Header Ads

SHAHIDI WA SERIKALI AMTAKASA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa tatu katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala mstaafu wa Benki Kuu (BoT), Amatus Liyumba, ameiambia mahakama kuwa mshitakiwa huyo hakuwa na uamuzi wa mwisho katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha.


Shahidi huyo Julius Ruta Angelo (49) ambaye ni Mkurugenzi wa Fedha BoT, alitoa madai hayo mbele ya jopo la mahakimu wakazi; Edson Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akihojiwa na wakili wa utetezi, Majura Magafu.

Angelo aliieleza mahakama kuwa, Bodi ya Wakurugenzi ya BoT, ndiyo ilikuwa na uamuzi wa mwisho wa nini kifanyike na nini kisifanyike katika mradi wa ujenzi wa majengo ya Minara Pacha.

“Waheshimiwa, mshitakiwa (Liyumba) kwa wadhifa wake kipindi kile hakuwa na uamuzi wa mwisho katika mradi huo, bali bodi ya wakurugenzi ndiyo ilikuwa na uamuzi wa mwisho wa nini kifanyike na nini kisifanyike,” alidai Angelo.

Yafuatayo ni mahojiano baina ya mawakili wa utetezi Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke dhidi ya shahidi Anjelo:

Wakili: Nani alikuwa na majukumu ya kusimamia ujenzi wa mradi huu?

Shahidi: Ulikuwa unaratibiwa na Kurugenzi ya Utumishi na Utawala iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba.

Wakili: Ni nani alikuwa na maamuzi ya mwisho ya hili lifanyike na hili lisifanyike katika mradi huu?

Shahidi: Bodi ya Wakurugenzi ya BoT.

Wakili: Nitakuwa sijakosea nikisema aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala (Liyumba), asingeweza kusema ili lifanyike au ili lisifanyike bila kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi?

Shahidi: Nakubaliana na wewe.

Wakili: Maoni au mapendekezo yaliyotolewa na kurugenzi iliyokuwa ikiongozwa na mshitakiwa kuhusu mradi huo yalikuwa yanatoka wapi. Kwenye Menejimenti, Utawala?

Shahidi: Mmh! Naomba uniulize kuhusu mambo ya fedha, hayo mengine siyajui.

Wakili: Masuala ya fedha kwenye mradi huo yalikuwa yanaanzia wapi?

Shahidi: Yalikuwa yanaanzia kwa Meneja wa Mradi (Deogratius Kweka), na yakitoka kwake yanaenda kwenye ofisi ya Liyumba, kisha yanapelekwa kwa Gavana (Daud Balali) ambaye yeye ndiyo anaidhisha.

Wakili: Kwa kifupi, Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, hakuwa na kauli ya mwisho kwenye ujenzi wa mradi huo?

Shahidi: Ni kweli kabisa, hakuwa na kauli ya mwisho.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya jopo la Mahakimu Wakazi na shahidi huyo:

Hakimu: Liyumba kama Liyumba aliwahi kuidhinisha malipo?

Shahidi: Kimya.

Hakimu: Ulisema Bodi ya Wakurugenzi iliikemea menejimenti, tueleze bodi hiyo ilikemea mambo gani hayo?

Shahidi: Mengi iliyoyakemea ni malipo yaliyoidhinishwa na gavana na mengine iliyokemea siyakumbuki.

Hakimu: Bodi ilimkemea Liyumba?

Shahidi: Hapana, ilikemea malipo makubwa yaliyoidhinishwa na gavana na malipo madogo yaliyoidhinishwa na Liyumba kabla ya kupata kibali cha bodi.

Kesi hiyo ilipangwa ianze kusikilizwa mfululizo kuanzia jana hadi Novemba 26, lakini hata hivyo wakili wa serikali, Mzarau aliomba iahirishwe hadi Jumatatu hiyo kwa sababu aliyepanga kutoa ushahidi leo ni mgonjwa na anatibiwa nchini Kenya.

Alidai kuwa mashahidi wengine, wanakaa mbali na wanatarajia kuongeza idadi ya mashahidi na watawasilisha ombi hilo kwa maandishi.

Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na wakili Magafu, akidai kuwa hoja kwamba mashahidi wapo mbali si ya msingi kwani wanafahamu baadhi ya mashahidi wa upande wa mashitaka Bosco Kimela, yupo gereza la Keko, Profesa Semboja yupo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanapatikana kwa urahisi.

“Naomba tuwe makini na kesi hii, mteja wetu anaendelea kuteseka rumande na ni mgonjwa, anahitajika kwenda kutibiwa nje ya nchi, lakini inashindikana kwa sababu yupo rumande, kama upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kesi yao useme,” alidai Magafu.

Liyumba alifikishwa mahakamani hapo Januari 27 mwaka huu, akikabiliwa na makosa ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuidhinisha ujenzi wa mradi huo bila idhini ya Bodi ya BoT, hivyo kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Liyumba anaendelea kusota rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka atoe fedha taslimu au hati yenye mali yenye thamani ya sh bilioni 111.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 19,2009

No comments:

Powered by Blogger.