Header Ads

KESI YA KIKATIBA YA LIYUMBA YATAJWA LEO

Na Happiness Katabazi

KESI ya Kikatiba iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania,Amatus Joachim Liyumba , akiomba mahakama hiyo itamke kwamba kifungu 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, kinapingana na Katiba ya Nchi,jana ilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo.


Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Kaijage, Zainabu na Projest Rugazia, hata hivyo jana iliweza kutajwa mbele ya jaji mmoja Rugazia, ambaye hata hivyo aliwaeleza mawakili wa mlalamikaji, Hudson Ndusyepo na Majura Magafu kwamba anaairisha kesi hiyo hadi Oktoba 9 mwaka huu kwaajili ya kuona siku hiyo kama upande wa mlalamikaji utakuwa umepewa majibu na upande wa mdaiwa.

Hata hivyo wakati Jaji Rugazia akiairisha kesi hiyo upande wa mdaiwa ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hakuwa umetuma mwakilikishi katika kesi hiyo hali iliyosababisha mahakamani kuwepo na mawakili wa mdaiwa na jaji Rugazia tu.

Liyumba ambaye hadi hivi sasa anaendelea kusota rumande kwaajili ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, alifungua kesi hiyo mapema Julai mwaka huu, na kwa mujibu wa hati yake ya madai katika kesi hii ya Kikatiba, anafafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, kina mtaka mtuhumiwa anayedaiwa kuiba zaidi ya sh milioni kumi,atoe fedha taslimu au hati ya nusu ya mali anayotuhumiwa kuiba mahakamani ,ndipo apate dhamana.

Kwa mujibu wa hati , Liyumba anaiomba mahakama hiyo itamke kifungu hicho kuwa kinapingana na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977, inayotamka bayana kwamba mtu asichukuliwe kuwa ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Aidha hati hiyo ya madai inadai kuwa kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, pia kinapingana na Ibara 17(1) ya Katiba ya Nchi, ambapo ibara hii inatamka bayana kuwa kila mtu ana haki ya kuwa huru.

Liyumba anadai hatua ya mtuhumiwa kutakiwa kutoa fedha taslimu au nusu ya mali wakati bado hajatiwa hatiani na kesi inayomkabili, ni wazi mshitakiwa anakuwa ameishahukumiwa jambo alilodai linakwenda kinyume na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Tanzania.

“Kwa sababu hizo tunaiomba mahakama hii,itamke kifungu hicho kuwa ni batili kwani kinakwenda kinyume na haki za msingi zilizoainishwa kwenye ibara hizo za Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama” ilisomeka hati hiyo.

Aidha Liyumba aliendelea kudai kuwa yeye kama Mtanzania ana haki ya kuwa huru kwa mujibu wa ibara hiyo, lakini hivi sasa ameshindwa kupata haki hiyo ya uhuru kwasababu kushindwa kuwasilisha fedha au hati ya nusu ya mali ya bilioni 110, mahakamani ili apate dhamana.

“Hivyo haki zangu kwa mujibu wa ibara hizo za Katiba zimenyang’anywa na kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa Janai, hivyo naiomba mahakama iliangalie na hilo wakati ikisikiliza kesi hii ya Kikatiba niliyofungua”.alidai Liyumba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 15,2009

No comments:

Powered by Blogger.