Header Ads

'HAPPY BIRTHDAY' JWTZ

Na Happiness Katabazi

‘HAPPY birthday to you, happy birthday to you.
‘Happy birthday Tanzania People’s Defence Forces (TPDF), happy birthday to you’.


Naamini Watanzania wote tunakumbuka Septemba mosi mwaka huu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilitimiza miaka 45 baada ya kuundwa mwaka 1964, baada ya kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na jeshi la kikoloni la King’s African Rifles (KAR) lililovunjwa baada ya machafuko ya Januari 1964.

Tarehe hiyo wakati jeshi letu lilikuwa likitimiza miaka hiyo, pia ndiyo ilikuwa ni siku ya hitimisho la maadhimisho yaliyoanza takriban wiki moja iliyopita katika viwanja vya Jeshi la Anga, Ukonga Dar es Salaam.

JWTZ ilihitimisha kwa kuweka wazi silaha zake mbalimbali za kivita pamoja na kuonyesha mbinu na shughuli zinazofanywa na jeshi hilo ambalo katika kipindi hicho , nadiriki kusema pasipo shaka kwamba jeshi letu limepata mafanikio makubwa.

Wakati jeshi letu linatimiza umri huo, wanajeshi wamefanya mengi licha ya kushiriki kwenye ukombozi wa nchi nyingi za kusini mwa Afrika ili kuhakikisha zinakuwa huru kama ilivyo kwa Tanzania,JWTZ, imekuwa ni tanuri la kuyapika baadhi ya majeshi mengine ya nchi za Afrika.

Wananchi wenzangu waliopata fursa ya kutembelea maonyesho hayo watakubaliana nami kwamba jeshi letu sasa limekubali kubadilika na sasa limeanza kufanya kazi kisayansi na kiteknolojia na kwamba limekataa kuendelea kufanya kazi zake gizani na wasiwasi mithili ya mtu anayeoga barazani.

Kwa moyo mkunjufu napenda kutoa pongezi kwa wafanyakazi wote wa JWTZ na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwanza kwa kutimiza umri huo, pili, kwa uamuzi wao kukataa kuendelea kuficha dhana zetu za kivita ambazo zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi, kwani umri huo ni mkubwa ukilinganisha.

Sote ni mashahidi kila kukicha tumekuwa tukisia au kuona majeshi ya nchi nyingine za Afrika yamekosa mshikamano wake kweli na hivyo kufikia uamuzi wa baadhi ya wanajeshi wake kuasi na kuanzisha vikundi vyao haramu vinavyokuwa na maskani misituni na lengo la vikundi hivyo vya waasi limekuwa ni kupambana na jeshi linaloshika hatamu.

Huwa vimedhamiria kupindua serikali kisha watwae madaraka, jambo limeleta machafuko katika nchini nyingi lakini kwa kuwa Mungu bado anaipenda nchi yetu, JWTZ bado haijafikia hatua hiyo kwani wanajeshi wake wana mshikamano wa dhati kweli kweli.

Mapema wiki iliyopita niliposikia JWTZ imeanika silaha zake katika maonyesho hayo, iliniwia vigumu kuamini taarifa hizo.

Kwa sababu tangu nianze kufuatilia shughuli zinazofanywa na jeshi letu na binafsi nimezaliwa na kulelewa katika kambi ya jeshi, sikuwahi kusikia jeshi letu likithubutu kufanya maonyesho ya namna hii hadharani.

Kwa wale tunaopenda kutembelea vikosi, makambi ya JWTZ tumekuwa tukiona zana mbalimbali zikiwamo maghala ya silaha, ndege za kivita n.k, lakini pindi umuulizapo mwanajeshi hata kama ni rafiki yako kwamba ile ni silaha aina gani au komandoo naye anafamilia? Mwanajeshi ataishia kukujibu kwa mkato “fuata kilicho kuleta, hizo ni siri za jeshi hutakiwi kujua, umekuja kutupeleleza na utaruka kichurachura sasa hivi.”

Si siri majibu ya aina hiyo ambayo nilianza kuyapata tangu nikiwa mtoto hadi leo hii, ndiyo yalifanya wiki iliyopita niwe mgumu kukubali kwamba JWTZ imeanika silaha zake na wananchi wakajitokeza kwa wingi kushuhudia na wakapewa fursa ya kuuliza maswali na kujibiwa na wanajeshi wetu. Kweli Mungu mkubwa.

Wakati nikitoa pongezi kwa maadhimisho hayo, nitoe angalizo kwa jeshi letu kwamba bado wananchi wana imani nalo licha ya kuwapo kwa baadhi ya vitendo vya utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya askari wa chache, hivyo ambayo wakati mwingine vitendo hivyo vinalipaka matope jeshi.

Hata hivyo, hivi sasa jeshi letu limekuwa likitoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pindi wanapokamatwa wanajeshi kwenye matukio ya ujambazi na hatimaye wanafikishwa mahakamani.

Naunga mkono ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, katika maadhimisho hayo la kutaka raia wawe na uhusiano mwema na jeshi hilo. Lakini napenda kutoa angalizo kwamba uhusiano mwema kati ya pande hizo mbili uwe na mipaka na masilahi ya kwa nchi.

