Header Ads

DPP APINGA DHAMANA YA WAVUVI HARAMU

Na Happiness Katabazi

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP)Eliezer Feleshi amekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kupinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya uvuvi haramu inayowakabili raia 32 wa kigeni waliokamatwa kwenye meli ya Tawariq 1.

Kwa mujibu wa vyanzo kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu, zimelieleza gazeti hili kuwa ofisi ya DPP iliwasilisha ombi la rufaa mahakamani hapo hivi karibuni na imeishapewa Na.78 ya mwaka huu.

‘Nakukuakikisha DPP amefungua ombi hilo la rufaa na Jaji Njegafibile Mwaikugile ndiye amepangwa kusikiliza rufaa na ombi hilo litaanza kusikilizwa rasmi Septemba 3 mwaka huu’kilisema chanzo chetu kwa masharti ya kutotajwa jina.

Katika ombi hilo, DPP anapinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Kisutu ambayo moja ya sharti la dhamana lilisema ili mshitakiwa adhaminiwe ni lazima awe na wadhamini wawili wanaotambulika na ofisi za ubalozi,sharti ambalo linapingwa na DPP kwa madai kwamba ofisi ya ubalozi siyo sehemu ya Tanzania.

Julai 22 mwaka huu, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alitupilia mbali ombi la upande wa mashitaka katika kesi hiyo lilokuwa likiomba mahakama isipokee ripoti ya tathimini ya meli hiyo kwasababu ripoti hiyo ni ya uongo na kamwe haiwezi kuisaidia mahakama.

Lema alisema mahakama hiyo ilichokuwa ikikitaka katika ripoti ni tathimini na si dosari za uandaaji wa ripoti kama inavyodaiwa na upande wa mashitaka na kuongeza kuwa ripoti hiyo imewezesha mahaka a hiyo kufikia uamuzi wa kutoa dhamana kwa washitakiwa ambao ambao wamesota rumande kwa miezi saba sasa.

Akitoa masharti ya dhamana siku hiyo alisema meli hiyo na samaki ambao wanathamani ya sh bilioni 2.7, vitadhaminiwa kwa bondi ya dola za kimarekani 250,000, kila mshitakiwa anadhaminiwa na wadhamini wawili wanaotambulika na ofisi za balozi ambapo wadhamini hao wawili watasaini bondi ya dola 25,000 hata hivyo washitakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi sasa.

Machi 10 mwaka huu, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mawili, shitaka la kwanza ni kuvua samaki bila leseni kinyume na sheria ya Uvuvi wa Samaki katika kina kirefu ya mwaka 2009.

Alidai Machi 8 mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja, saa sita usiku katika ukanda wa bahari ya Hindi ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakiwa wakivua samaki bila leseni.Na washtakiwa wote walikana mashtaka na wapo rumande kwaajili ya wameshindwa kutimiza masharti dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 1,2009

No comments:

Powered by Blogger.