Header Ads

VIONGOZI WA DECI WAPANDISHWA KIZIMBANI

Na Happiness Katabazi

KWA mara nyingine tena viongozi watano wa kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) iliyokuwa ikijihusisha na shughuli za kuvuna na kupanda fedha, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na mashtaka ambayo bado hayajafahanika.


Vigogo hao ni Jackson Sifael Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Saigaran ole Loitginye, Samwel Sifael Mtares, Arbogast Francis Kipilimba na Samwel Mtalis ambao walifikishwa, Juni 12 mwaka huu, mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi ya kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 inayoendelea mahakamani hapo na wanatetewa na mawakili wa kujitegemea, Hudson Ndusyepo, na Simon Kitulu.

Waandishi wa habari za mahakama waliwashuhudia watuhumiwa hao wakifikishwa mahakamani hapo saa nane mchana wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari kanzu kutoka jeshi la polisi na kupelekwa moja kwa moja katika ofisi moja inayotumiwa na mawakili wa serikali mahakamani hapo.

Hata hivyo wakati waandishi wa habari wakiwasubiri wapandishwe kizimbani watuhumiwa hao, waliwashuhudia maaskari kanzu wakiondoka nao na kwenda kuwapandisha kwenye magari yenye namba za usajili T 515 BBH aina ya Mistubishi Pajero na T833 BDU aina Toyota Carina mali ya jeshi hilo bila watuhumiwa hao kupandishwa kizimbani.

Jana Tanzania Daima iliwasiliana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, ili athibitishe ni kweli jeshi lake linawashikilia vigogo hao tangu Desemba 8, mwaka huu; alipokea simu na kumtaka mwandishi wa habari kuwasiliana na msemaji wa jeshi hilo Abdallah Msika ili kupata taarifa zaidi.

Lakini kwa mujibu habari za kuaminika kutoka ndani ya jeshi hilo, watuhumiwa hao walikamatwa Desemba 8, mwaka huu, katika benki moja (jina linahifadhiwa) wakipokea malipo yao ya sh milioni 120 kutoka kwa mtu mmoja ambaye jina lake halijafahamika ambapo kabla ya serikali kuifunga DECI, mtu huyo aliwauzia nyumba watuhumiwa hao kwa thamani ya sh milioni 260 na watuhumiwa hao walimlipa kwa awamu sh milioni 120.

“Ndiyo, siku hiyo pande zote zilikutana ndani ya benki hiyo na kiasi hicho cha fedha walichokuwa wakirejeshewa kilikuwa kipitie kwenye akaunti ya watuhumiwa....nafikiri unakumbuka akaunti za DECI zote na fedha zote zinashikiliwa na serikali na akaunti hiyo waliyokuwa wakiitaka kupitishia kiasi hicho cha fedha tulikuwa hatuifahamu na raia wema wakaijulisha polisi ndipo tukaenda kuwamata na kiasi hicho cha fedha mkononi,” kilidai chanzo chetu.

Shughuli za kupanda na kuvuna mbegu DECI, zilisitishwa baada ya serikali kuifunga kampuni hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika hali ambayo ilisababisha uvunjifu wa amani katika ofisi za kampuni hiyo eneo la Mabibo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Desemba 15 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.