Header Ads

WALIOKAIDI AGIZO LA EWURA WATOZWA FAINI MIL.10/-

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es salaam, imewahukumu kifungo cha miezi sita nje na kulipa faini ya sh milioni 10 wafanyabiashara wawili wa vituo vya mafuta baada ya kupatikana na hatia ya kukaidi amri ya Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ya kufunga vituo vyao vilivyokuwa vikiuza mafuta yaliyochachuka.

Wafanyabiashara hao ni Mohamed Twalib Nahdi na ndugu yake Abdulatif Twalib Nahdi ambao wote ni wakazi wa Morogoro.

Akitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Jaji Thomas Mihayo, alisema amekubaliana na hoja zilizowasilishwa na Wakili wa Ewura, James Kabakama, kwamba amri iliyotolewa na mamlaka hiyo Septemba 19, 2008 inapaswa kuheshimiwa.

Jaji Mihayo alisema yeyote atakayekiuka amri ya mamlaka hiyo atachukuliwa hatua kali za kisheria na kwamba ametoa adhabu nafuu kwa wafanyabiashara hao, ili waweze kujirekebisha.

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Mihayo amewataka wafanyabiashara hao kutotenda kosa kama hilo ndani ya miezi sita na akawapa wiki mbili wawe wameshalipa faini ya sh milioni tano kila mmoja. Vituo vya mafuta anavyomiliki Abdulatif Twalib Nahdi ambavyo vimefungiwa ni Kobil Msamvu Petrol Station na Abdulatif Petrol Station.

Aidha, Mohamed Twalib Nahdi naye anamiliki vituo vya Mohamed Twalib Petrol Station, Oilciom Kihenda Petrol Station na Mohamed Twalib Oilcom Petrol Station.

Ilidaiwa kuwa EWURA walifanya ukaguzi wa vituo vyote vya mafuta mkoani Morogoro kati ya Septemba 13 na 14 mwaka jana na kubaini vituo vya wafanyabiashara hao kuwa vilikuwa vinauza mafuta yaliyochakachuliwa.

Kutoka na hali hiyo, EWURA, iliwataka wafanyabiashara hao kufunga vituo vyao na kujieleza kwa nini wasichuliwe hatua kwa kuuza mafuta yaliyochakachuliwa. Hata hivyo, wafanyabiashara hao walikiuka amri hiyo na kuendelea na shughuli zao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Agosti 31, 2009

No comments:

Powered by Blogger.