' Katika Wimbo huo wa Escrow uliotungwa na Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila na kuwekwa 'sauti na uzushi ' na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ,Zitto Kabwe wachunguzwe.
Mei 18 Mwaka huu, niliandika makala iliyokuwa na kichwa Cha Habari kisemacho ' KASHFA YA ESCROW ISITUVURUGE'. Na baadhi ya mambo niliyo yataadharisha Katika makala hiyo ndiyo yalikuja kujitokeza Katika mjadala wa Escrow Novemba Mwaka huu.
Nampongeza Spika Anne Makinda na Timu yake Kwani , ameonyesha ameiva kiutendaji na ana heshimu dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka hivyo Bunge siyo Chombo peke yake na Chenye maamuzi ya mwisho Katika kila jambo ndiyo Manaa Makinda mara kwa Mara alikuwa aliwaambia wabunge wakati kibao Cha Escrow kikitumbuizwa bungeni Kuwa yeye ni Bush Lawyer hivyo anaitaji kujifunza na kuwataka wabunge wengine ambao ni Ma Bush Lawyer Kama yeye Wakubali kujifunza kuhusu Sakata.
Kwasababu amebaini kuna baadhi ya wabunge wanachangia maoni kuhusu Wimbo huo lakini hawafahamu Maudhuhi ya Wimbo huo jambo ambalo ni kweli Kwani kuna baadhi ya wabunge walikuwa wakitoa maoni Yao ambayo ukipata zama Maoni Yao kwa jicho la Sheria unaishia kuwaona ni mapunguani wa akili.
Tulishuhudia baadhi ya wabunge wakisema Profesa Muhongo na wenzake ni wezi wa Fedha hizo za umma wakati hata CAG Katika ripoti yake ameshindwa Kusema wazi wazi Fedha za Escrow ni za umma au laa lakini wabunge wale ghafla wakajigeuza wao ndio CAG, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kuanza kuwatungia mashitaka Profesa Muhongo na wenzake ni wezi wa Fedha za Escrow ,wameisababishia Tanesco Hasara ya mabilioni na ni majambazi sugu wakati wataja yote haya hawajatuonyesha vielelezo Vyovyote kut ushawishi sisi watu ambao akili zetu zinafikiti sawa sawa tukubaliane nao.
Maana Ibara ya 59B (2) ya Katiba ya nchi inasema; ' Mkurugezi wa Mshitaka atakuwa na uwezo wa kufungua,kuendesha na kusimamia mashtaka yote nchini.Na at ateuliwa na Rais .Tuwaulize hawa wabunge, wanasiasa ,wananchi walipora majukumu ya DPP ya kuwaundia watuhumiwa makosa ,lini Rais Kikwete aliwateua Kuwa DPP?
Mbali na wabunge hao kujigeuza DPP kuwatungia Mashitaka viongozi Hao wa serikali na kidini kuhusu Escrow, pia baadhi ya wabunge wale waliojigeuza Mahakama, Takukuru,Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Jeshi la Polisi.
Wenye akili timamu ambao tunafahamu fika nani yupo nyuma ya Escrow, tulikuwa tunawaona baadhi ya wabunge ambao waliojipachika madaraka hayo niliyoyayataja hapo juu Kuwa uwenda wana matatizo ya akili au uenda fedha wanazodaiwa kupewa waliyopewa na watu waliyokuwa wakitaka viongozi hao waondolewe madarakani bila mamlaka husika kufanya uchunguzi wao imewapofusha macho hadi wakasahau wao wabunge ni watunga Sheria ndiyo waliotunga Sheria za kuanzisha Ofisi za DPP,TAKUKURU, Jeshi la Polisi na Sheria mbalimbali zilizoanzisha Taasisi za umma . Aibu sana.
Kifungu Cha 258(1) Cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 ya Mwaka 2002 imetoa Tafsiri ya neno 'wizi'.
Na ukiifuatilia ripoti ya PAC na maneno yanayotolewa baadhi ya wananchi , taarifa ya Benki ya Mkombo,na Hao wanasiasa uchwara wanaotaka Rais Jakaya Kikwete amtimue kazi Profesa Muhongo na wenzake ,ni wazi Hakuna ushahidi wowote unaonyesha hao viongozi wametenda makosa ya wizi wa Fedha za Escrow .
