Header Ads

KESI YA RADA BADO YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa mara nyingine imeendelea kuahirisha kesi ya rushwa katika ununuzi wa rada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) inayomkabili Seileth Vithlani kutokana na mshitakiwa huyo kutokamatwa hadi sasa.


Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 4 mwakani, baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo kutokana na sababu hiyo.

Tangu kufunguliwa kwa kesi hiyo, Novemba mwaka 2007 mahakamani hapo, imekuwa ikiahirishwa kwa kuwa mshitakiwa hiyo ambaye alikuwa wakala wa ununuzi wa rada hiyo kutokamatwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, mshitakiwa huyo anadaiwa kusema uongo kuhusiana na Kampuni ya Envers Trading Corporation iliyokuwa ikimilikiwa na Pablo Espino na Adelina Estriby,tofauti na maelezo hayo, mtuhumiwa ndiye aliyekuwa mmiliki halali wa kampuni hiyo akiwa kama mkurugenzi na kwamba alipokea kiasi cha asilimia 31 ya uwakala wa mauzo ya rada ambayo ni sawa na dola 12,391,459.50 chini ya mkataba uliokuwa kati ya Red Diamond Trading Corp na Enves Trading Corp.

Katika shitaka la pili, inadaiwa Julai 28 mwaka jana, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mtuhumiwa alitoa maneno ya uongo kuwa alilipwa dola 390,000 za Marekani na Kampuni ya British Aero Space (BAE System) ambayo ni sawa na asilimia moja ya manunuzi ya rada ambayo ilinunuliwa na Tanzania wakati ukweli ni kwamba alipewa asilimia 31.

Mtuhumiwa huyo pia anakabiliwa na shitaka la kutoa taarifa za uongo kwa ofisa wa TAKUKURU, Kassim Ephrem, Desemba 27, mwaka jana, eneo la Kinondoni, Dar es Salaam kuwa alilipwa asilimia moja ya manunuzi ya rada huku akijua taarifa hiyo itaharibu upelelezi wa suala hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Novemba 20, 2009

No comments:

Powered by Blogger.