Header Ads

MWANASHERIA MAARUFU AUAWA KINYAMA DAR


*Ni Profesa Mwaikusa wa Chuo Kikuu Dar
*Jaji Mkuu, DPP wapigwa butwaa

Na Happiness Katabazi

MHADHIRI Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Juani Timoth Mwaikusa (58) ameuawa kinyama kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, nyumbani kwake usiku wa kuamkia jana.


Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP), Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu waliohusika wanasakwa kwa udi na uvumba.

Kamanda Kenyela alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4 usiku, Barabara ya Makonde eneo la Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Alisema Mwaikusa alifikwa na mauti baada ya kufika nyumbani kwake akiwa na gari lake aina ya Nadia, lenye namba za usajili T 876 BEX wakati akitoka kwenye shughuli zake. Alivamiwa na watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi.

“Wakati Mwaikusa akijiandaa kushuka katika gari lake, majambazi hao walimgongea kioo na kumwamru kushuka, lakini Profesa Mwaikusa alisita, ndipo majambazi hayo yalipomvuta kwa nguvu kisha kummiminia risasi mwilini.

“Wakati wamemaliza kumpiga risasi, alitokea mpwae Profesa Mwaikusa, Gwamaka Daudi (25), ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi VETA kwa lengo la kumnusuru, lakini ghafla majambazi yakamgeukia na kumpiga risasi mgongoni na kufariki dunia papo hapo,” alisema Kamanda Kenyela.

Baada ya kuwaua ndugu wawili, majambazi hayo yalisogea mbele kidogo na kuona kikundi cha watu ambacho walikitilia shaka kwamba wanataka kupambana nao, ndipo walipompiga risasi mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la John Mtui (45), ambaye ni mfanyabiashara anayeishi jirani na marehemu Profesa Mwaikusa, aliyekuwa na bastola aina ya Revolver namba 87668.

Alisema Mtui alipigwa risasi kifuani na kufariki dunia hatua chache kutoka alipouawa Profesa Mwaikusa.

Alisema majambazi hayo baada ya kumuua marehemu Profesa Mwaikusa yanadaiwa kupekua mifuko ya nguo zake alizokuwa amevaa na ndani ya gari lake, ingawa mpaka sasa haikufahamika waliondoka na nini.

Kamanda Kenyela alisema majambazi hao wa
nadaiwa kufika eneo la tukio kwa kutumia usafiri wa pikipiki na baada ya tukio yalitokomea kusikojulikana. Miili yote imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Katika hatua nyingine, kada ya wanasheria nchini wameeleza kuguswa na mauaji hayo na kusema pengo hilo kamwe halizibiki.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhan, alisema taifa limepoteza mtu hodari kwenye taaluma ya sheria.

Alisema marehemu Mwaikusa alikuwa mwenyekiti wa jopo la majaji saba waliosikiliza rufaa ya kesi ya mgombea binafsi.

Aprili 11, mwaka huu, Profesa Mwaikusa alikuwa miongoni mwa magwiji wa sheria ambao waliitwa kutoa maoni yao kama marafiki wa mahakama kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi nchini mwaka jana.

Naye Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, alisema yeye na ofisi yake wameshtushwa na taarifa hiyo, kwani Mwaikusa ambaye alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Sheria Tanzania katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, enzi ya uhai wake alifanya kazi kwa uadilifu mkubwa.

“Katika kesi hizo mbili Profesa alikuwa akiudhuria kama rafiki wa mahakama,siyo wakili kwahiyo umuhimu wake haukuwa kwenye taaluma yake ya uwakili bali hata rafiki wa mahakama na aina ya mauti iliyomkuta inatufundisha kwamba uhalifu hauchagui kwahiyo tujifunze kukemea uhalifu na kifo hicho kiwe ni changamoto kwa jamii kwa kuwafichua waahalifu na kuviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili viweze kupambana na kuzuia uhalifu”alisema Feleshi kwa sauti ya unyonge ambaye alisema marehemu alikuiwa mwalimu wake wa sheria.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu, alisema mhimili wa Mahakama nchini ulimfahamu marehemu kuwa ni mchapa kazi shupavu, aliyetoa hoja zilizosaidia kupata ufumbuzi wa kesi mbalimbali.

Alisema Katiba ya nchi ipo kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na kwa msingi huo haki za binadamu ni mama wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na kuongeza kuwa kama kuna kifungu kinavunja haki za binadamu basi kifungu hicho ni wazi kinakiuka haki za binadamu kwa sababu haki za binadamu zilianza, Katiba ikafuata.

