Header Ads

MED MPAKANJIA AFARIKI DUNIA

Maelfu wafurika nyumbani kwake Sinza
Msiba wake waibua simanzi ya kifo cha Amina

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA mume wa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), marehemu Amina Chifupa, Mohamed Mpakanjia, amefariki dunia.


Mpakanjia, ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu, amefariki dunia jana majira ya saa nane mchana katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya hospitali hiyo aliyofia mkewe Amina miaka mitatu iliyopita, vilisema kuwa Mpakanjia, maarufu kwa jina la Med, alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo kwa matibabu.

Kwa mujibu wa habari hizo, mara baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo, Mpakanjia aliingizwa kwenye wodi ya watu mashuhuri (VIP), ambako amekuwa akilazwa mara kwa mara na kupatiwa matibabu.

“Ni kweli Mpakanjia amefariki dunia na alifikishwa hapa mchana huu na ndugu zake, lakini alionekana kuzidiwa na ugonjwa, kwani hata baada ya kupokewa na kuanza kutibiwa, aliendelea kuzidiwa na baada ya muda mfupi, alifariki dunia,” alisema mmoja wa wauguzi hospitalini hapo na kuongeza kuwa mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Ndugu wa karibu wa Mpakanjia, waliiambia Tanzania Daima kuwa Mpakanjia amekuwa akifika hospitalini hapo na kutibiwa na wakati mwingine kulazwa kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua tangu alipofariki dunia mkewe na hali hiyo ilidaiwa kutokana na msongo wa mawazo, hasa ikizingatiwa kuwa mkewe alifariki siku chache tu baada ya wanandoa hao kutalikiana.

Akizungumzia kifo hicho, baba wa marehemu Amina, mzee Gabriel Chifupa, alithibitisha kutokea kwa kifo cha mkwewe na kuongeza kuwa msiba utakuwa nyumbani kwa marehemu Mpakanjia, Sinza Mori, Dar es Salaam.

Mpakanjia amekuwa maarufu, lakini umaarufu wake ulizidi hasa baada ya kumwoa Amina, na ndoa ya wawili hao kutawala kwenye vyombo vya habari.

Amina alifariki dunia Juni 27, mwaka 2007, siku ya kilele cha maadhimisho ya Kupambana na Madawa ya Kulevya Duniani.

Enzi za uhai wa wanandoa hao, walibahatika kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Rahman.

Marehemu Amina Chifupa, ambaye alikuwa mbunge kijana, kitaaluma alikuwa mtangazaji na mwandishi wa habari na alifanikiwa kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kupitia UVCCM.

Katika kipindi kifupi alichokaa bungeni, Amina alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na hoja zake nzito, katika kutetea masilahi ya vijana na kukemea rushwa na kuvalia njuga mapambano dhidi ya dawa za kulevya

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 15,2009

No comments:

Powered by Blogger.