Pia Hakuna kosa la utakatishaji fedha na wala fedha hazikuchukuliwa katika Benki ya Mkombozi kwa Magunia kama ilivyodaiwa Kama inavyodaiwa na mambumbumbu wa Sheria akiwemo Zitto Kabwe ambaye yeye Katika ripoti ya PAC alisema Fedha za Escow zilipitishwa Katika Benki ya Mkombozi na waliozichukua waliozichukua kwa Magunia jambo ambalo siyo kweli kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Mkombozi.
Kitendo Cha Kamati ya PAC siku ile kusoma mapendekezo yake ya awali ambayo nadiriki Kusema mapendekezo yale ya awali yalikuwa ni ya jazba Kama siyo ya kutaka kukomoana na kuivuruga serikali na ambayo yalikuwa yamevunja dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka na yalikuwa yameegemea Katika baadhi ya taarifa za uongo na uzushi sana na uenda pia lilikuwa na lengo la kuipaka matope Benki ya Mkombozi , waliokuwa wakiwapatia taarifa za kiuchunguzi uenda ni " mashushushu wa Kichina yaani mashushushu Feki".
Kama hawa ndiyo wa tunga Sheria wetu ambao tuliwashuhudia kupitia michango Yao bungeni iliyokuwa ikadhihirisha wazi kuingilia majukumu ya Taasisi nyingine za umma wakitaka Muhongo na wenzake bunge litoe maamuzi ya kuwawajibisha wakati Bunge halina mamlaka ya kumwajibisha Waziri isipokuwa rais wa nchi. Tunajifunza nini kutoka kwa baadhi ya wabunge waliotoa maoni ya aina hiyo?
Tunajifunza nini kutoka Kwa Kamati ya PAC iliyokuwa ikiongozwa na Zitto Kabwe ambapo Maazimio ya awali ya Kamati hiyo yalitoa baadhi ya mapendekezo ambayo binafsi nilisema mapendekezo yale ni ya kijinga ambayo mwisho wa siku yanaweza kuleta madhara kwa bunge ,mjumbe mmoja mmoja katika Kamati ya PAC na kuibua uasama wa kidini baina ya Zitto na kanisa Katoliki.
Kwani Moja ya azimio la awali la Kamati ya Zitto walitaka Benki ya Mkombozi Itangazwe ni Benki ya Utakatishaji Fedha chafu.
Hii Kauli ni nzito sana na Ina madhara makubwa Katika Soko la Ushindani wa Biashara ya mabenki hapa nchi Kwani Benki hiyo ya Kanisa Katoliki ,waumini wengine wa Kanisa Hilo na wananchi wengine wa naitumia na kuamini na kwa mAana hiyo mdau mkubwa wa Benki ya Mkombozi ni Kanisa Katoliki wa Benki ni Kanisa ambalo Kumbe linahusika na Biashara hiyo chafu ya Utakatishaji Fedha haramu.
Kwa hiyo Idara ya Usalama wa Taifa, Polisi zilikuwa zimelala usingizi wa Pono hadi siku zote hizo zikashindwa kubaini Kuwa Benki ya Mkombo ni Benki inayotumika kupitisha Fedha chafu?
PAC ndiyo wamejifanya wao Ndio wamejifanya TISS, Polisi ambao ndani ya Miezi mchache tu wamejigeuza makachero waliokubuhu na wachapakazi ,wakafanya uchunguzi wao wakabaini eti Benki ya Mkombozi Benki inayotakatisha Fedha chafu.Kituko Cha Kufunga Mwaka.
Tuiulize Kamati ya Zitto nayo iliwahi kuhudhuria Mafunzo ya Ushushushu kule Chuo CPP Moshi ? Maana nijuavyo Mimi kazi za upelelezi ni taaluma za watu, watu waliingia darasani wakafundwa na wakafundika na wametulia kimya wala hawanaga papa para wala Kutafuta sifa wakati wakifanya kazi Yao.
Kamati ya PAC kwakuwa Nyie siyo wapelelezi Matokeo yake ilienda kufanya kazi ya upelelezi ambayo siyo taaluma mliyoisomea Matokeo yake mmeenda kukusanya vielelezo vingine vya kizushi ambavyo zilianza kuwaumbua mapema kabisa mfano taarifa ya Benki ya Mkombozi imewavua nguo nguo.
Uamuzi wa PAC kukubali kufanyia marekebisho maazimio ya awali ya PAC ni wazi ripoti ya PAC bado Ina Mashaka makubwa .
