Header Ads

SHAHIDI MWINGINE ABANWA KESI YA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa tano wa upande wa mashitaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, ameieleza mahakama kuwa hana kumbukumbu ya idadi ya maombi na kiasi cha fedha za nyongeza kilichokuwa kikiletwa na menejimenti kwenye bodi ya wakurugenzi ili ipate idhini.


Liyumba, anakabiliwa na tuhuma za matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Shahidi huyo ambaye ni mhadhiri kutoka Idara ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Dk. Natu Mwamba (48), alitoa amelezo hayo jana wakati akijibu maswali ya jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, baada ya kuhojiwa na mawakili wa utetezi na upande wa mashitaka.

“Kwanza, sikumbuki menejimenti ilileta maombi mara ngapi kwenye bodi yetu ya kutaka idhini ya matumizi ya nyongeza ya mradi…vile vile siwezi kukumbuka hayo maombi yaliletwa mara ngapi na menejimenti, pia sikumbuki ni kiasi gani cha fedha kilichokuwa kimeainishwa kwenye maombi hayo.

“Na kuniuliza hilo ni changamoto kubwa kwangu,” alidai Dk. Mwamba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya mahakimu wakazi na shahidi huyo:

Hakimu: Ulisema maombi ya nyongeza ya kutaka bodi yenu iyaidhinishe yalikuwa yakiegemea kwenye vikao vya dharura, je, dharura za menejimenti za kuitaka bodi ikutane zilitokea mara ngapi?

Shahidi: Siwezi kukumbuka.

Hakimu: Kwanini hukushtuka? Ni menejimenti iliyoomba vikao vya dharura vya bodi mara kwa mara?

Shahidi: Kwakuwa mwenyekiti wa bodi, yaani gavana, alikuwa ana kofia mbili, yaani pia ndiye aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, naweza kusema alikuwa anatu ‘over power’ wajumbe.

Hakimu: Unaweza kukumbuka bodi ililetewa na menejimenti mara ngapi maombi hayo ya matumizi ya nyongeza ya mradi wa ujenzi wa minara pacha?

Shahidi: Sikumbuki.

Hakimu: Ni kiasi gani kikubwa wewe kilikushtua katika maombi hayo ya matumizi yaliyowasilishwa na menejimenti katika bodi yenu?

Shahidi: Sikumbuki kiasi sahihi, ila ni kama mabilioni.

Hakimu: Hayo malipo ya matumuzi ya nyongeza kabla ya bodi kuyapa idhini, yalikuwa yanapitishwa na nani?

Shahidi: Gavana.

Hakimu: Bodi yenu iliiyaidhinisha malipo hayo?

Shahidi: Tuliyaidhinisha, kwani tulikuwa hatuna jinsi.

Hakimu: Kwa mujibu wa maelezo yako umeieleza mahakama bodi iliyaidhinisha malipo kwa sababu mlikuwa hamridhishwi na utaratibu huo, sasa kwanini hamkufikiria kujiuzulu ujumbe wa bodi?

Shahidi: Mmh! Hilo la kujiuzulu tulilifikiria ila tuliona tumekabidhiwa jukumu la kitaifa, tukashindwa kujiuzulu.

Hakimu: Mahakama imepokea ripoti inayoonyesha imeandikwa na wajumbe wa bodi, je, ieleze mahakama hii ripoti ni ripoti ya bodi?

Shahidi: Hapana siyo ripoti ya bodi, hiyo ripoti tuliandika sisi wajumbe wa bodi wa kuchaguliwa na ambao tulikuwa tunamaliza muda wetu na tuliweka saini zetu, wala haikumhusisha gavana, naibu gavana na Katibu wa Benki, ambao nao hao ni wajumbe wa bodi na wanaingia kwenye bodi hiyo kwa mujibu wa nyadhifa zao katika benki hiyo na tulivyomaliza kuiandika tuliikabidhi kwa bodi mpya.

Kwa hiyo naomba ieleweke hiyo taarifa siyo ya bodi, wala bodi ndogo, ni ya sisi wajumbe wa bodi ambao tulichaguliwa na tulikuwa tunamaliza muda wetu.

Yafuatayo ni mahojiano baina ya mawakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, Jaji mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke na Majura Magafu kwa shahidi huyo:

Wakili: Bajeti ya BoT zilikuwa zinaidhinishwa mara ngapi?

Shahidi: Mara moja.

Wakili: Baada ya bajeti hiyo, kwa mwaka kulikuwa na bajeti nyingine?

Shahidi: Mara nyingine zilikuwa zinakuja bajeti za nyongeza (supplementary bajeti).

Wakili: Umeieleza mahakama mara nyingi menejimenti ilikuwa inaleta maombi kwenye bodi, wakati inakuwa tayari imeishatekeleza nyongeza ya matumuzi?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Aliyekuwa anawasilisha taarifa ya maombi ya matumizi ya nyongeza kwenye bodi ni nani?

Shahidi: Meneja Mradi (Deogratius Kweka), na alikuwa anafanya hivyo baada ya Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Liyumba kuomba idhini kwa mwenyekiti wa bodi ili meneja mradi atoe taarifa hiyo.

Wakili: Taarifa hiyo ya maombi ya nyongeza ilikuwa imetayarishwa na nani?

Shahidi: Menejimenti ya BoT.

Shahidi: Bodi kupitisha ombi la nyongeza ya matumuzi wakati tayari matumizi yameishafanyika ni sahihi?

Shahidi: Kiutaratibu siyo sahihi.

Wakili: Bodi kupitisha ombi la nyongeza ya matumuzi baada ya matumuzi kuwa yameishafanyika kisheria, mnaweza?

Shahidi: Bodi inaweza, ila ni kinyume cha taratibu.

Wakili: Taratibu zipi hizo?

Shahidi: Kimya.

Awali akiongozwa na Wakili wa Serikali, Juma Mzarau, kutoa ushahidi wake, aliiambia mahakama kuwa wajumbe wa bodi walikuwa hawalidhishwi na menejimenti jinsi ilivyokuwa ikiwaletea maombi ya nyongeza ya bajeti wakati tayari matumizi yameishafanyika, lakini bodi haikuwa na jinsi, ikawa inaidhinisha maombi hayo.

Aidha, kiongozi wa jopo, Edson Mkasimongwa, aliahirisha kesi hiyo hadi leo, ambapo shahidi wa sita wa upande wa mashitaka anatarajiwa kuanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 25 mwaka 2009.

No comments:

Powered by Blogger.