Header Ads

KIFO CHA MWAIKUSA:PIGO KWA TASNIA YA SHERIA


Happiness Katabazi

WIKI hii tasnia ya wanasheria nchini, Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na taifa kwa ujumla lilipata pigo baada ya kuondokewa na gwiji la sheria nchini, Profesa Juani Timoth Mwaikusa (58), ambaye aliuawa kinyama kwa kumimiwa risasi mwilini mwake na watu wasiojulikana.

Licha ya wauaji hao kutojulikana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyela, ameuleza umma kuwa watu hao wanasadikiwa kuwa ni majambazi.

Vilio, mshtuko, kwiki, mshangao, wasiwasi na majonzi vilitawala ndani ya familia ya marehemu ambaye alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kada ya wanasheria na taifa kwa ujumla muda mfupi baada ya kupokea taarifa ya kifo hicho kilichotokea Julai 13 mwaka huu, saa nne usiku nyumbani kwa marehemu eneo la Salasala.

Katika mahojiano ya Tanzania Daima Jumapili na wanataaluma wa sheria walitoa maoni yao jinsi walivyomfahamu marehemu na mchango wake kwa taifa.

Jaji Mkuu wa Tanzania Agustino Ramadhani , alisema taifa limepoteza mtu hodari kwenye taaluma ya sheria.

Alisema wakati wa rufaa ya kesi ya mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila, marehemu alikuwa kiongozi wa jopo hilo akisaidiwa na Januari Msofe, Eusebio Munuo, Natalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk, Sauda Mjasiri na Bernard Ruhanda kusikiliza rufaa hiyo.

Marehemu aliitwa mahakamani kama rafiki wa mahakama kutoa maoni yake katika kesi hiyo na alifanya hivyo katika hukumu ya Mahakama ya Rufaa iliyoandaliwa na yeye na majaji wenzake sita, hawakukubaliana na maoni ya gwiji huyo wa sheria nchini lakini kutokubalina na mawazo yake si kukosana naye.

Ikumbukwe kuwa Aprili 11 mwaka huu, siku hiyo mvutano wa kisheria uliendelea katika Mahakama ya Rufaa, miongoni mwa magwiji wa sheria, ambao waliitwa kutoa maoni yao kama marafiki wa mahakama kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi nchini.

Magwiji hao ni Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi, Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (DDP), Othman Masoud na marehemu Profesa Juani.

Walikuwa wanaishauri Mahakama ya Rufaa kabla haijatoa hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka jana kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi, katika kesi hiyo.

Binafsi nimeguswa na msiba huo hasa ninapoikumbuka siku hiyo kwani Profesa Mwaikusa wakati akitoa maoni yake alikuwa pia akitumia mikogo ya wananasheria wanayoitumia wakati kesi zinaposikilizwa.

Mwaikusa alilieleza jopo lile kuwa ni suala la haki za binadamu na kwamba mahakama kwa mamlaka yake, haina kikomo cha kujadili haki hiyo.

Alisema Katiba ya nchi ipo kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na kwa msingi huo haki za binadamu ni mama wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kuongeza kuwa kama kuna kifungu kinavunja haki za binadamu. basi kifungu hicho ni wazi kinakiuka haki za binadamu.

“Kwa uamuzi ule wa Mahakama Kuu wa kubatilisha vifungu vya ibara 21(1) (c), 39(1) (c) (b) na 69(1) (b) za Katiba ya nchi, kama kuna ibara zinapingana, ibara inayopaswa kutumika ni ile inayolinda haki za binadamu na kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kutamka ibara hizo ni batili kwani Katiba inalinda haki za binadamu na haki hizo za binadamu zilianza, Katiba ikafuata, hivyo haki hizo ni sheria mama.”

Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, anasema yeye na ofisi yake wameshtushwa na taarifa hiyo, kwani Mwaikusa enzi ya uhai wake alifanya kazi kwa uadilifu mkubwa.

“Katika kesi hizo mbili Profesa Mwaikusa alikuwa akiudhuria kama rafiki wa mahakama wakati si wakili, hivyo umuhimu wake haukuwa kwenye taaluma yake ya uwakili bali hata rafiki wa mahakama.