Kitendo Cha Kamati ya Zitto kuikubali hoja ya mmoja ya watu waliotajwa kuchota Fedha za Escrow ambaye ni Mwanasheria mkongwe Andrew Chenge lililotaka wote waliotajwa katika Escrow majina yao yafikishwe katika vyombo maalum wafanyie kazi mapendekezo hayo na siyo Bunge tena Katika dakika za mwisho ni wazi uenda PAC iligundua mapendekezo yake ya awali yana mapungufu kisheria na yana puuza dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka (Separation of Power).
Kwa mtu mwenye akili timamu na anayefahamu madhara ya azimio lile,asingethubutu kutoa azimio lile lililotaka Serikali itangaze kuwa Benki ya Mkombozi ni Benki ya kutakatisha fedha chafu mbele ya umma.
Wakati PAC haijaonyesha ushahidi wa kuthibitisha hilo Katika ripoti yake , Matokeo yake Benki ya Mkombozi imetoa taarifa yake kwa umma na imekanusha vikali Kuwa Benki yake haifichi Fedha chafu, watu hawa kuchukua Fedha kwa Magunia ,Fedha zilitoka Benki Kuu Kuja Benki ya Mkombozi kwa mujibu wa Sheria na Benki Yao na iliwapatia fedha Wahusika wahusika kwa utaratibu wa Sheria.
Ndiyo maana Wasomi wa fani ya Sheria ambao siyo wanasiasa wanawadharau sana wanasiasa na wanawaita 'Kunguru' yaani kazi Yao kubwa ni kubwatabwata tu hata Katika vitu wasivyo na ushahidi navyo wao wana bwata.
Tujiulize ni kwanini Kamati ya PAC Imechukua muda mrefu kufanyakazi yake lakini ndani ya siku saa Chache tu ikakubali kufanyia marekebisho baadhi ya maazimio yake?
Tujiulize ni kwanini baadhi ya wabunge wa upinzani Novemba 28 Mwaka huu, usiku wa Bunge walisusia Kikao wakaondoka lakini Kesho yake Novemba 29 walivyorejea jioni walikuwa wapole sana na Kudai eti wametanguliza maslahi ya nchi kwanza na Mbunge wa Hai( Chadema), Freeman Mbowe akasikika bungeni kwa sauti ya Upole kabisa akimshauri Waziri Mkuu Mizengo Pinda zaidishe ukali Kwani amezidi Kuwa mpole mno.
Kama siyo unafki ni nini.Si ni hawa hawa wapinzani hasa Chama Cha Chadema walimkalia Kooni Pinda Mwaka Jana, Pinda alipotoa amri kwa vyombo Vya dola kuwapiga wale wote wasiyotaka kutii Sheria za nchi?
Tena wakati Pinda akitoa agizo Hilo, Chadema ndiyo ilikuwa imeshika kasi kwa kufanya maandamano. Haya Leo hii watu wale wale waliopinga agizo lile la Pinda Leo hii ndiyo wanaushawishi Pinda awe mkali?ajabu sana.Nilichokigundua Katika nchi hii watu wazima ndiyo wanaongoza kwa uongo, uzushi na tabia mbaya Mbaya.
Kwa nini Kamati ili kubali kufanyia marekebisho baadhi ya maazimio yake?Ina maana ilibaini ripoti yake Ina Matundu mengi yanayoitaji kuzibwa. Kama ilibaini mapungufu kwanini sasa tusitilie Shaka pia hiyo ripoti nzima ya PAC uenda Ina mapungufu mengine zaidi ya hayo waliyokubali kayafanyia marekebisho dakika za mwisho?
Zitto ndiyo Mwenyekiti wa PAC ,yeye na Kamati yake wametoa mapendekezo wakina Profesa Muhongo na wenzake wajiuzulu na wachunguzwe.
Lakini Zitto nayeye kupitia Mvumbuzi wa tuhuma za Ufisadi wa Zitto,Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde alitoa Nyaraka zinazoonyesha Zitto nayeye aliomba Fedha kwa Singasinga Yule ambaye Katika ripoti ya PAC ya awali Zitto alitaja Majina ya watu waliopewa Fedha za Singasinga na Kusema Fedha zile ni chafu na kutaka watu wale wachukuliwe Hatua ila yeye alivyotuhumiwa kuziomba Fedha zile hakuona ni Rushwa.
