Header Ads

MKAPA ALIPULIWA MAHAKAMANI

.YADAIWA ALITOA IDHINI KULETWA ALEX STEWART
.SHAHIDI ADAI YONA ASINGEKATAA AGIZO LA RAIS
Na Happiness Katabazi

RAIS mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa anadaiwa kuandika barua iliyomtaka aliyekuwa Waziri wa NiShati na Madini, Daniel Yona kuharakisha mchakato wa kuileta Kampuni ya Alex Stewart Government Business Corporation kuja nchini kufanya ukaguzi wa dhahabu.


Yona ni mshitakiwa wa pili katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7. Pamoja nae washitakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gray Mgonja.

Kuhusika kwa Mkapa kulibainishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, na shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri, Godwin Nyero (48) mbele ya jopo la mahakimu wakazi; John Utamwa, Saul Kinemela na Sam Rumanyika, wakati akihojiwa na wakili wa utetezi, Hurbet Nyange.

Nyero, aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Masuala ya Uchumi katika Wizara ya Nishati na Madini, alitoa maelezo hayo baada ya wakili Nyange kumtaka asome kwa sauti kielelezo namba 10 kilicholetwa mahakamani hapo na upande wa mashitaka, ambacho ni barua iliyotoka kwa Mkapa akimjibu Yona.

“Kwa mujibu wa barua ya Rais Mkapa aliyomjibu Yona, inasomeka kama ifuatavyo: Nakubaliana na ombi lako Waziri Yona na ninataka wizara yako iendelee na mchakato huo haraka,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.

Shahidi huyo, jana alionekana kuzungumza baadhi ya maelezo mapya yaliyokuwa yakitofautiana na aliyoyatoa juzi wakati akiongozwa na wakili wa mashitaka. Alidai kuwa licha ya yeye kumpatia mapendekezo yaliyokataza serikali isifanye haraka kuikubali Kampuni ya Alex Stewart kwa sababu haikuwa na mtaji wa kutosha, Yona asingeweza kukataa maagizo ya Rais Mkapa yaliyomtaka kuendelea na mchakato wa kuileta kampuni hiyo nchini.

Aidha, mahojiano kati ya shahidi huyo na wakili wa utetezi yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Juzi ulitamba hapa mahakamani kwamba wewe ulikuwa mtaalamu na ulitoa ushauri wako kwa Yona wa kuikataa hiyo kampuni, lakini mshitakiwa alipuuza. Je, ilikuwaje serikali ilikubali wewe ujiuzulu na isikatae ombi lako kwa gharama yoyote?

Shahidi: Sijui. Ninachofahamu mimi nilijiuzulu.

Wakili: Katika kamati yenu, wewe ulishauri nini kuhusu Alex Stewart?

Shahidi: Nilishauri isipewe tenda.

Wakili: Kuna andiko lolote uliloandika kwenye kamati hiyo kwamba hukubaliani na kampuni hiyo kupewa tenda?

Shahidi: Mh! Sina andiko la kuthibitisha hilo.

Wakili: Tutaamini vipi kama ushauri huo wa kitaalamu ndiyo huo huo ulimshauri Yona?

Shahidi: (Kimya)

Wakili: Sasa Yona alikosea nini kama si wewe ndiye uliyeisaliti kamati yako?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kwa hiyo unataka kusema walioisababishia serikali hasara ni wajumbe wenzako wa kamati?

Shahidi: Siwezi kusema hilo.

Wakili: Hii asilimia 1.9 ya malipo ya ada kwa kampuni hiyo, kamati yenu iliikubali?

Shahidi: Hatukuipitisha, tulifanya ulinganisho.

Wakili: Mlipitisha kampuni hiyo ilipwe ada asilimia ngapi?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Baada ya kamati yenu kuandaa ‘proposal’, kulifanyika tathimini ya kuipata kampuni hiyo, je, wewe ulishiriki kufanya tathimini kwa kampuni hizo mbili?

Shahidi: Nilishiriki.

Wakili: Tathimini ilionyesha Alex Stewart Government Business Corporation ilipata pointi ngapi?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Nakukumbusha, kampuni hizo mbili mlizipa alama za ushindi, Alex Stewart mliipa asilimia 92.9 na Walker & World mliipa asilimia 73.3.

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Ukiwa mtaalamu wa masuala ya madini, ni kampuni gani hapo ilikuwa na mafanikio zaidi ya kupata tenda?

Shahidi: Alex Stewart.

Wakili: Kamati ilipendekeza ni kampuni gani ipewe kazi ya kukagua dhahabu?

Shahidi: Alex Stewart.

