Header Ads

SERIKALI YAMBANA MRAMBA

*Yadai alitoa msamaha wa kodi bila kuwashirikisha mawaziri, AG
*Yaeleza Yona, Mgonja walivyoshiriki kuifutia kodi Alex Stewart
*Yatoboa siri kwamba washitakiwa waliwahi kukiri kutenda kosa

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa serikali katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, umeieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo alitoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation bila baraka za Baraza la Mawaziri na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Maelezo hayo yalitolewa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda wakati akisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo, mbele ya jopo la mahakimu wakazi linaloongozwa na John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela.

Maelezo hayo yanatofautiana na aliyowahi kuyatoa Mramba kwamba Ikulu wakati huo chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa pamoja na Baraza la Mawaziri, walitoa baraka za msamaha huo wa kodi.

Huku akisaidiwa na Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tabu Mzee, Manyanda alidai kuwa Mramba aliidhinisha na kuweka saini matangazo ya serikali ya kusamehe kodi kampuni hiyo namba 423/2003, 224/2003, 497/2004, 498/2004, 377/2005 na 378/2005, na kwamba matangazo hayo ya serikali, yalitolewa bila kuzingatia ushauri wa Mamlaka ya Kodi nchini (TRA).

Alidai kuwa, uchunguzi uliofanywa na TRA, umeonyesha kuwa kutokana na misamaha hiyo ya kodi iliyotolewa na Mramba bila baraka za Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu, ilisababisha serikali kupata hasara ya sh 11,752,350,148.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea; Hurbet Nyange, Peter Swai, Professa Leonard Shaidi na Joseph Tadayo.

Kuhusu Yona, Manyanda alidai kuwa Mei 26, 2003, alishauriwa na Godwin Nyero kutoka Kitengo cha Sheria, kwamba haikuwa vyema kuichukua Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation kwa madai kuwa ilikuwa ni kukiuka taratibu za zabuni, lakini Yona hakukubaliana na ushauri huo.

Wakili Manyanda aliendelea kudai kuwa, pamoja na ushauri huo, hatimaye hati ya makubaliano ya awali kati ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kampuni hiyo uliandaliwa, ambapo katika kipengele cha nne na tano, vilikuwa vinatoa msamaha wa kodi zote kwa kampuni hiyo.

Alidai kuwa, Mei 26, 2003, ofisa namba moja wa Menejimenti ya Fedha, Mrs Soka, aliishauri Wizara ya Fedha kwamba itafute ushauri kutoka TRA ili kujiridhisha endapo Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation ilikuwa inastahili kupewa msamaha wa kodi, na kama kulikuwa na barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Fedha.

“Na katika hati ile ya makubaliano, ilikuwa na mambo mawili ndani yake. Mosi; msamaha wa kodi na alishauri kwamba ni vyema wapate ushauri kutoka TRA,” alidai Manyanda.

Huku washitakiwa hao wakifuatilia maelezo hayo kwa makini, Manyanda alidai kuwa mbali na dokezo hilo, kuna barua iliyoandikwa na Mrs. Soka ya Mei 26, 2003 kwenda kwa Kamishna Mkuu wa TRA, ambayo pia iliambatanishwa na hati ya makubaliano kati ya BoT na kampuni hiyo, ikiomba TRA itoe ushauri kuhusu kifungu cha 4.1 B-D na 5 cha hati ya makubaliano, vinavyohusiana na msamaha wa kodi.

“Wakati ushauri wa TRA unasubiriwa, hati ya makubaliano ilifanyiwa marekebisho katika vifungu hivyo na kisha ikatiwa saini na kuambatanishwa na viambatanisho vya makubaliano hayo, vyote vilitiwa saini Juni 18, 2003 na aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali kwa niaba ya BoT na Erwin Flores ambaye ni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Alex Stewart Government Business Corporation.

“Marekebisho hayo hayakufuata mahitaji ya msamaha wa kodi wa kampuni hiyo na makubaliano hayo yalitiwa saini Juni 18, mwaka huo kwa maelekezo ya Mramba pasipo kuthibitishwa na Baraza la Mawaziri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, uamuzi ambao ulikiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2001,” alidai Manyanda.

Aidha, alidai Mramba aliamua kwenda kwa mshitakiwa wa tatu, Mgonja, na kukiri kwamba taratibu za utiaji saini makubaliano hayo zilikiukwa na kuomba ushauri wa namna ya kuidhinisha msamaha wa kodi.