Zitto Katika historia yake ya Maisha ya siasa amekuwa akipenda kulazimisha wanasiasa wenzake wanaotuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali wajihuzuru nyadhifa zao eti hiyo ndiyo dhana ya uwajibikaji.
Lakini Zitto huyu huyu naye kwa Miaka miwili sasa amekuwa akituhumiwa na Chama Chake Kuwa ni msaliti wa Chama ,hadi Chama Chake kilifikia Hatua ya Kumvua nyadhifa zote za uanachama na hivi sasa Zitto ni Mbunge wa Mahakama.
Yeye wakati akikabiliwa tuhuma hizo za Usaliti wa Chama Chake na sote tunafahamu tuhuma za Usaliti ni tuhuma kubwa sana, Zitto hakujihudhuru nyadhifa zake Kama Cheo Cha Ubunge, Naibu Katibu Mkuu.
Zitto alishupaa hadi viongozi wa Chadema walivyomvua madaraka kwa Kusema huo Umaarufu anaolinga nao amepata kutokana na Chadema hivyo Zitto siyo maarufu kuliko Chadema jambo ambalo ni kweli Kwani Umaarufu aliyokuwa nayo Zitto Miaka ile siyo aliyonayo sasa Kwani HIvi sasa Baadhi ya watu wamekosa Imani na Zitto kutokana na tuhuma za Usaliti kwa Chama Alichokuwa alilitumikia cha Chadema.
Kama Kujihudhuru kwa tuhuma tu na Kujihudhuru kuna mjengea Mtu heshima, kwanini Zitto asingeanzaga yeye Kujihudhuru ili awe mfano?Maana na yeye alikumbwa na anaendelea kuandamwa na kashfa Chungu mbovu zikiwemo za kuhongwa fedha kwaajili ya kusaliti Chadema?
Hivi kashfa zilizokuwa zikimwandama Zitto si kashfa nzito kuliko kile kinachodaiwa kuwa ni kashfa ya Escrow iliyomwandama Jaji Werema, Profesa Muhongo, Tibaijuka,Maswi?
Watoto wa mjini tunamuita Mtu msaliti ni ' Chaja ya Kobe' .Yaani anatoa Siri za upande mmoja anapeleka upande mwingine.Maana Chaja ya Kobe Ina Chaji aina zote za Betri za simu.
Profesa Muhongo tangu ashike wadhifa wa kuongoza Wizara ya Nishati , amekutana na misukosuka mizito ambayo Iliiletea taifa Hasara kubwa barabara kuaribiwa,baadhi ya wananchi kuumizwa na nyumba zao kuchomwa Moto baadhi ya wananchi huko Mtwara wapo magereza na wengine wanakabiliwa na Kesi za jinai kwasababu walisababisha vurugu kubwa huko Mtwara wakishinikiza Bomba la Gesi lisijengwe Mtwara Kuja Dar Es Salaam.
Tulishuhudia Mwenyekiti wa IPP, Reginal Mengi alivyokuwa akikabana Koo na Muhongo kwa kile kilichodaiwa na Mengi Kuwa Muhongo anawadharau wafanyabiashara wazawa Kuwa hawana Fedha.
Tulishuhudia Katika Bunge la Bajeti la Mwaka huu, jinsi baadhi ya wabunge walivyokuwa wamempania Profesa Muhongo ili Wawakikishe Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini isipite.
Lakini Hila zote hizo zilishindwa Bajeti ikipita, wafanyabiashara waliokuwa wakidai wana fedha za kutosha ili Wapewe vitalu Vya gesi walishindwa kwenda kujiorodhesha TPDC na kutimiza vigezo na bomba la gesi likajengwa Mtwara na Hali ya utulivu imerejea Mtwara.
Minasema mnyonge mnyonge ni lakini haki yake mpeni.Kama kuna mazuri yaliyofanywa na Muhongo chini ya Utawala wake basi Nyie mabingwa wa fitna my aseme siyo kila kukicha Kusema Mabaya ya Muhongo mazuri yake hamuyasemi.
Hivyo ndiyo maana napongeza uamuzi wa Bunge chini ya Spika Makinda kuamua kupeleka maazimio ya bunge kwenye Taasisi za dola ili zifanyie kazi na wataalamu Kwani hata mwenyekiti wa PAC yaani Zitto na yeye ni mtuhumiwa.