Uhusiano mwema huo usiwe ni ule wa baadhi ya wanajeshi wetu kutumia mafunzo ya kivita waliyoyapata kwenye vyuo vyao vya kijeshi, wakaanza kutoa mafunzo hayo kinyemela kwa baadhi ya wananchi watukutu ili mwisho wa siku waunde magenge ya kihalifu kwa maana ya mwanajeshi anatoa mafunzo kwa raia, silaha na kumcholea michoro ya kwenda kufanya ujambazi.

Naweza kusema kilichofanywa na JWTZ sasa, kinataka kulandana na kinachoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi chini ya Inspekta Jenerali Said Mwema, kwani tangu kamanda huyo ateuliwe kushika wadhifa huo kwa kushirikiana na askari wake wameweza kuanzisha mfumo mpya wa ‘Ulinzi Shirikishi’ na kwa hakika mfumo huo nadiriki kusema umeleta mafanikio ya kiutendaji katika jeshi hilo, kwakuwa wananchi ndio wanaoishi na wahalifu mitaani na maofisini.

Ni kazi ya Jeshi la Polisi kupitia makachero wake na kikosi chake cha kupambana na ujambazi ‘scopion’ ndiyo kinatakiwa kuwasaka majambazi, lakini Jeshi la Polisi kwa kutambua kwamba bila kushikirikisha raia haliwezi kufanikiwa, wakaamua kushirikisha raia na kweli leo hii tunalisikia Jeshi la Polisi likijitokeza hadharani kupongeza raia kwa kuwapa ushirikiano.

Lakini nimng’ate sikio Jenerali Mwamunyange, kwamba licha ya yeye kutoa wito kuendelezwa kwa mahusiano mema kwa raia vijana wake, namtaka aigeukie Kurugenzi ya Habari ya jeshi hilo, kwani baadhi ya waandishi wa habari nikiwemo mimi, tumekuwa tukiwasilisha maombi kwa njia ya maandishi katika kurugenzi hiyo ya kuomba turuhusiwe kufanya mahojiano na baadhi ya viongozi ukiwamo wewe, lakini katika hali ya kushangaza, kurugenzi yako imekuwa ikishindwa kutupatia majibu kwamba kiongozi tunayetaka kumhoji masuala mbalimbali yahusuyo jeshi ambayo yakijibiwa yatakuwa yanaelimisha taifa, tumekuwa hatujibiwi chochote.

Kitendo hiki kimekuwa kikitukera kwani waandishi wa jeshi pindi wanapokuja kwenye vyombo vya habari vya uraiani huwa wanapewa ushirikiano wa kutosha.

Na baadhi ya vijana wako ambao nimekuwa nikiwadadisi kuhusu hali hiyo kila mmoja wao kwa nafasi yake wamekuwa wakinijibu kwamba Kurugenzi ya Habari ya jeshi haipo huru hivyo na wao imekuwa ikiwawia vigumu kuwasilisha maombi yetu kwa maafande wao.

Ni rai yangu kwa Jenerali Mwamunyange na makamanda wako mlitazame hili, kwa mtazamo mpana, kwani wananchi wanahitaji kupata taarifa za jeshi lao ambapo taarifa hizo jeshi litahakikisha linatoa taarifa ambazo hazimnufaishi adui wa taifa letu.

Hii aipendezi na kwa namna nyingine hali hiyo ni aina fulani ya kukandamiza uhuru wa wananchi kupata habari za jeshi letu.

Watanzania hawawezi kuamini, kwa wiki moja sasa gazeti hili limeanza kuandika makala za habari za maadhimisho ya JWTZ, wananchi mbalimbali waliokuwa wakizisoma makala hizo wamekuwa wakipiga simu katika chumba chetu cha habari wakisema makala hizo zimewafunza mengi na wengine wakadiriki kuuliza taratibu za kujiunga na jeshi ni zipi lakini tukawaelewesha nafasi za jeshi huwa zinatangazwa kwenye vyombo vya habari.

Sasa kwa hali hiyo, tunaona kwamba kuna wananchi wanaopenda kupata taarifa mbalimbali za jeshi letu, wengine wanapenda kujiunga na jeshi hilo, kutembelea makumbusho ya jeshi lakini kwa sababu ya jeshi hili ama kwa kushindwa kuwa karibu na wananchi ama kwa kuandaa vipindi maalumu katika televisheni au redio au kuweka taarifa mpya mara kwa mara katika tovuti ya jeshi hilo ambalo lilizinduliwa na Luteni Jenerali Abdulahman Shimbo, pale Upanga Mess, ambapo nami nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari tuliohudhuria uzinduzi wa tovuti hiyo, kama wanavyofanya Jeshi la Polisi hivi sasa ndiyo kuna sababisha wananchi wengi kubaki gizani kuhusu utendaji wa jeshi letu.

Lakini cha kushangaza kama si cha kustaajabisha, licha ya JWTZ kuwa na wasomi wa taaluma ya teknolojia ya habari lakini tovuti ya jeshi hilo imekuwa haina vitu vingi, ama kuweka taarifa mpya mara kwa mara.

Natoa rai kwa Jeshi la Magereza nalo liige mfano huo ulioonyeshwa na majeshi mengine ili wananchi wafahamu majukumu yao kwani wananchi wengi wanaelewa jukumu lao ni kutunza mahabusu na wafungwa.Happy Birthday JWTZ.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Septemba 6, 2009

No comments:

Powered by Blogger.