“Kwa uamuzi ule wa Mahakama Kuu wa kubatilisha vifungu vya ibara 21(1) (c), 39(1) (c) (b) na 69(1) (b) za Katiba ya nchi, kama kuna ibara zinapingana, ibara inayopaswa kutumika ni ile inayolinda haki za binadamu na kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kutamka ibara hizo ni batili kwani Katiba inalinda haki za binadamu na haki hizo za binadamu zilianza Katiba ikafuata hivyo haki hizo ni sheria mama.”

Naye Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Profesa Paramaganda Kabudi alisema kifo hicho ni pigo kwani marehemu alikuwa ni mtafiti mahiri na msomi makini kwa wanafunzi na walimu wake na alikuwa mwenye vipaji vingi kwani mbali na taaluma yake ya sheria pia marehemu alikuwa mshahiri mzuri wa mashahiri aliyoyatunga kwa lugha ya kiingereza ambayo ameyaweka kwenye kitabu cha ‘Summons Poems of Tanzania’ na kwamba mara mwisho alishirikiana naye kwenye rufaa ya mgombea binafsi ambao wote walikuwa ni marafiki wa mahakama ambao waliotoa maoni yao ya kitaaluma.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alimwelezea marehemu kuwa alikuwa mtaalamu mzuri na mwenye msimamo wa kutetea wananchi na kwamba taarifa ya kifo hicho imewaumiza.

Naye wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa, alimwelezea marehemu kuwa alikuwa miongoni mwa mawakili walioendeleza sheria kwa kiwango cha juu na kutolea mfano kuwa alikuwa wakili katika kesi ya Uchaguzi Mkuu iliyofunguliwa na Jaji Mkuu mstaafu Joseph Warioba, dhidi ya aliyekuwa mgombea mwenzake wa Chama cha NCCR –Mageuzi, Steven Wassira, mwaka 1996.

“Na hoja ya rushwa kwenye uchaguzi ambayo ilitolewa kwenye kesi hiyo na Profesa Mwaikusa kwamba mgombea akitoa vitu vidogo vidogo kwa wapiga kula ni rsuhwa na hoja yake hiyo ilisababisha bunge kutunga sheria Takrima ya mwaka 1998...kwakweli nimeupokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo marehemu ambaye alikuwa mwalimu wangu na ninaomba polisi wafanye uchunguzi wa kina ili hatimaye washtakiwa wafikishwe mahakamani”alisema Wakili Mgongolwa.

Huyo ni wakili wa pili nchini kuuawa kikatili na watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi. Wa kwanza alikuwa Dk. Eliuther Kapinga, mwaka 2002.
Kapinga aliuawa kikatili kwa kunyongwa shingo na kupigwa nondo kichwani nyumbani kwake, Mbezi Beach.

Majambazi waliomuua Kapinga walitiwa hatiani kwa kosa la mauaji na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Juston Mlay, ambaye aliwahukumu adhabu ya kunyongwa kwa kamba hadi kufa.

Katika hatua nyingine, mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, aliyetambuliwa kwa jina la Saddam (20), aliuawa jana kwa kupigwa risasi na mmiliki wa baa ya Angel Pub iliyopo Ilala, Sharif Shamba.

Chanzo cha Saddam kupigwa risasi inadaiwa ni vurugu kubwa iliyozuka katika baa hiyo baada ya kundi lililoongozwa na marehemu huyo kuvamia baa hiyo majira ya saa 9 alasiri.

Kundi la vijana wapatao 20 walifika eneo hilo ghafla na kuanza kurusha mawe pasipo sababu zilizowekwa bayana.

Baada ya kuona hali hiyo inazidi, mmiliki wa baa hiyo alitoka nje kuzuia fujo hizo lakini hakufanikiwa.

Aliamua kuchukua bastola yake na kumpiga risasi marehemu kifuani na ambayo ilitokea mgongoni.

Kamanda wa Polisi Ilala, Faustin Shilogile, aliwataja vijana wengine wawili waliokamatwa kutokana na vurugu hizo waliotambuliwa kwa majina ya Thabit Mussa (19), ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Bariki, iliyopo Mbagala na Donald Tadei (22), wote wakazi wa Ilala, Sharif Shamba ambao walijeruhiwa kwa risasi na wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
Kaimu Kamanda Kenyela amesema chanzo cha vurugu hizo ni mteja kuibiwa mali zake chooni.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Julai 15 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.