Ndiyo maana Nampongeza Spika Makinda na Timu yake kutoka azimio la kutaka maazimio hayo yapelekwe kwenye mamlaka za dola zinazohusika na masuala ya uchunguzi zitafanyie kazi kitaalamu tuhuma hizo maana za Wimbo wa Escrow ambao umeanza kushuka chati kwa kasi sana.
Maana Hakuna ubishi PAC haina mamlaka Ya kuchunguza tuhuma za Uhalifu na kufikisha mtuhumiwa mahakamani ,mamlaka zenye mamlaka hayo ndiyo zenye jukumu la kufanyia kazi maazimio hayo ya Bunge.
Tayari Spika Makinda ameishatamka zaidi ya Mara mbili bungeni na Mara ya mwisho ni Novemba 29 Mwaka huu, akifunga vikao Vya Bunge Alisema kuna baadhi ya wabunge wanatumiwa na wafanyabiashara Kuja kuwasemea Shida zao bungeni na kwamba siku walikamatwa na polisi NA kufikishwa Mahakamani yeye hatakuwa Tayari kwenda kuwawekea dhamana na wa akawataka waache tabia hiyo.
Na Katika Escrow kuna taarifa ambazo bado hazijathibitishwa na mamlaka husika kuwa kuna mwanasiasa na mfanyabiashara wenye Nguvu za kiuchumi wamekuwa wakidaiwa kutapanya Fedha kwa wanasiasa, vyombo Vya Habari na wapambe washikilie Bango suala la Escrow ili Rais Kikwete aweze kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Profesa Muhongo, Jaji Werema, Maswi na wengine wajiudhuhuru kwasababu ni wahusika wa ufisadi wa Escrow.
Minasema Kama taarifa hizi ni za kweli Hao watu Wawili ndiyo wapo nyuma ya sekeseke hili lililoacha majeraha Katika Mhimili wa Mahakama, Bunge na serikali ikabainika hakuna matendo yoyote ya kijinai,kimaadili yaliyotendwa na watu waliotajwa kwenye Wimbo wa Escrow, serikali kupitia njia zake inazozijua iwashughulikie kikamilifu waliopo kwenye sekeseke la Escrow na wale wabunge ambao Spika Makinda ametuambia wamekuwa wakipewa Fedha za Wafanyabiashara Kuja kuwasema mambo Yao bungeni ambayo hayana tija kwa taifa zaidi ya kutaka kuivuruga nchi kwa kuwapandika wananchi Chuki Mbaya ambayo mwisho wa siku wananchi wanaanza kumkukia Waziri Mkuu Pinda, Profesa Muhongo na serikali kwa ujumla Kumbe siyo kweli.
Tuwaulize wale wote wanaoshabikia suala la Escrow na wanataka Muhongo ,Pinda Wafukweze kazi Wanaofahamu madhara ya hayo wanayoyasema?
Kama wangekuwa wa nafahamu wasingekuwa wanafadhili na kuchochea taarifa hizo potofu ambazo hata CAG Katika ripoti yake hajathibitisha Kama Fedha zile ni za umma na kweli zilibwa na wahusika.
Kumbukeni Nyie wapayukaji mnaopayuka bila vielelezo Kuwa Kikwete awatimue kazi viongozi Hao, Hao nao wana Mungu anawalinda na vile vile wanastahili heshima Katika Jamii inayowazunguka.
Kitendo Cha kuwaita eti ni wezi wakati hata hiyo ripoti ya PAC, CAG haijasema kuna wizi umefanyika Katika Fedha za Escrow ,mnawakosea adabu na Mungu atawadhibu hapa hapa Duniani licha Tayari Mungu ameishaanza kuwaanika hadharani wale wote waliokuwa NA ajenda chafu kuhusu Escrow.
Kama kweli Escrow ni kashfa na Fedha za umma zimeibwa, ni kwanini kuwepo na taarifa Kuwa kuna mfanyabiashara na mwanasiasa wanatapanya Fedha kwa baadhi ya wa Bunge na baadhi ya waandishi wa Habari ili waandike wanavyotaka wao kuhusu Escrow kushinikiza Pinda, Muhongo ,Werema wajiudhuhuru nyadhifa zao?
Hivi Hao waliopo nyuma ya Mpango huu Kama kweli wana uchungu wa Fedha za Escrow zimeliwa,kwanini sasa wasijitokeze hadharani kuamasisha wanasiasa,wananchi,vyombo Vya Habari bila kuvihonga Fedha wakidai Fedha za Escrow?
