Header Ads

ALEX STEWART ILIANZA KAZI BILA USAJILI-SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

MSAJILI Msaidizi wa Makampuni toka Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), Frank Kajusi (37) ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba kampuni ya Alex Stewart (Assayers)Govement Bussiness Corporation ilianza kufanya biashara bila kupata hati ya usajili toka BRELA.


Kajusi ni shahidi wa 10 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake wawili.

Kajusi alitoa maelezo hayo wakati akiongozwa kutoa ushahidi na wakili mwandamizi wa serikali, Fredrick Manyanda. alidai kisheria kampuni yoyote ya nje inapokuja nchini kabla ya kuanza kufanya biashara inatakiwa iwe imepata hati ya kufanya biashara kutoka BRELA, lakini kampuni hiyo haikuwa imetimiza sharti hilo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Hurbet Nyange, alipombana kwa maswali shahidi huyo kwamba maelezo hayo ndiyo ushahidi wake ambao anaiomba mahakama iupokee shahidi huo alidai kuwa si wake, hali iliyofanya jopo la Mahakimu Wakazi linaloongozwa na John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela kuingilia kati na kumkumbusha shahidi huyo kuwa awali aliiambia mahakama kampuni hiyo ilianza biashara bila hati ya BRELA na wakati huo anatoa maelezo tofauti.

Hali hiyo ilimfanya shahidi huyo arudie kueleza kuwa kampuni hiyo ilianza biashara bila kupata hati ya BRELA na kuongeza kuwa haoni tatizo kwa BoT kuingia mkataba na kampuni hiyo ya Alex Stewart bila ya kampuni hiyo kuanza kufanyabiashara.

Hakimu Mkazi Saul Kinemela aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa 11 anatarajiwa kuja kuanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 13 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.