Header Ads

RUFAA YA LIYUMBA KUSIKILIZWA AGOSTI 27

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Agosti 27 mwaka huu, inatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba(62) ambaye Mei 24 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimuhukumu kifungo cha miaka miwili jela baada ya kumkuta na hatiani kwa kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.


Kwa mujibu wa hati ya wito wa kuitwa mahakamani siku hiyo iliyotolewa na uongozi wa Mahakama Kuu kwa mrufani mwenyewe(Liyumba) , wakili wake Majura Magafu na upande wa Jamhuri na inaonyesha Jaji Emilian Mushi ndiye aliyepangwa kusikiliza rufaa hiyo Na 56 ya mwaka huu.

Tanzania Daima ambayo ilifanikiwa kuiona na kuisoma nakala hiyo ya wito(summons), ambayo imezitaka pande zote katika rufaa hiyo kufika mahakamani hapo saa tatu asubuhi siku hiyo ambapo rufaa hiyo itakuja kwaajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza tangu ilipofikishwa na mrufani Mei 28 mwaka huu.

Hata hivyo taarifa za kuaminika toka Mahakama Kuu zinasema tayari mrufani(Liyumba)ameishapelekewa nakala hiyo ya wito tangu juzi katika Gereza la Ukonga anakoishi kwasasa toka alihukumiwa na kwamba jana mchana nakala nyingine ya wito inatarajiwa kupelekwa ofisini kwa wakili wa mrufani Majura Magafu.

Kwa mujibu rufaa hiyo, mrufani ametaja sababu 12 za kukata rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakimu wa Kazi wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa ambao ndiyo waliomtia hatiani mrufani Wakati aliyekuwa kiongozi wa jopo hilo la mahakimu hao wakazi Edson Mkasimongwa alitoa hukumu yake peke yake na akamwachiria huru mrufani na hukumu ya hakimu huyo imeifadhiwa na kwenye kumbukumbu za mahakama hiyo.

Liyumba anadai mahakama ya Kisutu ilishindwa kuchambua ushahidi uliotolewa mahakamani kikamilifu na matokeo yake jopo hilo la mahakimu wakazi wa tatu likajikuta linatoka na hukumu mbili tofauti,mahakimu hao wawili walifanya makosa kwa kushindwa kwake kukubali mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Minara Pacha yalifanywa baada ya Meneja Mradi huo Deogratius Kweka kuketi kwenye kikao na timu ya wataalamu wa ujenzi na kujadili shughuli za mradi huo,kwani kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekedi za mahakama hauonyeshi Liyumba alikuwa akiudhuria kwenye kikao hicho cha wataalamu wa masuala ya ujenzi wa mradi.

Mrufani katika sababu ya tatu anadai mahakimu hao wakazi wawili(Mlacha na Mwingwa) walifanya makosa kwa kushindwa kwao kukubali kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mradi ule zilikuwa chini ya Meneja Mradi Deogratius Kweka ambaye alikuwa akiwajibika moja kwa moja kwa Gavana na si kwa mrufani(Liyumba), walifanya makosa kwa uamuzi wao wa kuutupilia mbali ushahidi uliotolewa na Liyumba na shahidi wake ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa Benki Kuu, Bosco Kimela kwa maelezo kuwa mashahidi wote walikuwa wakiishi pamoja katika gereza la Keko.

“Sababu ya tano, mahakimu hao walifanya makosa kwa kusema kwamba Liyumba na Kimela ushahidi wao ulikuwa kama hadithi ya kutunga....sisi tunapinga hoja hiyo ya mahakama kwa kusema ushahidi huo haukuwa hadithi ya kutunga,mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema malipo ya mradi huo yalikuwa yakiidhinishwa na Liyumba...sisi tunapinga hoja hiyo ya mahakama kwani ni wazi kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama hauonyeshi Liyumba alikuwa akiidhinisha malipo ya mradi huo, sasa ushahidi huo hao mahakimu wameupata wapi?alidai mrufani.

Aidha aliitaja sababu ya saba ni kwamba mahakama ya kisutu ilifanya makosa kusema Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ilipoteza mwelekeo na kwamba Liyumba na aliyekuwa Gavana marehemu Daud Balali walikuwa wakiiburuza bodi hiyo.Magafu anadai hoja hiyo ya mahakama ni ya kufikirika na hata ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama hauonyeshi mahali popote kwamba bodi hiyo ilikuwa ikiburuzwa na mrufani.

Alidai sababu ya nane ni mahakama hiyo ilifanya makosa kusema idhini za mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa Minara Pacha zilitolewa baada ya utekelezaji kufanyika hazikubariki kisheria, wakili huyo anadai kuwa hoja hiyo ya mahakama si ya kweli kwasababu idhini zote zilizokuwa zikitolewa zinaruhusiwa na Kanuni za Fedha za Benki Kuu(BoT Financial Regulation).

“Sababu ya tisa ni kwamba mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema mrufani hakuwa na mamlaka ya kusaini zile barua ambazo zilikuwa zimeandikwa na mrufani kwaniaba ya BoT ambazo zilikuwa zikienda kwa mkandarasi ambazo ni kielelezo cha 5-12 na kwamba alifanya hivyo kinyume cha sheria....sisi mawakili wa mrufani tunasema hilo si kweli.

“Sababu ya kumi,mahakama hiyo ilifanya makosa iliposema kwamba mabadiliko ya mradi ambayo yalisababisha ongezeko la gharama katika mradi ule yalikwenda kinyume na matakwa ya bodi na kwamba bodi iliathirika”alidai mrufani.

Sababu ya 11, mrufani anadai mahakama ilikosea kusema kwamba upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliweza kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka yoyote dhidi ya mrufani, wakili wa Liyumba anadai hilo si kweli kwani ushahidi ule wa upande wa mashtaka umeacha mashaka makubwa.Aidha sababu ya 12, mrufani anadai mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifanya makosa kwa kushindwa kwake kufuata taratibu zilizoainishwa kisheria katika kutoa adhabu.

Januari 27, mwaka huu, Liyumba na Meneja Mradi, Deogratius Kweka walifikishwa mahakamani hapo, wakikabiliwa na makosa mawili ya matumuzi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.Lakini, Mei 27 mwaka jana mahakama hiyo iliifuta hati ya mashitaka baada ya kubaini ina dosari za kisheria na ikawaachia washtakiwa ingawa walikamatwa muda mfupi tu na kesho yake Mei 28 mwaka jana ,ni Liyumba peke yake ndiye alifikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 16 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.