Header Ads

VIGOGO DECI KIZIMBANI TENA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE waliokuwa wakurugenzi wa Kampuni ya Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI) iliyokuwa ikijihusisha na shughuli za kuvuna na kupanda fedha, jana walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, na kusomewa mashitaka ya wizi wa sh milioni 118 mali ya DECI (Tz) Ltd.

Washitakiwa hao ni Dominick Kagendi, Jackson Sifael Mtaresi, Timetheo ole Lating’ye na Samuel Sifael Mtaresi wanaotetewa na wakili wa kujitegemea, Hudson Ndusyepo.

Wakili wa Serikali Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana alidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa mawili.

Kishenyi alidai shitaka la kwanza ni kwamba washitakiwa wote hao kati ya Desemba 1 na 8 mwaka huu katika sehemu isiyofahamika walikula njama kwa nia ya kulaghahi umma ili kuiba sh 118,440,000.

Alidai shitaka la pili ni la wizi kwamba Desemba 8 mwaka huu, katika Benki ya Standard Chartered tawi Kariakoo jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote waliiba kiasi hicho cha fedha mali ya DECI (Tz) Ltd. Na washitakiwa wote walikana mashitaka hayo.

Hata hivyo, wakili huyo wa serikali Kishenyi alisema upande wa mashitaka unapinga washitakiwa hao wasipewe dhamana kwa sababu wametenda kosa hilo wakati wapo nje kwa dhamana katika kesi ja jinai Na.109 ya mwaka huu, inayoendelea mahakamani hapo.

Juni 12, mwaka huu, washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi Na.109 ya mwaka huu, ya kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na kifungu 111A(1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kampuni ya DECI iliyowanufaisha watu wengi hasa wale waliojiunga mwanzoni, iliibua malumbano kati ya serikali, viongozi wa kampuni hiyo na wanachama wao, waliopinga hatua ya serikali kusitisha shughuli zake kwa madai kuwa haiko kihalali.

Kusimamishwa kwa shughuli za kampuni hiyo, kulitokana na uamuzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutoa taarifa ya kuwatahadharisha Watanzania waliojiunga na upatu huo kuwa, taasisi hiyo haiko kisheria na wanaweza kupoteza fedha zao walizopanda.

Shughuli za kupanda na kuvuna mbegu DECI zilisitishwa baada ya serikali kusimamisha akaunti za kampuni hiyo hadi hapo uchunguzi utakapokamilika, hali ambayo baadaye ilisababisha uvunjifu wa amani katika ofisi za kampuni hiyo, baada ya wanachama wake kuamua kuchukua sheria mkononi kwa kuvunja vioo vya magari ya viongozi, wakitaka warejeshwe fedha zao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Desemba 16 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.