Wakili: Wewe ulikuwepo kwenye kamati wakati pendekezo hilo linatolewa?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Kwa mujibu wa kielelezo cha kumi, baada ya kamati yenu kutoa pendekezo hilo kwa serikali, wewe uliwazunguka wajumbe wa kamati yako na ukaenda peke yako kwa Yona na ukamwambia kampuni hiyo isipewe kazi, si ndiyo?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Wewe unajua Yona ni mtu mmoja katika serikali hii, ni kwa nini ulifanya hivyo?

Shahidi: (Kimya)

Wakili: Huu mkataba wa serikali na kampuni hiyo si ulitokana na mapendekezo ya kamati yenu?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Ndiyo maana awali wakati naanza kukuhoji nilikwambia wewe wakati unafanya kazi Wizara ya Nishati na Madini ulikuwa hupikiki chungu kimoja na wenzio. Mwanzo uliiambia mahakama kamati yenu ilipendekeza kampuni ipewe kazi, sasa hivi unasema ilikataa isipewe kazi.

Shahidi: Kimya( wananchi wanaoudhuria kesi hiyo wakaangua vicheko).

Wakili: Kwa hiyo shahidi umeanza siyo kubadili maelezo yako kwamba kamati yenu ilipendekeza kampuni hiyo ipewe tenda?

Shahidi: Sikumbuki kamati kwamba tulipendekeza au tulisema imeshindwa kutimiza vigezo.

Wakili: Ni mapendekezo gani mlipeleka kwa Gavana marehemu Daud Balali kuhusu kampuni hiyo?

Shahidi: Mapendekezo kwamba Alex Stewart ilishinda.

Wakili: Baada ya kamati yenu kumpelekea mapendekezo hayo, mlitegemea gavana afanye nini?

Shahidi: Sijui (watu wakaangua vicheko)… Tulichotegemea aiite kampuni hiyo na aieleze imeshinda tathimini na wakubaliane namna ya kufanya kazi na makubaliano hayo yawekwe kwenye mkataba.

Wakili: Ndugu shahidi, ulishawahi kufanya utafiti wa madini katika nchi nyingine?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Unajua hupaswi kuzungumzia kitu kama hujakifanyia utafiti, sasa ni kwanini unadai uliandika pendekezo kwa Yona kwamba tenda ya kampuni hiyo isitishwe na badala yake ufanyike utafiti katika nchi nyingine kwanza?

Shahidi: (Kimya)

Wakili: Kuna mahali popote wewe binafsi uliwahi kutoa taarifa kwa gavana kwamba hukubaliani na wajumbe wenzio?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Mapendekezo yenu yaliyopelekwa kwa gavana uliwahi kuyaona?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Wewe ulimshauri Waziri Yona kwamba hakuna haraka ya kuingia mkataba na kampuni hiyo. Nakuuliza akiambiwa na wakubwa wake aruhusu kampuni hiyo ije nchini kufanya kazi angekataa?

Shahidi: Hapana asingeweza kukataa.

Wakili: Nakwambia sasa Yona alimuandikia barua rais wa wakati huo Benjamin Mkapa akimuarifu kuhusu serikali kuitaka kampuni hiyo ije ifanye kazi ya ukaguzi hapa nchini na rais alimjibu barua hiyo ambayo naomba uisome kwa sauti.

Shahidi: Inasomeka kwamba. “Nakubaliana na taarifa yenu na endeleeni na mchakato wa kuipata kampuni hiyo haraka.”

Wakili: Sasa kama Rais Mkapa alimuagiza Yona aendelee na mchakato, waziri angeendelea kusikiliza ushauri wako wa kukataa serikali isitishe tenda na kampuni hiyo wakati wewe ni mdogo kimadaraka?

Shahidi: Ni kweli Yona asingeweza kukataa agizo la Mkapa.

Wakili: Uliwahi kuusoma ule mkataba?

Shahidi: Hapana, nilisoma rasimu ya mkataba na wala sikuona kipengele kilichonitatiza isipokuwa kipengele cha ada ya asilimia 1.9.

Wakili: Unavifahamu hivi vitabu?

Shahidi: Ndiyo, ni kumbukumbu ya majadiliano katika Bunge.

Wakili: Majadiliano ya Bunge mwaka 2004 uliyafuatilia?

Shahidi: (Kimya)

Wakili: Chukua hiki kitabu kimoja fungua ukurasa wa 25, kisha usome kwa sauti ili mahakama ijue unasema nini.

Shahidi: Unasomeka miswaada ya sheria ya nyongeza na matumizi ya fedha mwaka 2004.

Wakili: Kwa hiyo kuna uwezekano wa kufanyika ‘supplementary’ bajeti kabla ya mwaka wa fedha kuisha?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Juzi uliiambia mahakama bajeti ya mwaka 2003/2004, haikutengwa bajeti ya malipo ya kampuni hiyo na kwamba Benki Kuu na wizara ilitumia njia zake kutafuta fedha kuilipa kampuni hiyo. Je, nikikwambia hii hansad inasema bajeti hiyo ilikuwa na nyongeza ya bajeti?