Alidai kuwa, baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, TRA ilitoa ushauri wake kupitia barua ya afisa wake, AAM. Temba ya Septemba 24, 2003 ambayo ilisisitiza kampuni hiyo haikustahili msamaha wa kodi.

Wakili huyo alidai kuwa, Juni 12, 2003, Mramba katika barua yake aliyomwandikia Yona, alisema kuwa zoezi la kuajiri kampuni hiyo lililetwa wakati bajeti ya mwaka 2003 hadi 2004 ilishapita, na kwamba matokeo ya kutumia makusanyo kutoka kwenye mirahaba, yangetumika katika ukaguzi wa dhahabu.

“Mramba alimshauri Yona atumie bajeti ndogo ya mwaka 2003-2004 kupeleka makadirio ya matumizi ya bajeti hiyo ili Bunge liweze kujadili kama makusanyo ya mirahaba yatatumika kusaidia zoezi hilo la ukaguzi wa dhahabu,” alidai Manyada na kuiomba mahakama ipokee barua hiyo kama kielelezo, ombi ambalo lilikubaliwa na Wakili wa Mramba, Nyange.

Manyanda alidai kuwa, lakini Mramba hakufikisha suala hilo bungeni katika bajeti ndogo ili liweze kufanyiwa maamuzi, badala yake alimtaka Mgonja amshauri jinsi gani angeweza kutoa misamaha hiyo ya kodi iliyokuwa inaombwa na kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Manyanda, Agosti 19, 2003 barua toka Wizara ya Fedha kwenda kwa Kamishna Mkuu wa TRA, iliambatanishwa na hati ya makubaliano yaliyotiwa saini Juni 18, 2003 kwa ajili ya ushauri wa pili kama kampuni ya Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation, ilistahili msamaha wa kodi.

“Kwa mara nyingine tena, TRA kupitia barua yake ya Oktoba 2003, ilithibitisha kuwa kampuni hiyo, haikustahili msamaha wa kodi,” alidai Manyanda.

Alidai kuwa, Septemba 5, 2003, Wizara ya Nishati na Madini, iliiandikia barua Wizara ya Fedha ikiomba msamaha wa kodi kwa niaba ya kampuni hiyo iliyoandikwa na G. L. Mwakalukwa, ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, ikiomba msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Aidha, wakili huyo wa serikali alidai baada ya barua hiyo, Mgonja alimshauri Mramba atoe matangazo ya serikali yaliyokuwa yanatoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
Kwa kuzingatia ushauri huo, alidai kuwa Mramba aliidhinisha na kuweka saini matangazo ya serikali ya kusamehe kodi kampuni hiyo na yalitolewa bila kuzingatia ushauri wa TRA.

“Tunayo barua toka TRA kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ya Septemba 6, 2002, iliyoandikwa na Christine Shekidele, ikieleza matangazo hayo na hasara iliyopatikana, na tunaomba ipokelewe kama kielelezo kama upande wa mashitaka hauna pingamizi,” alidai.

Manyanda alidai kuwa, kati ya Novemba 2003 hadi 2007, Mgonja alikuwa anafanya malipo ya gharama kwenda kwa kampuni hiyo yaliyofikia sh 56,426,913,932.60 ambapo kiasi hicho kilicholipwa, ndicho kampuni hiyo ilipaswa kulipia kodi, na kuongeza kwamba kuna rundo la barua 44, zinazoonyesha malipo hayo na kuomba zipokelewe kama kielelezo.

Aidha, alidai Mramba, Yona na Mgonja walitoa maelezo ya ungamo, na walikiri kila mmoja kwa nafasi yake kwamba walishiriki kutenda makosa wanayoshitakiwa nayo na kuiomba mahakama hiyo ipokee maungamo ya washitakiwa hao.

Hata hivyo, mawakili wote walipinga mahakama isipokee maungamo hayo kwa madai kuwa wateja wao hawajawahi kuungama sehemu yoyote.

Hali hiyo ilisababisha kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Utamwa, kutaka vielelezo vyote vilivyobishaniwa na upande wa mashitaka, visipokelewe na jopo lake hadi hapo upande wa mashitaka utakapoanza kuleta mashahidi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Septemba 17,2009

No comments:

Powered by Blogger.