Header Ads

KESI YA MRAMBA,YONA YAIBUA MAPYA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, Godwin Nyero (48), ameendelea kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kuwa, waziri akiona ushauri uliotolewa na mtaalamu haufahi, anaweza kuukataa.


Nyero ambaye alikuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Masuala ya Uchumi katika Wizara ya Nishati na Madini, alitoa maelezo hayo jana mbele ya jopo la mahakimu wakazi; John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika wakati akijibu maswali aliyokuwa akihojiwa na Wakili Cuthbet Tenga na E. Msuya ambao wanamtetea mshitakiwa wa pili, Daniel Yona na Profesa Leonard Shahidi, anayemtetea mshitakiwa wa tatu, Gray Mgonja.

Shahidi huyo ambaye pia alikuwa mjumbe wa kamati ya kuandaa mchakato wa kuileta kampuni ya ukaguzi wa madini nchini ya Alex Stewart Government Business Corporation, alidai kuwa baada ya kumalizika kwa mchakato huo, alimpelekea dokezo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Yona kutaka serikali isiipe kazi kampuni hiyo.

Hata hivyo, mawakili hao wa mshitakiwa wa pili walilazimika kuiomba mahakama isitishe kuendelea kumhoji shahidi huyo kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuleta nyaraka za mkataba wa serikali na kampuni hiyo ambazo walidai zingeletwa mahakamani hapo ili zitumike kumuuliza maswali.

Ombi hilo lilikubaliwa na jopo hilo ambalo liliuamuru upande wa mashitaka ulete nyaraka hizo Novemba 16 mwaka huu ili shahidi huyo aendelee kuhojiwa na mawakili hao.
Mahojiano kati ya shahidi huyo na mawakili hao yalikuwa hivi:

Wakili: Kwanini mapendekezo yako ya kuikataa kampuni hiyo hukutoa nakala kwa Katibu Mkuu na Kamishna wa Madini?
Shahidi: Katibu Mkuu nilimpatia taarifa kwa mdomo na Kamishna wa Madini sikumpatia taarifa.
Wakili: Ieleze mahakama mantiki ya kumpa waziri taarifa kwa maandishi, kamishna wa madini usimpatie taarifa na katibu mkuu umpatie kwa mdomo.
Shahidi: Mh! Ni taarifa tu ambayo nilimpa ushauri waziri (Yona) autumie yeye kama ataona unafaa na akiona haufahi pia kiongozi huyo wa wizara alazimiki kuniambia mimi mtaalamu.
Wakili: Waziri akiona ushauri wako wewe mtaalamu haufahi anakuwa amekosea?
Shahidi: Hajakosea.
Wakili: Kamishna wa Madini kama ulimwambia ushauri huo kwa mdomo alikujibu nini?
Shahidi: Alinijibu nimwandikie dokezo waziri wangu.
Wakili: Ni kweli kwamba kulikuwa na ulazima wa serikali kuleta mkaguzi wa dhahabu hapa nchini kufuatia malalamiko ya wabunge na wananchi kwamba madini yetu yanaibwa?
Shahidi: Ni kweli.
Wakili: Malalamiko ya wabunge yalijitokeza bungeni?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Serikali ilivyoanza mchakato wa kuipata kampuni hiyo ilikuwa inatekeleza matakwa ya Bunge?
Shahidi: Hilo sifahamu.
Wakili: Kamati yenu ya watu wanne iliteuliwa rasmi lini?
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Yawezekana ilikuwa Septemba 12, 2002?
Shahidi: Yawezekana.
Wakili: Mwenyekiti wa kamati yenu alikuwa nani?
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Katibu Mkuu wa kamati hiyo alikuwa nani?
Shahidi: Sikumbuki ila najua wajumbe wenzangu watatu walitoka BoT.
Wakili: Hao wajumbe watatu walikuwa wataalamu wa mambo gani kwenye hiyo kamati yenu kwa sababu wewe ulishaiambia mahakama ulikuwa mtaalamu wa madini?
Shahidi: Sifahamu.
Wakili: Kabla ya kwenda kwenye hiyo kamati mlipewa mwongozo wa kufanya kazi?
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Mlikuwa mnatumia utaratibu gani wa kufikia uamuzi?
Shahidi: Consensus.
Wakili: Ni kweli kwamba na wewe ulikuwa unafikia consensus hiyo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Consensus inafikiwa baada ya majadiliano ya wajumbe wanne?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Juzi uliiambia mahakama kwamba masuala yenye utata mliyapeleka kwa gavana na yasiyo na utata kwenye kamati yenu yaliendelea kujadiliwa?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Hiyo kamati yenu ilifanya kazi yake kwa uhuru bila kuingiliwa na washitakiwa waliopo kizimbani?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwanini ulipeleka mambo msiyokubaliana kwa Waziri Yona badala ya Gavana?
Shahidi: Kwa maelekezo ya waziri alivyonituma kazi, nikitoka kwenye kamati hiyo niwe namletea taarifa.
Aidha, shahidi wa pili, Betha Msoka (44), ambaye ni mwanasheria kitaaluma na kati ya mwaka 1992-2003 alikuwa ni ofisa mwandamizi msimamizi wa fedha toka Wizara ya Fedha, aliiambia mahakama kuwa mwaka 2003 alipewa maelekezo na mkuu wake kitengo cha huduma ya sheria wizarani hapo, Agness Bukuku ambaye sasa ni Msajili wa Hazina, akaiwakilishe wizara katika majadiliano ya mkataba wa kampuni hiyo ya ukaguzi wa madini na wizara yake.
Soka alidai aliudhuria majadiliano hayo yaliyoshirikisha wataalamu toka wizara ya Fedha,Nishati na Benki Kuu na majadiliano yalihusu mkataba wa mkaguzi wa madini ya dhahabu katika ya serikali ya Tanzania na Alex Stewart Gorvement Corporation ya Marekani na kwamba vikao vilijadili rasimu ya mkataba huo na baada ya kupitia walibaini vipengele vingi vya kitaalamu vinavyohusu Kodi na Ada.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Shahidi huyo na Wakili Mkuu wa Serikali Stanslaus Boniface:
Wakili:Hayo mambo mawili yalishughulikiwa vipi katika majadiliano yenu?
Shahidi:Suala la Ada lilishughulikiwa na Wizara ya Nishati.Na mkataba huo kwangu ulikuwa ni mgeni kwangu kwasababumimi nilikuwa natokea Wizara ya Fedha ,nilitizama kipengele cha kodi kwa makini.
Wakili:Baada ya kutizama kwamikini vipengele hivyo vilisema nini?
Shahidi:Vilikuwa vinatoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo na wataalamu wake.
Wakili:Wewe ulishughulikia vipi jambo hilo?
Shahidi:Mimi niliwaeleza wajumbe wenzake kwamba mwenye mamlaka ya mwisho ya kusamehe kodi ni Waziri wa Fedha kwahiyo hadi tupate ridhaa toka kwa waziri.
Wakili:Baada ya kuwaeleza hilo, wenzio majibu yao yalikuwaje?
Shahidi:Ni kitu ambacho waliamua kukiweka kando hadi Waziri atoe idhini.
Wakili:Wewe kama mwakilishi wa wizara ya Fedha ulifanyanini?
Shahidi:Nilimjulisha mkuu wangu wa kazi(Agnes Bukuku) kwa njia ya maandishi na baada ya kumueleza alikubaliana nami na barua ikaandikwa kwenda TRA kwaajili ya kuhusu vipengele vile viwili yaani vya ada na kodi.
Wakili:Namna gani ulishughulikana na kampuni hiyo ya ukaguzi?
Shahidi:Sikushiriki majadiliano tangu siku barua ya ushauri ilipopelekwa TRA wala sikujua nini kiliendelea kwani sikuitwa tena kwenye kikao.
Wakili:TRA walijibuje hiyo barua?
Shahidi:Ilisema kampuni hiyo haistahili kusamehewa kodi.
Wakili:Katika Timu yenu ya majadiliano ya mkataba huo alikuwepo mwakilishi toka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali?
Shahidi:Hakuwepo.
Wakili:Soma hiki kielelezo cha kwanza, katika aya ya tano inasomekaje?.
Shahidi:Kielelezo hiki ni dokezo la Yona alilomwandikia Rais Mkapa,Machi 3 mwaka 2003,kinasomeka: ‘Kabla ya BoT haijachagua kampuni inayofaha itazingatia mapato ya serikali yasipungue na wawekezaji wasiumie kiasi cha kukata tama kuwekeza zaidi kwenye madini .Aidha tutapa ushauri toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wakili:Soma tena na kielelezo hiki cha tatu kinasomekaje?
Shahidi:Hiki ni barua aliyoiandika Yona kwenda kwa rais Mkapa Mei 11,2003 na kinasomeka hivi: ‘Baada ya kukaandikia dokezo langu Machi 3 mwaka 2003 kuhusu umuhimu wa kuanzisha ukaguzi wa dhahabu inayochimba na kuuzwa nchi za nje , majadiliano kati ya Wizara ya Nishati.Fedha,BoT na Mwanasheria Mkuu wa Serikali yanaendelea vizuri.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, inaendelea tena ambapo mawakili wa utetezi wataanza kumhoji shahidi huyo wa pili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi Novemba 5,2009

No comments:

Powered by Blogger.