Header Ads

NKESHIMANA JOHN 'DIONE'



strong>KUTOKA HUKUMU YA KIFO HADI KUACHIWA HURU
*ASOTA JELA KWA MIAKA 12, ASIMULIA MATESO YA JELA

Na Hapinnes Katabazi

ADHABU ya kifo ni miongoni mwa adhabu zinazopingwa vikali na baadhi ya watu wanaotetea haki za binadamu kwa madai kuwa inakiuka haki ya kuishi ambayo kila mtu anastahili.

Nkeshimana John ‘Dione’, kamwe hawezi kusahau namna alivyonusurika na adhabu hiyo aliyopewa mwaka 2005 kwa kosa la mauaji ya Tatu Kuyamba, kosa lililomfanya akae gerezani kwa miaka 12 ambapo kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani mwaka 1997.

Tanzania Daima Jumapili, imefanya mahojiano kwa njia ya video na Nkeshimana ambaye amenusurika adhabu kifo ya kifo baada ya kushinda rufani yake aliyokuwa ameikata ambako alikuwa akitetewa na Shirika la Msaada wa Sheria (Nola) kupitia wakili wake Mugaya Mtaki.

Historia ya kilichompata Nkeshimana ni ndefu sana lakini kifupi anasema hakutenda kosa hilo na chanzo cha kesi hiyo ni ugomvi wa kiitikadi za siasa ulioanzia nchini kwao (Burundi) kwani kabla ya kuimbia nchi yao kwa sababu ya vurugu za kisiasa baina yake ya wakimbizi wenzake akiwamo marehemu ambaye alikuwa mfanyabiashara mwenzake wa vitenge.

Anasema na aliingia nchini kwa mara ya kwanza mwaka 1996 na kuendelea kuishi nchini akiendelea kujipatia kipato kwa kufanya biashara hiyo ya vitenge akishirikiana na wakimbizi wenzake.

anabainisha kuwa siku ya tukio, alikuwa yeye na wakimbizi wengine akiwemo marehemu walikuwa katika Kijiji cha Mwikigo wakifanyabiashara ya vitenge, lakini ghafla waliona watu wenye silaha na kuanza kuwakimbiza ambapo walianza kukimbia kwa lengo la kuokoa nafsi zao.

anabainisha kuwa jitihada zake za kujiokoa kutoka katika hatari hiyo iliyokuwa ikimkabili ilizaa matunda kwani alifanikiwa kujinasua pamoja na kunusuru kiasi cha sh 50,000 alichokuwa nacho kisiporwe na watu hao.

Anasema siku iliyofuata ilikuwa ni Jumapili ambapo alikwenda katika Kanisa la Sabato Manyovu na ibada ilipokuwa ikiendelea yeye na mwenzake walikamatwa na polisi walioingia katika kanisa hilo kwa madai kuwa anafanya kazi bila kibali na alipelekwa kituo cha polisi ambako alinyang’anywa fedha na polisi huku mkimbizi mwingine aliyekuwa amekamatwa naye akafanywa shahidi.

Alibainisha kuwa marehemu Tatu alionekana siku ya nne akiwa amekufa na kutumbukizwa kwenye shimo huku akiwa amefungwa kamba shingoni katika kijiji cha Mwikigo. Marehemu huyo alikuwa mfuasi wa chama cha Rais Burundi, Piere Nkurunzinza.

Anasema kisheria kesi hiyo ilikuwa haina dhamana hivyo mahakama ilimwamuru apelekwe gerezani Bangwe na baada ya miezi sita alifunguliwa kesi ya jinai Na. 478/1997 ya wizi wa kuiba kwa kutumia nguvu.

Anaongeza kuwa kesi hiyo mwisho wa siku ilifutwa kwa sababu mashahidi walikuwa hawatokei mahakamani hivyo akawa anakabiliwa na kesi moja ya mauaji ambayo ilikuwa ya kupikwa.

Anaeleza kuwa Desemba 1998 alihamishiwa Gereza la Uyui Tabora ambako alikaa hadi mwaka 2000, mwaka 2005 ndipo alihukimiwa adhabu ya kifo ambayo ilimfanya asote gerezani kwa miaka 12 kabla ya hivi karibuni kufutiwa adhabu hiyo. Adhabu ya kifo alianza kuitumikia Gereza la Uyui baadaye akaamishiwa kutumia kifungo hicho kwenye gereza la Bangwe-Kigoma.

Akizungumzia maisha ya gerezani baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo, anasema alikataa tamaa na kuona adhabu hiyo ndiyo mwisho wa maisha yake ila alikuwa anajua ameonewa lakini kilichokuwa kikimsikitisha zaidi ni nguo za bluu alizokuwa akizivaa.

Anasema wafungwa wanaosubiri kunyongwa angalau wanakula vizuri na wana uangalizi maalumu chini ya askari wa Jeshi la Magereza pamoja na kulala wafungwa watatu katika chumba kimoja kidogo.

“wakati mwingine chakula kilikuwa kinanishinda kula, niliugua mara tatu gerezani nusura nife ila nashukuru Mkuu wa gereza alinipenda sana, kwa kweli maisha ya adhabu ya kifo yanatisha sana ..tulivyokuwa tukiwasikia wabunge na wanaharakati kwenye redio na televisheni wakisema walioua nao wauawe basi siku hiyo sisi hatulali wala kula.

