DK.HOSEAH UNAMTISHIA NYAU DPP?
Na Happiness Katabazi
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inashughulikia makosa ya rushwa lakini taasisi hiyo si Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai hapa nchini.
Alhamisi wiki hii, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, ameuambia umma kupitia vyombo vya habari kwamba kesi zaidi ya 60 zinazohusu rushwa kubwa zilizochunguzwa na taasisi yake ziko katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi.
Dk. Hoseah anasema utaratibu wa kesi za jinai kupitia kwa DPP, kabla ya kupelekwa mahakamani, unachelewesha kesi nyingi za rushwa na kwamba angetamani kesi zote za rushwa zilizochunguzwa na Takukuru ziruhusiwe kwenda mahakamani bila kupitia kwa DPP, kwa kuwa taasisi yake ina wanasheria waliobobea katika kuchunguza matukio ya rushwa.
“Utaratibu huu unatukwaza, tungependa kila mtu ampande farasi wake kama anajiamini kuwa farasi ni wa kwake, tuna wanasheria wetu waliobobea na wanaojiamini, hivyo tungependa zetu ziende mahakamani bila kupitia kwa DPP na kazi yetu ingeonekana, lakini hatuna mamlaka zaidi ya hapo...ila sipingi utaratibu wa kesi kupitia kwa DPP kwa kuwa uliwekwa kisheria na lazima tuufuate,” anasema Dk. Hoseah.
Dk. Hoseah kupitia matamshi hayo anatuonyesha na kutaka kuuaminisha umma kuwa wanachapa kazi kuliko taasisi nyingine; ikumbukwe cheo cha DPP ni cheo cha Kikatiba na ndiyo maana anateuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo hata rais wa nchi hawezi kumlazimisha DPP amshtaki mtu ambaye hajajiridhisha kisheria kama kuwepo kwa kesi hiyo ni kwa mujibu wa sheria.
DPP anaruhusiwa kushtaki, kutoshtaki na pia kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 pia kinampa mamlaka kuiondoa mahakamani kesi wakati wowote pindi atakapoona hana haja ya kuendelea na kesi hiyo na hapaswi kuhojiwa na mtu yeyote.
Ibara ya 59B(1) ya Katiba inatamka kuwa kutakuwa na ofisi ya DPP na Ibara ya 59(2) inaeleza kazi za DPP na Ibara ya 59(3) inataja majukumu ya kiongozi huyo likiwemo jukumu la ufunguaji mashtaka kiongozi huyo pia anaweza kuteua watu wa kuzifanya na Ibara ya 59(4) inasema: “DPP katika kutekeleza majukumu hayo hatakiwi kuingiliwa na mtu yeyote ili mradi majukumu anayoyafanya yawe ni ya maslahi ya umma, haki na azuie ukiukwaji wa misingi ya kisheria.
Misingi hiyo iliyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kuhusu DPP pia imeainishwa kwenye kifungu cha 6 na 8 cha Sheria ya Kusimamia Mashtaka nchini ya mwaka 2008.
Hivyo basi tukianza kumwendesha DPP kwa ‘rimoti’ tutakuwa tunavunja Katiba ya nchi. Na kwa madaraka hayo makubwa aliyopewa DPP katika Katiba na sheria hizo ambazo tumeziridhia wenyewe zituongoze na tuzitii, ndiyo maana kila mara Mwalimu wangu wa habari za uchunguzi, ambaye pia ni mwandishi mwandamizi nchini, Ndimara Tegambwage, huishia kusema DPP ni ‘Mungu’ wa Tanzania.
Kwanza DPP anatakiwa ajiridhishe na ushahidi ulioletwa mbele yake na vyombo vya upelelezi; upelelezi unaotosha kuweza kuthibitisha kesi, ndipo anaporidhia kesi ifunguliwe mahakamani kwani DPP atapotoa kibali cha kufunguliwa kesi ya jinai mahakamani kisha mwisho wa siku ushahidi hakuna, hali hiyo inapelekea serikali kushindwa kesi hiyo.
Pili, lazima DPP ajiridhishe kwamba kumshtaki mtu ni kwa maslahi ya nchi. Kwa hiyo hapo anaweza kupeleka kama ushahidi unatosha; sidhani kama DPP ni mjinga wa kukurupuka na kukimbilia mahakamani halafu kesho yake serikali inashindwa na kuingia kwenye aibu.
Ni vyema vyombo vya dola vinapofanya kazi zake vizingatie Katiba na sheria za nchini. Pindi viongozi wa vyombo hivyo wanapoona wanataka kutoa malalamiko au mapendekezo yao ya nini kifanyike ili taifa lisonge mbele ni vyema wayafikishe kupitia vikao rasmi.
Hivyo, matamshi hayo ya Dk. Hosea hayapaswi kupewa nafasi mbele ya jamii ya kistaarabu, jamii ikifikia hatua hiyo ya kuamini maneno ya kushutumiana yatolewayo na viongozi wa taasisi nyeti hukosa imani kwa chombo husika jambo ambalo huleta dharau na kupunguza imani dhidi ya chombo hicho.
Cha kujiuliza kwa nini Dk. Hoseah anatumia vyombo vya habari badala ya kupeleka malalamiko yake kwa rais ambaye ndiye amemteua? Kwa nini asiandike mapendekezo yake ili Bunge lipelekewe lifanye mabadiliko katika sheria?
Lakini pia kauli kama hizo ni sawa na kushtakiana au upande fulani kutaka upate sifa ya kuwa unafanya kazi nzuri kuliko mwingine mbele ya Rais Jakaya Kikwete na jamii.
Bado tungali tukikumbuka mapema mwaka huu ni Dk. Hoseah huyuhuyu ambaye alijitokeza hadharani na kuishutumu mahakama kuwa inaendesha kesi za ufisadi taratibu, hivyo kupunguza kasi ya taasisi hiyo kushughulikia watuhumiwa wa rushwa.
Hivi tumuulize Dk. Hoseah malalamiko kama haya alishawahi kuyawasilisha kwenye vikao husika na yakapuuzwa? Je, ni kwa nini kiongozi anayeongoza taasisi inayochunguza kesi za rushwa tu na si Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, ambaye ofisi yake ndiyo imetwishwa mzigo mzito wa kupeleleza kesi zote za jinai, iwe kesi za ujambazi, kughushi, wizi wa kuku, ubakaji, mauji, nk?
Ni kwa nini hata siku moja DCI- Manumba hatujamuona wala kumsikia akijitokeza hadharani na kubwabwaja kwamba ameishapeleleza idadi kadhaa ya kesi za jinai na amezifikisha ofisini kwa DPP na DPP ameshindwa kuzifikisha mahakamani?
Hivi ni kwa nini Takukuru ina papara ya kutaka kesi nyingine za rushwa zipelekwe mahakamani kwa wakati mmoja badala ya kusubiri matokeo ya kesi za rushwa zinazoendelea mahakamani ili wajipime?
Si siri baadhi ya kesi za rushwa zilizopelelezwa na Takukuru ambazo zinahusisha baadhi ya vigogo zinazoendelea kuunguruma mahakamani, tayari upande wa mashtaka katika kesi hizo umekuwa ukipata wakati mgumu kwa sababu upelelezi wa kesi hizo ulifanywa hovyohovyo na hao wachunguzi ambao tumeelezwa wamebobea katika nyanja hiyo na matokeo yake mashahidi wa upande wa mashtaka wanapofika mahakamani kutoa ushahidi katika kesi hizo, wanatoa ushahidi ambao unawatakasa washtakiwa.
Hali inayosababisha hata mambumbu wa sheria kung’amua utumbo huo na kuishia kusema bila kificho kwamba kesi hizo ni sinema na kwamba siku kesi hizo zinapokuja kwa ajili ya kusikilizwa utawasikia wananchi hao wakisema, “Leo tunaenda kurekodi sinema katika kesi ya mshtakiwa fulani mahakamani!”
Hali hiyo inatia hasira kwa walipa kodi wanaojionea madudu hayo pale mahakamani na kufuatilia kesi hizo kupitia vyombo vya habari kwani fedha za walipa kodi zinateketea bure kwa ajili ya upelelezi wa kesi hizo, muda wa mahakama unapotea na serikali yetu inashushiwa heshima mahakamani kwa sababu ya baadhi ya wachunguzi wa kesi hizo wamekuwa wakifanya kazi kwa kukurupuka.
Napenda kumuasa DPP (Feleshi), kwamba afanye kazi yake kwa mujibu wa sheria na Katiba ambazo ndizo zimempa madaraka, kamwe asikubali kufanya kazi kwa maslahi ya watu wachache ambao hivi karibuni tumewabaini kwamba kipindi chote cha kesi hizo za vigogo zilivyoanza kufunguliwa Novemba mwaka jana na hadi sasa pale katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Na kesi mpya zinazowahusu watu wenye nyadhifa serikalini na kwenye jamii, kwa mbwembwe nyingi zinazochagizwa na kamera za waandishi wa habari tunaokuwepo siku zote za juma mahakamani hapo, inakuwa ni mtaji kwao na kujitapa mitaani na kwa baadhi ya viongozi wenzao wa serikali kwamba ofisi zao zinafanya kazi kwa ari, kasi na nguvu mpya.
Hata kama ni kweli kesi hizo 60 zimepelekwa ofisini kwa DDP, ni vema akaepuka kukurupuka kuzipeleka mahakamani kuliko kukurupuka kuzipeleka huko ambapo mwisho wa siku ikishindwa inakuwa ni aibu kwa ofisi hiyo nyeti pamoja na kuingiza nchi katika hasara.
DDP ni lazima ujue kuwa kama usipokuwa makini katika kazi yako na kuendeshwa na watu kama kina Hoseah utaondoka kwenye wadhifa huo ukiwa na sifa moja mbaya ya wewe “Feleshi ni DDP pekee uliyefungua kesi nyingi kwa kipindi kifupi na serikali ikashindwa mahakamani”. Tumuulize Feleshi je, yuko tayari kutunukiwa sifa hiyo?
Dk. Hoseah huko ni kutojua utendaji wa umma. Inawezekana kwamba humtishii DPP ila hujui vyema maadili katika taasisi ya serikali katika mamlaka aliyonayo au unayajua vyema umeamua kufyatuka kwenye vyombo vya habari.
Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Hoseah, ni miongoni mwa viongozi wa juu wa serikali, anatakiwa kufahamu maadili ya utendaji wa serikali. Sasa namshauri kiongozi huyo arejee (Civil Service Regulation), ataona wazi kwamba serikali yetu haiendeshwi hivyo.
Kwani siku zote tujuavyo, serikali inatoa taarifa kwa vyombo vya habari kwani huo ni wajibu wake, lakini kamwe serikali haiendeshwi kupitia vyombo vya habari. Naomba kutoa hoja!
Mungu Ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika
0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Desemba 13,2009
1 comment:
kama TAKUKURU WANA UWEZO KWANINI WALISEMA RICHMOND NI KAMPUNI YENYE UWEZO NA SAFI?ILITAKIWA UHOJI HILI KWENYE MAKALA YAKO.
MTOTO UNAPENDEZA SANA UMEOLEWA?
Post a Comment