Header Ads

DHAMANA YA MTOTO WA KINGUNGE YAZUA UTATA

Na Happiness Katabazi

IKIWA ni siku moja tu tangu Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Gabriel Milumbe atoe masharti ya dhamana kwa mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini,Kingunge Ngombale Mwiru, Tonny Mwiru(36),anayekabiliwa na makosa ya kula njama,kuwasilisha nyaraka za uongo,kughushi na kujipatia sh milioni 424 kwa njia ya udanganyifu baadhi ya mawakili wa serikali wamesema wanakusudia kukatia masharti hayo ya dhamana Mahakama Kuu haraka iwezekanavyo.


Juzi Hakimu Milumbe alisema ili mshitakiwa huyo apate dhamana ni lazima asaini bondi ya Sh milioni 10 na kuwasilisha hati ya mali yenye thamani ya Sh milioni kumi na mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana akapelekwa mahabusu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jana mahakamani hapo, Mawakili Waandamizi wa Serikali na wale wa kujitegemea kwa masharti ya kutotaka majina yao walisema wameshtushwa masharti hayo ya dhamana yaliyotolewa na hakimu Milumbe kwani ni wazi kabisa yanakwenda kinyume na masharti ya dhamana yaliyoainishwa kwenye kifungu cha 148((5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Kifungu hicho cha sheria ya jinai kinasema wazi mshitakiwa yoyote anayekabiliwa na makosa ya fedha taslimu au mali ambazo zinazaidi ya thamani ya Sh milioni ,basi mshitakiwa huyo atapaswa awasilishe nusu ya fedha taslimu au hati ya mali yenye nusu ya thamani hiyo na sivinginevyo:

“Sasa kwenye kesi ya mtoto wa Kingunge anakabiliwa na makosa hayo yakujipatia sh milioni 424 lakini cha kushangaza hakimu Milumbe ametoa masharti ambayo yanajumla ya thamani ya Sh milioni 20….hivi katika akili ya kawaida nusu ya sh milioni 424 ni sh milioni 20?....tunajipanga kukatia rufaa uamuzi wa hakimu huyo kwani sheria ya makosa ya jinai bado haijabadilishwa na bunge hivyo hatufikirii kwamba sheria hiyo ilibadilika juzi kwasababu ya mtoto wa Kingunge kushitakiwa na ikashindwa kubadilika kwa washtakiwa wengine ambao ni wananchi wa kawaida wanapofikishwa mahakamani”alisema Wakili Mwandamizi wa Serikali ambaye aliomba jina lake liifadhiwe.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Democratic(DP),Mchungaji Christopher Mtikila alisema sheria ipo wazi na alishangazwa na uamuzi wa hakimu huyo ambao alisema umeipaka matope mahakama hiyo na kuongeza kwa kumuasa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),Eliezer Feleshi pamoja na vijana wake wakakate rufaa Mahakama Kuu kupinga masharti hayo ambayo yanasigina sheria ya nchini.

“Au huyo Tonny ni kwasababu ni mtoto wa mzee Kingunge ndiyo maana hakimu alibabaika na kujikuta anatoa masharti yanayokinzana na kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002?Au inapofika watoto wa vigogo kuburuzwa mahakamani ndiyo basi baadhi ya mahakimu wetu wanaamua kupindisha sheria makusudi?.

“Hii aikubaliki DPP na vijana wake tunataka wafanye haraka wakatie rufaa masharti hayo kwani watanzania wote bado tunakumbuka ni aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Nyigulila Mwaseba alilegeza masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 221 na DPP alikata rufaa Mahakama Kuu na Jaji Geofrey Shahidi alitengua masharti hayo ya Mahakama Kisutu na kutaka Liyumba apewe dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria hilo, lakini hadi Mei 24 mwaka huu, Mahakama hiyo Kisutu ina mhukumu kwenda jela miaka miaka mwili alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana.

Hata hivyo gazeti hili lilifanya jitihada za kuwasilisha na DPP-Feleshi ili kujua msimamo wa ofisi yake kuhusiana na madai hayo, simu zake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.

Kabla ya hakimu Milumbe kutoa masharti ya dhamana,alimtazama usoni Tonny sekunde kadhaa na kisha alimuuliza kama mzee Kingunge Ngombale-Mwiru ni baba yake , naye alijibu kuwa ndiyo.

“Ujue baba yako tunamheshimu sana, sasa kwanini wewe mtoto wake unajihusisha na mambo kama haya?”.Alihoji Hakimu Milumbe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 19 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.