Shahidi: Ukisema hivyo ina maana hauna bajeti.

Wakili: Kwa hiyo ukipata nyongeza ya bajeti unakuwa hauna bajeti?

Shahidi: Unakuwa na bajeti.

Wakili: Zoezi la kuileta kampuni hiyo nchini lilikuwa halina faida yoyote?

Shahidi: Kifedha halina faida na kule kuthibitisha hakuna wizi wa madini yetu ni faida.

Wakili: Na nikikwambia sababu ya kampuni hiyo kushindwa kufanya kazi yao sawasawa ilitokana na kampuni za uchimbaji wa madini kukataa kukaguliwa?

Shahidi: Sijui.

Wakili: Unakumbuka aliyekuwa Waziri wa Fedha (Mramba) aliziita kampuni za uchimbaji wa madini nchini akazionya na kuzitaka zikubali kukaguliwa na kampuni hiyo?

Shahidi: Sawa kabisa Waziri wa Fedha alitenda hilo.

Wakili: Unakumbuka kampuni hiyo ilikataa taarifa za mahesabu za kampuni zinazochimba dhahabu hapa nchini zilizoonyesha zimepata hasara?

Shahidi: Hiyo sikumbuki.

Wakili: Unakumbuka sababu za serikali kuongeza mkataba na kampuni hiyo mwaka 2005 hadi 2007 ili iwezeshe kampuni hiyo kumaliza kazi yake ya ukaguzi iliyocheleweshwa na kampuni zilizokataa kukaguliwa?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili: Kwa hiyo serikali iliingia hasara miaka miwili kwa sababu kampuni hizo zilikataa kukaguliwa, halafu wewe leo hii unatetea kampuni hizo hazijaitia hasara serikali?

Shahidi: Hiyo ni sababu mojawapo.

Wakili: Unajua nyaraka 6,000 zilifichwa na kampuni hizo za uchimbaji ili Kampuni ya Alex Stewart isizikague?

Shahidi: Ni zaidi ya 6,000.

Wakili: Hivi una habari hizo nyaraka zaidi ya 6,000 zilifichwa kwa ajili ya kukwepa kodi?

Shahidi: Hilo nalijua.

Wakili: Kama hilo unalijua asante sana kwani hizo nyaraka zilizofichwa ziligunduliwa na Kampuni ya Alex Stewart.

Shahidi: (Kimya)

Wakili: Unaifahamu Kampuni ya Plaser Dom na Resolut zilikuwa zinachimba madini, na katika ukaguzi Kampuni ya Alex Stewart iligundua zimeshindwa kuthibitisha matumizi ya dola 160 kwa sababu nyaraka zilikuwa Makao Makuu ya kampuni zao na si hapa nchini, nje ya nchi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Unajua nyaraka za kampuni za madini zinatakiwa zibaki hapa hapa nchini?

Shahidi: Najua.

Wakili: Wataalamu wenzio wametoa taarifa serikalini, wamesema takwimu za upatikanaji wa dhahabu ni za uongo, lakini wewe unasema takwimu za upatikanaji ni sahihi, tuamini lipi?

Shahidi: (Kimya)

Wakili: Hapa ninalo dokezo lililopokelewa na Spika wa Bunge kwamba Alex Stewart iligundua upungufu mkubwa katika uchimbaji na usafirishaji dhahabu, sasa unataka kusema kamati ilikosea?

Shahidi: Najua, ila siwezi kulisemea hilo.

Wakili: Juzi, uliiambia mahakama hii tukufu kwamba Alex Stewart haikutoa mafunzo kwa Watanzania?

Shahidi: Ni kweli ila kwa upande fulani.

Wakili: Una ushahidi wa hilo unalosema?

Shahidi: Sina hakika.

Wakili: Kama huna uhakika ni kwanini unadai kampuni hiyo haikutoa mafunzo kwa Watanzania?

Shahidi: (Kimya, watu wakaangua vicheko)

Wakili: Sasa tumepokea taarifa, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Arthur Mwakapugi, kupitia gazeti la The Citizen aliuambia umma kwamba hivi sasa Tanzania inatumia wataalamu Watanzania waliopata mafunzo ya ukaguzi wa madini toka Kampuni ya Alex Stewart. Je, utabisha?

Shahidi: Sibishi.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Utamwa, aliahirisha kesi hiyo hadi leo na kumtaka shahidi huyo wa kwanza afike mahakamani ili endelee kuhojiwa na mawakili wa utetezi kwa kuwa jana kwa saa nne mfululizo alihojiwa na wakili Nyange, ambaye anamtetea Mramba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 4,2009

No comments:

Powered by Blogger.