Header Ads

SHAHIDI:UJENZI BOT HAUKUSABABISHA HASARA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa saba wa upande wa mashitaka katika kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, amedai kuwa hapakuwapo na hasara iliyopatikana katika ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo.


Shahidi huyo ambaye ni mkadiriaji wa gharama za majengo kitaaluma, Harold Herbert Webb (74), raia wa Uingereza, alitoa maelezo hayo jana wakati akijibu maswali ya wakili wa utetezi, Onesmo Kyauke, mbele ya kiongozi wa jopo la mahakimu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Webb alidai hapakuwepo hasara yoyote licha ya kuwapo kwa mabadiliko ya ujenzi na kiasi cha fedha kuongezeka kutoka dola milioni 73 hadi dola 357,568, kiasi chote hicho kilitumika kwenye mradi wa ujenzi huo.

“Hakuna hasara ya fedha iliyopatikana kwenye ujenzi huo, kwa sababu kiasi hicho kilichotengwa awali na kilichokuja baadaye baada ya BoT kuagiza yafanyike mabadiliko ya nyongeza ya maghorofa, kiasi hicho chote kiliingizwa kwenye mradi huo,” alidai Webb.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano baina ya mawakili wa utetezi Onesmo Kyauke, Majura Magafu, Hudson Ndusyepo na shahidi huyo:

Wakili: Nani alikuteua kufanya kazi ya ukadiriaji wa gharama za ujenzi wa mradi huo?

Shahidi: Kampuni ya ukandarasi ya Design & Services Ltd, kampuni ambayo ndiyo iliyopewa kazi ya kuchora majengo ya BoT.

Wakili: Ni mazoea katika shughuli za ujenzi kufanyika kwa mabadiliko?

Shahidi: Ni mazoea na inaruhusiwa.

Wakili: Katika mkataba wa awali kabla mabadiliko hayajafanyika ulikadiria mradi uwe wa gharama kiasi gani?

Shahidi: Dola za Marekani milioni 73.

Wakili: Kama kiasi hicho cha fedha kilitumika chote kwenye mradi, unafikiri kilisababisha hasara?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Nani alikuambia BoT imefanya mabadiliko ya mradi huo?

Shahidi: Nilipata maelekezo kutoka Kampuni ya D&S Ltd.

Wakili: Kwanini BoT ilifanya mabadiliko ya mradi?

Shahidi: Si kazi yangu kujua.

Wakili: Hicho kielelezo ulichokitoa ni ripoti ya mradi mzima?

Shahidi: Mmh! Siyo ripoti ila ni sehemu ya ripoti (watu wakaangua kicheko).

Wakili: Nani alikuambia uandae ripoti ya mradi huo?

Shahidi: Kampuni ya D&S.

Wakili: Lini ulimaliza kazi uliyopewa katika mradi huo?

Shahidi: Mwishoni mwa Februari 2008.

Wakili: Ulipata sababu za kufanyika kwa mabadiliko ya mradi?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Utakubaliana na mimi mabadiliko ya mradi yalitokana na matakwa ya mteja wenu ambaye ni BoT?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Wakati ukifanya kazi hiyo, uliwahi kuwasiliana moja kwa moja na Liyumba?

Shahidi: Hapana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 10 na 24 itakapokuja kwa kutajwa na kuendelea kusikilizwa mfululizo kuanzia Januari 26 – Februari 6 mwakani.

Liyumba anakabiliwa na makosa ya kuidhinisha mradi wa ujenzi wa majengo pacha BoT bila idhini ya bodi ya wakurugenzi, hivyo kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 27 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.