Header Ads

MRAMBA,YONA WAWEWESEKA KORTINI

Na Happiness Katabazi

HALI ya mambo katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake wawili, imeanza kubadilika baada ya washitakiwa hao kukubali maelezo kuwa waliwahi kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) na kutoa maelezo baada ya juzi kuyakana.

Washitakiwa hao walifikia uamuzi huo jana baada ya kuongozwa na mawakili wao, Hurbert Nyange, Msuya na Profesa Leonard Shahidi, Joseph Tadayo na Peter Swai, kukiri maelezo hayo yaliyotolewa na mawakili wa upande wa serikali.

Jana upande wa utetezi ulikuwa ukijibu hoja za upande wa serikali ambazo jana waliziwekea pingamizi.

Wakijibu hoja hoja, mawakili wa utetezi, walianza kwa kukubali kwamba wateja wao walitoa maelezo katika taasisi hiyo ila hawajawahi kukiri kwamba walitenda kosa hilo.

“Nakubali pia mteja wangu Mramba anakubali alipata kusailiwa na PCCB na akatoa maelezo ila ninaomba ieleweke alitoa mawelezo si kukiri kosa,”alidai wakili Nyange.

Juzi wakili Mwandamizi Fredrick Manyanda aliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao na kudai kabla ya kufikishwa mahakamani walihojiwa na taasisi hiyo na kukiri kutenda kosa, ambapo mawakili wa utetezi walikanusha na kudai wateja wao hawajahi kuhojiwa mahala popote.

Aidha, mawakili hao wa utetezi walikubali wateja wao walikuwa ni viongozi wenye nyadhifa kubwa serikali na wanakubaliana kwamba walipaswa kuwa waadilifu, waaminifu na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wa wakili Nyange, alieleza kuwa Mramba aliombwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, marehemu Daud Balali ruhusa ya kutia saini mkataba wa kampuni Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation.

Mramba pia alikubali alimwandikia barua mshitakiwa wa pili (Yona) kwamba katika makisio ya matumuzi ya fedha za serikali mwaka 2003/2004 hakukutengwa fungu la kumlipa mkaguzi wa dhahabu ambaye ni kampuni hiyo.

Kuhusu wakili wa mshitakiwa watatu, Profesa Shaidi, alidai kuwa Mgonja anakubali alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha mwaka 2002-2008 na kuyakana maeneo mengine.

Kesi hiyo imeahirishwa haod Septemba 22 mwaka huu kwa ajili ya upande wa mashitaka kuanika idadi ya mashahidi wake na vielelezo vitakavyotumika wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 18,2009

No comments:

Powered by Blogger.