Header Ads

WIZI WA NMB TEMEKE

Watuhumiwa wengine sita wakamatwa

*Wakutwa na SMG moja, bastola mbili na risasi 52
*Yumo mwanajeshi mstaafu raia wa nchini Burundi
*Wawili wafikishwa kortini wakiwa hoi kwa kipigo

Na Happiness Katabazi

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watuhumiwa wengine sita, akiwemo raia wa Burundi, wakiwa na silaha tatu, zinazodaiwa kutumika katika tukio la ujambazi, lililotokea katika Benki ya Microfinance (NMB), tawi la Temeke, Julai 31, mwaka huu.
Kati ya watuhumiwa sita waliokamatwa hivi karibuni, wawili kati yao, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa zaidi ya sh milioni 60 na kusababisha vifo vya askari wawili waliokuwa lindoni siku ya tukio.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kunafanya idadi ya waliokwishakamatwa kuhusina na tukio hilo la ujambazi wa kutumia silaha nzito za kivita lililotikisa nchi, kufikia 17.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watuhuniwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti, ikiwemo jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Pwani.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Richard Muhonza (29), raia wa Burundi aliyewahi kuwa mwanajeshi wa nchi hiyo, Willibert Ugini (22), mkazi wa Arusha, Selemani Nzowa (33), na Halima Mvungi (49), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam. Wengine wawili majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

“Msako huu ni mkali na wa aina yake, ambao unaendelea nchi nzima ili kuwabaini wote waliohusika kwa njia moja au nyingine katika ujambazi uliofanyika NMB Temeke,” alisema Kamanda Kova.

Aidha, alizitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni SMG namba AB 2763836, ikiwa na risasi 40, magazini moja yenye risasi 30 na nyingine risasi 10, bastola mbili, moja ikiwa imetengenezwa China, yenye namba 073095 na risasi mbili na nyingine ni aina ya Maknov, iliyokuwa na risasi sita kwenye magazini na risasi nyingine 10 zilizokutwa kwenye paketi ya sigara iliyofichwa kwenye soksi.

“Majambazi wote wamekamatwa katika operesheni ya pamoja iliyofanyika kwa ushirikiano wa askari wa Mkoa wa Pwani, vikosi maalum vya kudhibiti uhalifu, wananchi na Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,” alisema Kova.

Tayari watuhumiwa wawili kati ya sita waliotangazwa jana, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuungana na wenzao wanane, kujibu mashitaka yanayowakabili.

Mbele ya Hakimu Mkazi Binge Mashabala, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Richard Lucas Mahuza maarufu Leonard ambaye ni raia Burundi na Selemani Omar Nzowa.

Kimaro alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na makosa mawili ya mauaji ambapo kwa pamoja na wenzao wanane waliofikishwa mahakamani hapo hivi karibuni, wanadaiwa kuwa Julai 31, mwaka huu, katika benki ya NMB, tawi laa Temeke, walimuua Seif Abdallah.
Katika shitaka la pili, Kimaro alidai kuwa mnamo tarehe na muda kama huo, washitakiwa hao na wengine ambao walishafikishwa mahakamani hapo hivi karibuni, katika tawi la NMB Temeke, walimuua askari polisi mwenye namba E329, Koplo Joseph.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.

Hata hivyo, watuhumiwa hao waliingia mahakamani hapo wakiwa hoi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kipigo, kwani walishindwa kutembea na kulazimika kutembea kwa msaada wa askari polisi.

Hata walipoingizwa ndani ya mahakama hiyo, watuhumiwa hao walishindwa kukaa na kulazimika kulala kwenye viti.

Walipopandishwa kizimbani na kuanza kusomewa mashitaka, watuhumiwa hao walimwomba hakimu awape kibali cha kwenda kutibiwa kwa madai kuwa wana maumivu makali mwilini, yaliyotokana na kipigo walichokipata.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi keshokutwa na hakimu aliagiza washitakiwa wakapatiwe matibabu wakiwa gerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 8,2009

No comments:

Powered by Blogger.