Header Ads

MAWAKILI ZINGATIENI USHAURI WA JAJI JUNDU


Na Happiness Katabazi

JUNI 24 mwaka huu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu, alisema hadi kufikia siku hiyo Tanzania ina jumla ya mawakili wa kujitegemea 1,322 idadi ambayo alisema ni ndogo ukilinganisha na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Jaji Jundu, aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Jaji Mkuu Agustino Ramadhani kufunga sherehe za kuwakubali na kuwasajili mawakili wapya 128.

Alisema mahitaji ya huduma ya mawakili, inazidi kuongezeka lakini idadi ya mawakili wa kujitegemea hapa nchini bado haikidhi mahitaji ukilinganisha na nchi kama ya Kenya ambayo ina zaidi ya mawakili 3,000.

”Nchi yetu ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na siku chache zijazo, itafungua milango ya soko la ajira kwa ajili ya raia wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo , chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja.

Kutokana na hali hiyo, mawakili kutoka nchi hizo watakuwa wakiruhusiwa kutoa huduma za kisheria katika mahakama za nchi jirani, hivyo idadi ya mawakili isipoongezeka, ni wazi Tanzania tutashindwa kufurukuta,”anasema Jaji Jandu.

”Hivyo, sisi kama mhimili wa mahakama nchini tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kuapisha mawakili wengi zaidi ili taifa liwe na mawakili wengi ambao wataenda kutoa huduma hii kwa wananchi,” anasema Jaji Jandu.

Jaji Jundu, alisema idadi ya mawakili wapya 128 imegawanyika katika mafungu mawili, kundi la kwanza ni waombaji 53 waliohitimu shahada ya sheria na baadaye kuhitimu katika chuo cha Wanasheria kwa Vitendo.

Anasema kundi hilo ni la kihistoria kwa vile hii ni mara ya kwanza kwa wanasheria wanaohitimu kutoka chuo hicho kukubaliwa kuwa mawakili kwa mujibu wa kifungu cha 12(3) cha Sheria ya Chuo hicho ya mwaka 2007.

Anasema kundi la pili, lina waombaji 75 ambao walipitia usaili wa Baraza la Elimu ya Sheria.

Alisema hapa nchini, mawakili wa kujitegemea wengi ofisi zao zina mawakili wasiozidi watatu au wakili mmoja hali inayosababisha baadhi ya wateja kusita kuwapatia kazi za kuwawakilisha mahakamani.

Hata hivyo, aliwashauri waombaji wa usajili wa uwakili ambao bado majina yao hayajapitishwa kuwa mawakili, wawasiliane na Baraza la Elimu la Sheria ambalo yeye ni mwenyekiti wake.

Kutokana maelezo hayo, Fukuto la Jamii linapenda kuunga mkono ushauri huo, uliotolewa na Jaji Kiongozi kwani safu hii inaona ushauri huo umejaa uzalendo endapo utafuatwa na wadau husika.

Itakumbukwa kwamba, Alhamisi wiki hii Tanzania ilifungua milango ya soko la ajira kwa ajili ya raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja iliyoanza kutekelezwa rasmi. Pia Fukuto la Jamii linapongeza utekelezaji huo.

Kwa sisi waandishi wa habari za mahakama nchini, tumeshuhudi kesi mbalimbali zikiahirishwa, wananchi wakikosa mawakili wa kuwawakilisha mahakamani kwa madai kuwa mawakili wao wana kesi katika mahakama zingine, wanaumwa au wamesafiri, hivyo inakuwa sababu moja wapo mahakama kuahirisha kesi kwa sababu ambayo nayo naweza kusema inachangia kesi kuchukua muda mrefu mahakamani bila kumalizika.

Kwa muda mrefu, wananchi wengi na baadhi ya viongozi wa serikali, wamekuwa hawaoni uhaba wa mawakili kama unachangia kesi kuchelewa mahakamani na badala yake wamekuwa wakiitupia lawama kila kukicha ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ambayo kwa sasa inaongozwa na Eliezer Feleshi.