Kwani wanatumia Fedha Katika Escrow? Na Nyie Mavuvuzera wa Escrow Kama kweli ni wazalendo wa taifa Hilo na mnadai Fedha za Escrow zimeibwa ,kwanini basi hamjitolei kupiga kelele bila kutumiwa kupokea bahasha?
Hata Kama ni kweli wamekula hizo Fedha,wakishajihudhuru nyadhifa zao Ndio hizo Fedha za Escrow zitarudi?
Haya hata hizo Fedha zikirudi , Ndio Nyie mavuvuzera wa Escrow ndiyo mtaitwa mmoja mmoja Mpewe Fedha hizo mkononi mkalipie Ada watoto wenu mashuleni?
Watanzania Hasa wanasiasa wanaume acheni tabia ambazo hata sisi watoto wa kike siku hizi Tumeacha kuzifanya, yaani ya roho Mbaya , tabia za Chuki, wivu,uzushi, husuda,kulipizana visasi,kutaka Kumuendesha Waziri Muhongo jinsi unavyotaka eti Kwasaabu alikunyima 'ulaji ' Fulani.
Au Waziri Mkuu Pinda anataka Kugombea Urais basi unaamua kumzulia zengwe ili aonekane hafai ni mchafu, jinsi unavyotaka wewe eti kwasababu una Nguvu ya Fedha na mali .Ni Ujinga wa aina yake na dhambi kwa Mungu Kwani Biblia inasema ole wake anayeshiriki Katika mashauri ya uongo.
Eleweni siyo kila kila kiongozi atakubali kuendeshwa na matajiri wanavyotaka, kuna baadhi ya viongozi ndani ya serikali nawafahamu ni waadilifu wa nafanyakazi zao kwa kufuata Sheria na siyo matakwa ya wafanyabiashara na wanasiasa uchwara kutekeleza ajenda zao chafu.
Wafadhili na waasisi wa zengwe la Escrow hivi sasa mnatakiwa Mkae chini na Kama mnaakili timamu, mjiulize ni kwanini Bunge kwa kauli Moja lilitoa azimio la Kusema Bunge halina mamlaka ya kuwawajibisha watuhumiwa. mwenye mamlaka ni aliyewateua na Bunge likasema litapelaka mapendekezo kwa mamlaka za serikali zifanyie kazi.
Nawaombea kwa Mungu watendaji wote waliopo kwenye mamlaka husika ambazo zinafanyia kazi jambo hilo ,Mungu awaongoze na awape hekim na busara ili muweze kutenda haki katika kufikia uamuzi na anayestahili kupata haki yake na apewe bila kudhurumiwa.
Historia inaonyesha ni Bunge hili mwaka 2004 lilizushusha uzushi mkubwa kuwa aliyekuwa Balozi wa Italia, Profesa Costa Mahalu amefadha ubadhilifu katika ununuzi wa jengo la Ubalozi wetu Italia.
Takukuru wakakurupuka wakamfungulia kesi mahakamani na mwisho wa siku Aliyekuwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Elvin Mugeta alimwachilia huru Mahalu kwasababu hakuwa ametenda makosa aliyoshitakiwa nayo na DPP akakata rufaa Mahakama ya Rufaa na mapema mwaka huu, DPP mwenyewe akatumia mamlaka yake kuiondoa rufaa ile kwasababu alikuwa hana haja ya kuendelea na rufaa ile.
Siyo Siri wakati Kesi ya Mahalu ilipokuwa ikiendelea huku mitaani tena baadhi ya maofisa wa serikali toka Taasisi za kichunguzi walikuwa wakisema wazi wazi Kuwa Kesi hiyo ilikuwa na mkono wa Kikwete na wakati wakisema hayo hawatoi ushahidi Kuwa Kikwete alikuwa akimgandamiza Mahalu.
Ni tabia Mbaya sana kumzushia Rais tuhuma Kama hizi Kwani zinaweza kusababisha kupandikiza Chuki baina ya mtuhumiwa na rais na familia yake.
Tumeshuhudia Leo hii Mahalu amekuwa msaada mkubwa Katika taifa Hilo hasa Kipindi kile Cha Bunge Maalum la Katiba, sote ni mashahidi alivyoweza kutumia taaluma yake ya Sheria na kushirikiana na wajumbe wenzake kuanzisha Katiba Pendekezwa imepatikana.