“Tulikuwa tunalala saa tisa alasiri kuamka hadi kesho yake saa moja asubuhi na tunapokuwepo chumbani tunakuwa tunazungumza kimya kimya ....gerezani kuna watu walikuwa wakijiita marehemu ...tukawa tunajiuliza lini tutanyongwa na kuhoji ni kwanini rais hanyongi,” anasema.

Anabainisha kuwa gerezani kuna sehemu ya kunyongea ambayo walikuwa wakiiona hivyo kuwafanya wachanganyikiwe na kujiona ni wafu wasio na mwelekeo.

“Chumba hicho kilikuwa kimefungwa ndani kilikuwa na minyoro, kwa kusmea ukweli lilikuwa jambo la kutisha na la kusikitisha sana kila nikikumbuka natawaliwa na huzuni,” anasema Nkeshimana.

Anasema adhabu hiyo imemfunza mambo mengi ambapo kwa muda mrefu alikuwa muhalifu halafu mfungwa na sasa yu huru, anabainisha kuwa sheria za Tanzania ni nzuri hasa zikimpata mtoa haki wenye kujali na kufuata misingi yake.

Anabainisha kuwa adhabu ya kifo haifai kabisa kwani wafungwa wa adhabu hiyo akili zao huwa si za binadamu wa kawaida kwa kuwa mtu hujua amepangiwa kufa na binadamu mwenzake jambo ambalo ni baya asana.

Aidha, anashauri sheria ibadilishwe ili kesi kubwa za mauaji angalau zipitie kwa mahakama zisizopungua tatu kuliko ilivyo hivi sasa ambapo kesi za mauaji zinasikilizwa katika Mahakama Kuu na mahakama ya Rufaa.

Anasema mfumo huo unahitaji umakini wa jaji na asipokuwa makini hutoa adhabu ya kifo kwa mshitakiwa asiyefanya kosa jambo ambalo ni sawa na kuminya haki ya msingi ya mtu mwingine.

Anasema kama ilivyo kwenye makosa mengine tofauti mauaji ambapo makosa ya wizi, kughushi na mengineyo yanaanzia kwenye mahakama za chini na kama mtu hajaridhika anakata rufaa mahakama za wilaya mkoa, Mahakama Kuu na Rufaa.

Nkeshimana ambaye anaendelea kuishi kwenye kambi ya Mtabira Kasuru, mkoani Kigoma anasema hivi sasa anaanza masiaha mapya lakini yenye furaha hasa baada ya kukwepa kitanzi kilichokuwa kikimkabili.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani lililokuwa likiongozwa na Jaji Natharia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk ndilo lilosikiliza rufaa ya mkimbizi huyo ambapo Oktoba 26 mwaka huu, ilitengua adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Shirika hilo la Nola linakodisha mawakili wa kuwatetea wakimbizi wanaokabiliwa na kesi mbalimbali hapa nchini chini ya mradi wa kutoa msaada wa kisheria kwa wakimbizi na jamii inayoizunguka (CPSP) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Mrufani huyo alikata rufaa kupinga hukumu hiyo iliyotolewa mwaka 2005 na Hakimu Mkuu Mkazi Kigoma, Awasi ambaye alipewa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauji (Extended Jurisdiction) na Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na alimhukumu kunyongwa hadi kufa mrufani ambaye alikuwa akidaiwa kumuua mkimbizi mwenzake aitwaye Tatu Kuyamba.

Nakala ya rufaa hiyo ambayo Tanzania Daima ina nakala yake, Jaji Mbarouk anasema upande wa mashitaka ulidai marehemu aliuawa na mwili wake ulikutwa na kamba shingoni, lakini ulishindwa kuleta kamba hiyo mahakamani ili iwe kielelezo, akasema upande wa mashitaka kushindwa kupeleka mahakamani kamba hiyo kunaacha shaka kubwa kama ni kweli marehemu aliuwawa kwamba na kuongeza kuwa kanuni za uendeshaji wa kesi za jinai upande wa mashitaka unatakiwa udhibitishe kesi yake bila kuacha shaka lolote na katika hilo umeshindwa kuthibitisha mashaka.

Jaji Mbarouk anasema kwa mujibu wa nakala ya hukumu ile Hakimu Awasi alitoa hukumu ya kifo kwa mrufani na kisha akapeleka nakala ya hukumu Mahakama Kuu, anasema kitendo hicho kimeonyesha wazi asivyojua vyema marekebisho ya Sheria Na.

32 ya mwaka 1994.Kwa mujibu wa kifungu cha 173(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002,ambacho kinasema Hakimu Mkazi anayepewa mamlaka ya Mahakama Kuu ya kusikiliza kesi ya mauji kabla ya kutoa hukumu hiyo hakimu huyo anatakiwa kupeleka rekodi ya uamuzi wake Mahakama Kuu ili uwakikiwe.

“Sasa kwa kitendo kile cha Hakimu Awasi kumhukumu mrufani bila kwanza kupeleka rekodi ya hukumu yake Mahakama Kuu ambayo ndiyo ilimteua na kumpa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauji, jopo hili linasema hukumu ile ni batili kisheria.

“Na kwamba ushahidi wa mazingira ambao Hakimu Awasi alisema ulitosha kumtia hatiani mrufani, jopo hili tunasema hiyo siyo hoja ya msingi ya kumuona mrufani ana hatia hiyo mahakama ya rufaa inatengea uamuzi wa Mahakama Kuu uliomhukumu mrufani kunyongwa hadi kufa na pia tunaamuru mrufani aondolewe gerezani,” anasema Jaji Mbarouk.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Desemba 6 mwaka 2009.

No comments:

Powered by Blogger.