Header Ads

JAJI KATEKA AULA

Na Happiness Katabazi

JAJI wa Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari (ITLOS) yenye makao yake nchini Ujerumani, James Kateka, ambaye ni Mtanzania pekee katika mahakama hiyo, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Taasisi ya Wanasheria wa Kimataifa.

Taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya taasisi hiyo inaeleza Jaji Kateka anakuwa mjumbe wa kwanza kutoka nchi za Afrika Mashariki kuchaguliwa kujiunga na taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1873 nchini Ubeligiji.

Taarifa hiyo ambayo imethibitishwa na Jaji Kateka, ilisema wajumbe wengine katika taasisi hiyo ni pamoja na majaji wa mahakama za kimataifa, maprofesa wa vyuo maarufu duniani na wakuu wa vyombo vya utafiti wa sheria za kimataifa.

Aidha, ilisema Waafrika wengine waliochaguliwa kuwa wajumbe ni pamoja na Jaji Abdul Koroma wa Mahakama ya Dunia kutoka Sierra Leone, Jaji Thomas Mensah kutoka Ghana ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa ITLOS, Jaji Abdi Yusuf wa Mahakama ya Dunia kutoka Somalia na Profesa John Dugard kutoka Afrika Kusini.

“Jaji Kateka alichaguliwa katika raundi ya kwanza kwa kupata kura nyingi kuliko wajumbe wote waliochaguliwa, katika kikao kilichofanyika Naples, nchini Italia. Walikuwapo wagombea 28 na waliochaguliwa ni 11. Baadhi ya walioshindwa katika uchaguzi huu ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Dunia,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo inasema wajumbe wengine waliochaguliwa katika taasisi hiyo ni pamoja na majaji wa mahakama za kimataifa, maprofesa wa vyuo maarufu duniani na wakuu wa vyombo vya utafiti wa sheria za kimataifa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Septemba 11, 2009

No comments:

Powered by Blogger.