Siku zote minasemaga Mtu Aliyesoma vizuri Darasani amesoma tu .Ila nchi hii imezuka tabia ya kudharau wasomi na kumpuuza kila ushauri au Utendaji unafanywa na wasomi wa ngazi ya juu Kama Maprofesa, Madaktari.Matokeo yake baadhi ya wasomi Hao wameamua kukaa pembeni.
Hivi inaingia akilini tumpoteze Profesa Muhongo,Tibaijuka, Werema kwa hoja kirahisi rahisi tu ambazo zinatolewa na watu ambao Tayari nao tunawatilia Mashaka uadilifu wao? Tujipe muda kwanza Tusubiri uchunguzi wa vyombo Vya dola vitatuleta majibu gani.
Ni wabunge hawa hawa walimwandama aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo Kuwa ni kiongozi jeuri, aliyetoa Rushwa kwa wabunge ili Bajeti ya Wizara yake ipite, lakini Makinda alikataa akasema Bunge lake halina mamlaka ya kumwajibisha Jairo hivyo maazio ya Bunge an aagiza yapelekwe kwenye Taasisi husika zitafanyie uchunguzi.
Kweli Taasisi zilifanywa uchunguzi wake kitaalamu na mwisho wa siku sijatoka na ripoti Kuwa Jairo hakutenda makosa aliyedaiwa Kutenda na wabunge hivyo Jairo.
Wazushi Hao ambao wanaomzushia Rais Kikwete wapo kila kona Kwani hata Sakata hili la Escow huku mitaani ,walidiriki Kusema zogo la Escrow limeundwa kwa makusudi na Kikwete Kwani Kikwete amekuwa na tabia ya Kuzusha zogo halafu anaenda nje ya nchi anatuacha tuparulane yeye anafuatilia zogo Hilo kupitia mitandao na Televisheni akiwa nje ya nchi huku akicheka.
Wazushi Hao walinitaka nikumbuka Enzi za zogo la Oparesheni Tokomeza Ujangili ,rais Kikwete alilijua zogo Hilo litalipuka baada ya muda mchache yeye kufika nje ya nchi.
Kwa hiyo zogo la kashfa ya Oparesheni Tokomeze Ujangili liliposhika kasi na Desemba Mwaka Jana Bungeni mawaziri watatu akiwemo Dk.Mathayo David, Balozi Kagasheki na Dk.Emmanuel Nchimbi na Shamsi Vuai Nahodha yeye Kikwete alikuwa nje ya nchi ila alikwenda huko eti kwa Lengo la Kuja kujiokosha Mbele ya safari Kuwa wakati zogo Hilo lilitokea yeye halikuwa hajui na alikuwa nje ya nchi.
Watu wengine wanasema Kikwete hawezi kuwachukulia Hatua wadaiwa Kwasababu zogo Hilo la Escrow linaiusu familia yake yaani mkwe wake aliyemuona Mtoto wake wa kwanza na mwanae wa Kiume,ndiyo taarifa hizo Mbaya zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa. Ukweli au uongo wa hili wanaujua wasambazaji na watengenezaji wa SMS hiyo.
Vyovyote Iwavyo minapenda kutoa raia kwa wananchi wenzangu waache tabia ya kushabikia na kutoa hukumu Katika mambo ambayo hawayajui chimbuko lake Kwani mwisho wa siku wanaonekana ni wendawazimu Mbele ya wajuzi wa mambo.
Maana huku vijiweni mitaani tunawashuhudia wanaume wazima na ndevu zao wanazungumzia jambo la Escrow bila woga wanasema wanataka Fedha zao zilejeshwe na Hao viongozi ni wezi wafikishwe.
Ukiwahoji ni kiasi gani Cha Fedha kimeibwa hawajui?Fedha zile zilikuwa ni mali ya umma au mtu binafsi hawajui? Kilibwa nani na lini hawajui? Wanafahamu kosa la wizi ili lithibitishwe ni lazima kuna vitendo gani vimetendwa na mtuhumiwa hawajui?
Ushahidi wa viongozi Hao wa umma kuiba Fedha hizo wanao wanajibu hawana ila walisoma taarifa za Escrow kwenye magazeti basi nao wameamua kuwaita viongozi wale ni wezi eti kwasababu Gazeti limesema.Ujinga wa aina yake.
Ni hatari sana kwa taifa Kuwa na watu wa aina hii ambao ni waropokaji na wasiyotaka kufanyia utafiti kwa kina jambo Fulani ndiyo watoe Itimisho.
