Header Ads

SHAHIDI:BODI BoT HAIKUWAHI KUMLALAMIKIA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

MENEJA wa Masuala ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Justo Tongola (45), ambaye ni shahidi wa pili katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BoT, Amatus Liyumba, ameieleza mahakama kuwa hajawahi kuona wala kusikia bodi hiyo ikilalamikia utendaji kazi wa Liyumba.


Akitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, pia alidai hajawahi kushuhudia bodi hiyo ikikataa kuidhinisha maombi ya menejimeti ya benki hiyo wala aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali, akilalamikia mradi wa ujenzi wa minara pacha.

Shahidi huyo alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa maswali na mawakili wa utetezi Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Hillary Mkate, na Onesmo Kyauke mbele ya Jopo la Mahakimu Wakazi linaloongozwa na Edson Mkasimongwa anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa.

Sehemu ya mahojiano ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Nani alitoa kibali cha Kurugenzi ya Utumishi na Utawala iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba, iratibu mradi huo?

Shahidi: Sina hakika, ila miradi yote inayoangukia kwenye eneo la Capital Expenditure inaratibiwa na ofisi hiyo.

Wakili: Umesema ofisi iliyokuwa ikiongozwa na mshtakiwa (Liyumba) ilikuwa ikiratibu mradi huo, ilikuwa ikifanyakazi hiyo kwa niaba ya Benki Kuu?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Taarifa za uaandaaji wa mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi zilikuwa zinaratibiwa na ofisi ya mshtakiwa na nani?

Shahidi: Ofisi ya Liyumba na Meneja Mradi, Deogratius Kweka, ambaye aliajiriwa na Benki Kuu kwa mkataba.

Wakili: Nani mwingine alihusika katika uandaaji wa taarifa hiyo ya mabadiliko ya ujenzi ukiacha Kweka?

Shahidi: Hilo sina taarifa.

Wakili: Taarifa ikishaandaliwa inapelekwa kwenye bodi?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Ulisema mradi ulikuwa kwenye Capital Expenditure katika kipindi chote bodi ilikuwa hairidhiki na mabadiliko?

Shahidi: Kuna kipindi bodi baada ya kupokea maombi kadhaa ilikuwa hairidhiki na ilikuwa inarudisha baadhi ya maombi kwa menejimenti, ili zifanyiwe marekibisho kisha zinarejeshwa tena kwenye bodi na bodi inatoa idhini.

Wakili: Kuna kipindi chochote bodi iliwahi kumlalamikia Liyumba kama Liyumba?

Shahidi: Hilo sijawahi kusikia wala kuliona kwenye vikao ila kuna wakati menejimenti ilikuwa inaondolewa kwenye vikao.

Wakili: Ina maana Gavana na Naibu Gavana waliondolewa kwenye vikao vya Menejimenti?

Shahidi: Hapana, kwani hao ni kwa vyeo vyao ni sehemu ya bodi ila baadhi ya watendaji waliondolewa.

Wakili: Kuna sehemu uliona Gavana aliwahi kulalamika kuhusu mradi huo?

Shahidi: Mimi binafsi sijawahi kuona hilo.

Wakili: Ni kweli kwamba hakuna hata siku moja kikao cha menejimenti hakijawahi kujadili mradi huo hata mara moja?

Shahidi: Sikumbuki kama menejimenti iliwahi kuzungumzia mradi huo.

Wakili: Inawezekana kurugenzi ya utawala ipewe jukumu la kuratibu mradi halafu isiujadili?

Shahidi: Menejimenti ipo katika sehemu mbili. Mosi, Gavana ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia menejimenti na halazimiki kupeleka kila jambo kwenye menejimenti.

Wakili: Nitakuwa sijakosoe, mambo yanayofanywa na utawala lazima Gavana awe na taarifa?

Wakili: Utakubaliana na mimi jukumu la bodi ni kulinda maslahi ya BoT na serikali kwa ujumla yasihujumiwe?

Shahidi: Ni kweli na hilo ni jukumu la kisheria.

Awali, akihojiwa na wakili wa serikali, Juma Mzarau, shahidi huyo alidai alianza kujishughulikia masuala ya bodi kwa kumsaidia katibu wa Benki ambaye alikuwa na majukumu ya kuratibu maandalizi ya mikutano ya bodi na menejimenti na kuhakikisha wajumbe wanapata madokezi yote na maazimo yote yanawekwa kwenye maandishi.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 28 itakapotajwa na kupangwa siku ya kuendelea kusikiliza.

Chanzo:Gazerti la Tanzania Daima la Jumamosi, Novemba 24,2009

No comments:

Powered by Blogger.