Header Ads

TUMSIHI MKAPA AENDELEE KUKAA KIMYA

Na Happiness Katabazi

MOJA ya mambo ambayo nina hakika yanaleta faraja kwa Serikali ya Awamu ya Nne ni ukimya wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, kuhusu tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazoelekezwa kwake, pamoja na malumbano ya hapa na pale ya kutaka kiongozi huyo aondolewe kinga ili aweze kufikishwa mahakamani kukabiliana na tuhuma hizo.


Pamoja na kufurahia jambo hilo, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa hivi sasa tumeanza kuwa na wasiwasi kwamba kiongozi huyo mstaafu ataendelea kukaa kimya?

Ni lazima wananchi watafakari kwa kina juu ya tuhuma za Mkapa, kwa nini zimeshamiri zaidi katika Awamu ya Nne?

Bila shaka jibu ni rahisi kuwa kulikuwa na uratibu maalumu wa kutangaza mabaya ya Mkapa ili watu watumie muda mwingi kufikiria na kuyazungumza mabaya yaliyofanywa na kiongozi huyo huku Serikali ya Awamu ya Nne ikiendelea kupumua na kufanya ufisadi kwa kadiri iwezavyo.

Ukitazama kwa kina utabaini kuwa mgawanyiko na malumbano ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo uliozaa haya tunayoyaona hapa nchini ambapo baadhi ya mambo ya maendeleo yanakwamisha kwa sababu ya chuki binafsi, kukomoa kunakofanywa na viongozi waliopo ndani ya chama tawala.

Hatuhitaji kuficha mabaya yaliyofanywa na kiongozi aliyetangulia lakini ni lazima tujiulize, je, ni kweli yatatusaidia kuziba nyufa zilizojitokeza au ndiyo yatabomoa kabisa nyumba tuliyoijenga kwa miaka mingi chini ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere?

Kwa nini hatujipi muda wa kutafakuri kwa nini viongozi na watendaji waliotenda maovu katika utawala wa Awamu ya Nne hawafikishwi mahakamani kama inavyoshinikizwa kwa Mkapa?

Si tunajua wapo watendaji na wanasiasa walishiriki katika kashfa za Richmond EPA, rada na nyinginezo lakini bado wanaendelea na nyadhifa zao pasi na aibu na uchungu kwa kutafuna rasilimali za taifa, tuna sababu gani la kumdhalilisha, kumuaibisha na kumkejeli Mkapa wakati tunajua fika kuwa hata Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, na yule wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, kuna makosa walifanya na mengine tunayajua waliyafanya kwa masilahi binafsi au familia zao, mbona hatujawaandama kama tunavyofanya kwa Mkapa?

Ni upumbavu kujadili makosa ya kiongozi mmoja mmoja alivyotumia vibaya madaraka yake akiwa Ikulu badala ya kujadili mfumo mzima uliomuwezesha kuingia madarakani pamoja na kufanya biashara zake akiwa Ikulu.

Kama tusipobadilika na kuuangalia mfumo huo kamwe hatutatua tatizo na kila kukicha tutakuwa tunawaandama viongozi wastaafu kwa sababu ya kutumia vibaya madaraka yao kwa misingi ile ile ya malumbano ya kutoa ahueni kwa serikali ya nne ambayo mpaka sasa imeshindwa kuleta maisha bora iliyowaahidi wananchi katika ilani yao ya uchaguzi ya mwaka 2005.

Mfumo uliopo wa wizi kutendeka kitaasisi ni hatari zaidi kuliko kuanza kushughulikia makosa ya mtu mmoja mmoja kama tunavyofanya sasa, tujiulize ni lini kulindana ndani serikali na chama tawala kutamalizika?

Kwa nini tusichukue hatua za kusafisha mfumo huu mbovu uliozaa EPA, rada, Richmond kuliko kumng’ang’ania Mkapa?

Si tumeshasikia fedha zilizoibwa Kampuni ya Kagoda Agricultural Limited kuchota kiasi cha sh bilioni 40 katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwapo chini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zilivyoisaidia CCM katika kampeni na hatimaye ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Leo hii tunawezaje kutoka mbele za watu na kudai tunapambana na ufisadi wakati wamiliki wa Kagoda hawajafikishwa mahakamani wakati wao ndio waliochota kiwango kikubwa cha fedha kulinganisha na wengine? Tutafakari tuchukue hatua.

Nani anayeweza kujitokeza hadharani na kuueleza umma kuwa ufisadi anaotuhumiwa kuufanya Mkapa aliufanya peke yake pasi na kushirikiana na wengine? Inawezekana vipi baraza la mawaziri lisijue kile kinachofanywa na kiongozi mkuu wa nchi? Bunge lilikuwa wapi mbona hawakupiga kura ya kutokuwa na imani na rais?

Waliamua kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kuwa walijua wazi kuwa mfumo wa serikali na chama tawala ni kulindana na wao kuna maeneo wanafaidika.

Tunapohoji nafasi ya Rais wa Awamu ya Tatu (Mkapa) kufanyabiashara akiwa madarakani, Serikali ya Awamu ya Nne inajiondoa vipi katika tuhuma kwamba wengi wa watendaji na viongozi ni wanatumia madaraka yao kufanyabiashara?

Kwa bahati mbaya wananchi wamekuwa vipofu wenye kupenda kushabikia kila kinachosemwa na wanasiasa ambao wanajua waseme au wafanye nini kwa wakati gani, wananchi wanapaswa wakae chini na kuchambua utekelezaji wa ahadi moja moja zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne badala ya kushabikia mambo ambayo mwisho wa siku hayana tija kwa taifa zaidi ya kuzidisha ugumu wa maisha.

Wananchi wana kitu gani cha kuipongeza Serikali ya Nne katika mapambano ya ufisadi wakati hata kesi zilizopo mahakamani nyingi zinaonekana zimepelekwa kwa ushabiki wa kisiasa au chuki binafsi?

Mfumo ndiyo chanzo kikuu cha kuzalisha kiongozi mzuri au mbaya, kama mfumo utakuwa mzuri kwa hakika hata viongozi watafanyakazi katika mfumo huo, utendaji wao utakuwa safi na uliojaa uadilifu lakini kama mfumo utakuwa mbaya hata aje kiongozi safi kama malaika hataweza kuubadilisha, kwani atamezwa na mfumo na mwisho wa siku naye atakuwa mchafu kama matope.

Kuna mifano mingi duniani ambapo serikali zilizoundwa na kuingia madarakani kwa mifumo mibovu imezivuruga nchi zao, Tanzania kabla ya kupata uhuru wake mwaka 1961 mfumo uliokuwapo kwa kiasi kikubwa ulikuwa ukitoa upendeleo kwa wakoloni lakini mara baada ya kupata uhuru Mwalimu Nyerere na viongozi wengine walijaribu kuboresha mfumo wa kiutawala kuanzia katika elimu, afya, miundombinu na huduma nyinginezo.

Lakini kwa bahati mbaya utawala wa Mwalimu Nyerere kuna baadhi ya mambo alishindwa kuyaweka katika mfumo uliokuwa unatakiwa, ulipoondoka madarakani na kuingia utawala wa mzee Mwinyi ‘Ruksa’ hatukusikia mabaya ya Nyerere kwa kiwango kikubwa kama tunavyosikia ya Mkapa hivi sasa, hivyo hivyo hata alipoingia Mkapa pia hatuyumbishwa na mabaya aliyoyafanya Mwinyi kwa sababu yaliyofanyika huko nyuma yalishapita, tulikuwa tukihitaji kujipanga vizuri pale tulipokosea ili maendeleo ya wananchi yapatikane.

Ni jambo la kusikitisha sana hivi sasa nchi ina wasomi wengi zaidi lakini maadili ya viongozi ndiyo yanazidi kumeguka siku hadi siku tofauti ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere na Mwinyi, kila mtu sasa ni muongeaji, mtendaji na kiongozi.

Tuulizane inawezekana vipi zaidi ya miaka 45 ya uhuru taifa halijitoshelezi kwa umeme kiasi cha kuingia katika mgawo wa kutisha, ni taifa gani linaweza kuendelea iwapo umeme haupo wa kutosha pamoja na kukatikatika hovyo hata katika hafla kubwa kama ile ya marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutiliana saini ya kuanzisha soko la pamoja pale kwenye ukumbi wa AICC Arusha wiki chache zilizopita.

Kwa nini nchi iwe maskini wakati kuna madini mengi ambayo kama yakitumika ipasavyo nchi haiwezi kutembeza bakuli la kuomba misaada ya wahisani katika bajeti yake, mbona utawala wa Rais Kikwete umeshindwa kusimamia madini kwa faida ya Watanzania?

Rais Kikwete aliunda tume ya kupitia mikataba ya madini ili itoe mapendekezo ya kuboresha kile kinachopatikana lakini mbona mpaka sasa kimya? Ripoti ile ilitolewa mapema sana lakini mbona imegeuka godoro la watu kuchapa usingizi?

Inawezekanaje mpaka leo hii nchi ikose dawa katika zahanati, hospitali, vituo vya afya wakati kuna mamilioni ya fedha yanatafunwa na viongozi kwa miradi ya uongo na ukweli, barabara mbovu, maji tabu, vyote hivi ni Mkapa kavisababisha?

Hapana huu ni mfumo mbovu wa chama tawala (CCM) bila kupigania kuuondosha kamwe maisha bora hayatapatikani, tutakuwa tukiyasoma, kuyasikia na kuyaangalia kwenye runinga, redio na magazeti kupitia kwa wenzetu.

Ni jukumu la Watanzania kuamka ili viongozi wasiendelee na utaratibu wa kufikiri wao ndio wenye akili zaidi kuliko wengine, tunahitaji mabadiliko lakini hayawezi kuja kama tutaendeleza woga, unafiki na chuki.

Tusipofanya hivyo tutakuwa tupo kwenye sala moja na uongozi wa Awamu ya Nne ya kumsihi Rais mstaafu Benjamin Mkapa aendeleze ukimya wake ili awape unafuu wa kutawala kwa kuwa tayari wameshaonyesha kushindwa kiuchumi, kimaadili, kiutawala na mengineyo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumapili, Novemba 29 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.