Wao wanatoa itimisho Kabla hata ya kujua undani wa jambo husika wanalolitaka ikiwa. Mnajichumia dhambi bure kwasababu mnashikiriki Katika mashauri ya uongo.
Niitimishe kwa kutoa rai yangu kwa Rais Kikwete siku ikifika ya yeye au Taasisi zake kutolea uamuzi jambo Hilo,watende haki bila kutoa watu kafara kwa Kigezo tu cha kujisafisha Chama Cha CCM kuelekea uchaguzi Mkuu na serikali za Mitaa.
Kwa utafiti wangu niliofanya zogo la Escrow haliwezi kusababisha wananchi wakaachaa kuipigia CCM kura za ndiyo Kwani kazi ya Kujenga Chama iliyofanyiwa na Mzee Mangula, Abdulahman Kinana, Nape Nnauye na maofisa wengine wa Chama Katika kutekeleza Ilani ya CCM ni vigezo tosha kwa CCM kupata ushindi mnono Katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14 Mwaka huu, na uchaguzi Mkuu Mwaka 2015.
Hata wapinzani wanalijua hilo Kwani kuna baadhi ya wabunge wa upinzani na madiwani wamelishalijua Hilo.
Tulimsikia Kafulila Bungeni akisema serikali ya CCM itaanguka Kama Muhongo na wenzake hawatawajibika.
Watu wenye akili timamu tulishia kujiuliza hivi huyu Kafulila si ni Mbunge wa Upinzania wa Chama Cha NCCR - Mageuzi ?Hivi serikali ya CCM kweli ikianguka Kama alivyodai Sindio itakuwa faida kwa wapinzani ?Sasa Kwani Kafulila alijifanya anaionea huruma serikali ya CCM isianguke ?Kama siyo unafki ni kitu gani?
Rais Kikwete Kumbuka hawa hawa baadhi ya viongozi wa upinzani ndiyo wamekuwa wakienda kwa nchi wafadhili kuzieleza nchi hizo zitunyime misaada kwasababu Viongozi wa serikali wamekuwa mafisadi wameshindwa kusimamia Fedha za misaada zinazotolewa na Mataifa hayo.
Minawauliza nyie baadhi ya viongozi wa vyama Vya upinzani mkishaenda kuissma vibaya Tanzania kwa Mataifa ya kigeni mtapata faida gani Kama siyo Kuwaumiza Watanzaia walalahoi ambayo watakosa huduma za kijamii Mataifa hayo yakisitisha kutoa misaada?
Inasemekana Wazengu Wengi wanatuona sisi Waaafrika ni watu tusiyo na akili timamu,wezi,tusiyopenda maendeleo?Haya mlivyoenda kuwaambia Wazungu serikali ya nchi yenu inavuja Fedha za umma ndiyo WAzungu wamewaona Nyie mnaakili sana,siyo wezi na wamewapatia makazi ya kudumu huko huko Ulaya?Mbona mmerudi hapa hapa Tanzania kuishi Katika nchi ambayo viongozi wake ni wezi?
Baadhi ya wananchi wanaopayuka mitaani na kwenye vyombo Vya Habari wakinipa fanya wanakusii sana wewe umwajiishe Pinda, Muhongo na wenzake siku za nyuma watu Hao ndiyo walikuwa vinara wakusema wewe ni Rais dhaifu, Huna Kauli wala huwezi kufanya maamuzi magumu, chekibomu, rais wa kupendakuchekacheka na Huna akili.
Sasa Kikwete jiulize imekuwaje ghafla watu Hao wanakuona leo hii baada ya bunge kutoa maazio yake kuhusu zogo la Escrow wakuone wewe ni rais mchapakazi , unauwezo wa kutoa maamuzi na siyo rais dhahifu?
Rais Kikwete umekuwa ukipenda kuwataka Watanzaia wasiwe na akili za Mbayuwai na kwamba akili za kuambiwa wachanganye na akili zao.
Na Mimi Leo naitimisha kwa kumwambia Rais Kikwete asiwe Kama Mbayuwaia,akili za kuambiwa achanganye na zake. Na Usiwasikilize 'Bush Lawyers' na wazushi Katika Escrow.
Mungu Ibariki Tanzania
Chanzo: Facebook: Happy Katabazi
Blogg: www.katabazihappy.blogspot.com
0716 774494
Disemba 12 Mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment