Header Ads

WAKILI ATAKA WATUHUMIWA EPA WAFUTIWE KESI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje, katika Benki Kuu, inayomkabili mfanyabiashara Bahati Mahenge na wenzake wanne, umeiomba mahakama iwaone washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu.


Ombi hilo lilitolewa jana na wakili wa utetezi Majura Magafu wakati akiwasilisha majumuisho ya ushahidi ili mahakama iwaone wateja wake wana kesi ya kujibu au laa kulingana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mbele ya jopo la Mahakimu Wakazi, Sekela Mosha, Lameck Mlacha na Sam Rumanyika.

Wakili Magafu alieleza kuwa anataka shtaka hilo lifutwe kwa sababu kifungu hicho hakipo kabisa kwenye sheria za nchi na badala yake kifungu sahihi kilichopo ni cha 305(a,b,c,d) cha sheria hiyo ya kanuni ya adhabu.

“Kwa hiyo mahakama haiwezi kuendeshwa kwa kifungu hicho cha 305(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kosa kama hilo la kujipatia ingizo kwa njia ya udanganyifu hapa nchini halijawahi kutumiwa na kifungu hicho na kwa sababu hiyo leo hii upande wa mashtaka hauwezi kutumia kifungu cha 334(1) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kufanyia marekebisho kwa sababu kifungu hiki kinataka makosa yaliyofanywa yaangukie kwenye vifungu vilivyopo kwenye sheria za nchi…sasa katika kesi hii upande wa mashtaka umewashtaki katika kifungu ambacho hakipo kwenye sheria za nchi,”alidai Magafu.

Akizungumzia shtaka la wizi wa sh bilioni 1.8, anadai katika mashahidi wote waliopelekwa na upande wa mashtaka , hakuna hata shahidi mmoja aliyetamka waziwazi kwamba washtakiwa waliiba kiwango hicho toka BoT.

“ASP-Mataba ameshindwa kudhibitisha fedha hizo ziliibwa; na suala jingine la kujiuliza fedha hizo zilizoibwa ni za nani? Sisi tunasema hakuna fedha zilizoibwa kwa sababu BoT yenyewe haijalalamika kuibiwa fedha na kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan ambayo ndiyo iliyotoa idhini kwa kampuni ya Changanyikeni Residential Complex ya hapa nchini kukusanya deni lake ndiyo yenye zile fedha.”

Pia alidai kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha hati ya kuhamisha deni ya Marubeni ya Japan ilighushiwa kwani hati hiyo haikupelekwa moja kwa moja kwa Mahenge bali ilipelekwa moja kwa moja BoT na kampuni hiyo ya Japan na kuongeza kuwa ushahidi unaonyesha kampuni hiyo ya nje siyo mara yake ya kwanza kufanya kazi na Changanyikeni Residential Complex.

“Kwa kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja wala mazingira, tunaomba mahakama ifikie uamuzi wa kuwaona washtakiwa Mahenge, Manase Makalle, Davis Kamungu na Edda Makalle, hawana kesi ya kujibu,” alidai Magafu.

Hakimu Mkazi Sekela Mosha aliairisha kesi hiyo hadi Desemba 21 mwaka huu, ambapo upande wa upande wa mashitaka nao utakuja kuwasilisha majumuisho yake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Desemba 12 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.