Ni rai yangu kuwa mawakili wa kujitegemea nchini, waanze kujitazama upya na kuufanyia kazi ushauri huu uliotolewa na Jaji Jundu kwani tutake tusitake viongozi wa mataifa ya nchi za EAC ndiyo wameisharidhia.

Hakuna ubishi kwamba idadi ya mawakili hapa nchini ni ndogo, lakini licha ya idadi hiyo, kuwa ndogo bado mawakili wengi wamejenga kasumba ya kufungua ofisi mijini zaidi kulikoa mikoani ambako kuna wananchi wenzetu wanateseka kwa kukosa huduma hiyo muhimu.

Hivyo, wananchi wengi wanapoteza haki zao au wanakubali kwa shingo upande haki zao, zipotee kwa sababu ya kukosa mawakili wa kuwawakilisha mahakamani au mawakili wa kuwapatia msaada wa kisheria.

Ikumbukwe mawakili walipokuwa vyuoni kusomea fani ya sheria walifundishwa na walimu hawa waende wakatende haki na kulisaidia taifa kupitia taaluma yao hivyo tutaona si burasa kwa mawakili wetu kuamua kufungua ofisi mijini tu eti kwa kigezo kwamba mijini ndipo kuna biashara zaidi kuliko kwenda kufungua maofisi katika wilaya ambayo mikoa yake bado haijapiga hatua za kimaendeleo au kupandishwa hadhi ya kuwa jiji.

Inasikitisha kuona vyuo vikuu vyetu kila mwaka wahitimu wa fani ya sheria idadi yake inazidi kuongezeka lakini kila siku tunasikia baadhi ya viongozi wa mhimili wa mahakama wakitoa taarifa kwa umma kwamba mawakili wengi hawataki kwenda kufanya kazi mikoani.

Na pia inasikitisha kama siyo kukatisha tamaa kuona idadi kubwa ya waombaji wa kusajiliwa kuwa mawakili kwenye Baraza la Elimu la Sheria ,maombi yao yanashughulikiwa kwa idadi ndogo.

Pia inastaajabisha kusikia malalamiko kutoka kwa baadhi ya waombaji wa usaili wa uwakili kwamba wamewasilisha maombi yao muda mrefu lakini cha kushangaza kuna baadhi ya waombaji wanaowasilisha maombi yao kwenye Baraza la Elimu la Sheria wakiwa wamechelewa lakini mwisho wa siku waombaji hao waliochelewa ndiyo wanakuwa wakanza kupewa leseni za uwakili.

Ama kwa hakika malalamiko hayo hayaleti picha nzuri kwenye baraza hilo na mhimili wa mahakama na kama yana ukweli wowote tunamuomba Jaji Jundu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, ayafanyie kazi ili mwisho wa siku haki ipatikane kwa wote na kwa wakati.

Fukuto la Jamii, linamaliza kwa kuwashauri mawakili wa hapa nchini kuacha ubinafsi wa kufungua ofisi zinazokuwa na mawakili wa wiwili au mmoja, badala yake watanue ofisi zao ambazo zitakuwa namawakili wengi zaidi(Partners) , ili wakili mmoja siku hayupo wakili mwingine wa kampuni hiyo hiyo anashika kesi ya mteja husika na kuendelea nayo mahakamani, naamini wakifanya hayo wanaweza kushindana katika Itifaki ya Soko la Pamoja.

Kwani wananchi wa nchi za EAC wataweza kuja kuwakodi kuendesha kesi zao katika mahakama toka nchi za jumuiya zao bila ofisi zao kuteteleka kwani wakili mmoja akienda kuhudhuria kesi ya mteja mmoja, mfano nchini Kenya, ofisi yake ya uwakili hapa nchini kesi nyingine alizokuwa akizishikilia wakili huyo, zitaweza kuendeshwa na wakili mwingine katika ofisi hiyo ambayo itakuwa na mawakili wengi, hivyo kipato katika kampuni hiyo kitaongezeka.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili la Julai 4 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.