Kifo chake ni changamoto kwa jamii kuwafichua waahalifu na kuviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili viweze kupambana uhalifu.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu, anasema Mhimili wa Mahakama nchini, ulimfahamu marehemu kuwa ni mchapa kazi shupavu, aliyetoa hoja zilizosaidia kupata ufumbuzi wa kesi mbalimbali.

Alisema marehemu alikuwa mwanataaluma aliyekuwa akijiandaa vyema kabla ya kuingia kwenye kesi, hivyo baadhi ya hukumu mbalimbali ambazo amepata kuzisimamia kama wakili, zitaendelea kuwa kumbukumbu na kutumika na mahakama kufikia maamuzi ya kesi mbalimbali na wanafunzi wa sheria vyuoni kuzitumia.

Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Paramaganda Kabudi, anasema kifo hicho ni pigo kwani marehemu alikuwa mtafiti mahiri na msomi makini kwa wanafunzi na walimu wake na alikuwa mwenye vipaji vingi kwani mbali na taaluma yake ya sheria pia alikuwa mshahiri mzuri wa mashahiri aliyoyatunga kwa lugha ya Kiingereza ambayo ameyaweka kwenye kitabu cha ‘Summons Poems of Tanzania’.

Mwadhiri Mwandamizi kutoka kitivo hicho, Dk. Sengondo Mvungi, ambaye pia ndiye aliteuliwa na kitivo hicho kuongoza shughuli ya mazishi, anamwelezea marehemu kama mtaalamu mzuri na mwenye msimamo wa kutetea wananchi.

Wakili wa kujitegemea na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini, Alex Mgongolwa, anamwelezea Profesa Mwaikusa kwamba alikuwa miongoni mwa mawakili walioendeleza sheria kwa kiwango cha juu na kutolea mfano kwamba alikuwa Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba (CCM) aliyefungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa Jimbo la Bunda ambayo yalimtangaza Steven Wassira (NCCR) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 kuwa mshindi.

Wassira ambaye hivi sasa ni Waziri wa Kilimo , Chakula na Ushirika alishinda kesi hiyo na hivyo ushindi wa Wassira ulitenguliwa na Mahakama Kuu mwaka 1996.

“Na hoja ya rushwa kwenye uchaguzi ambayo ilitolewa kwenye kesi hiyo na Profesa Mwaikusa kwamba mgombea akitoa vitu vidogo vidogo kwa wapiga kula ni rushwa na hoja yake hiyo ilisababisha Bunge kutunga sheria ya Takrima ya mwaka 1998, kwakweli nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo cha marehemu ambaye alikuwa mwalimu wangu na ninaomba polisi wafanye uchunguzi wa kina ili hatimaye washitakiwa wafikishwe mahakamani,” alisema Wakili Mgongolwa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani nchini, Edson Mkasimongwa, anasema marehemu alikuwa mwalimu wake katika kipindi cha 1997-2000.

Anasema marehemu alikuwa muungwana, asiye na vishindo na aliyekuwa tayari kusaidia kitaaluma na kumshauri mtu yeyote alipomjia kumuomba msaada, alifanya kila aliloweza na kuonyesha uwezo wake katika kufundisha wanafunzi na kwa sababu hiyo, wanafunzi wa sheria wamepoteza mwalimu mzuri.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP), Charles Kenyela, anasema Jeshi la Polisi na yeye binafsi wamepokea kwa masikitiko makubwa ya kifo hicho na kuahidi kuwasaka kwa udi na uvumba wauaji hao.

Kenyela ambaye ni mwanasheria kitaaluma anasema binafsi anahuzunishwa na msiba huo kwani marehemu alikuwa ni mwalimu wake wa sheria.

Meja Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Alfred Mbowe, anasema anamlilia Profesa Mwaikusa kwa sababu marehemu alikuwa mwadilifu na siku zote alikuwa mwana taaluma anayesimamia haki na usawa na kuongeza kuwa kifo chake kimemshtua na kuomba vyombo vya dola vifanye upelelezi wa kina ili kuwabaini waliohusika na unyama huo.

Sisi tulimpenda sana Profesa Mwaikusa lakini Bwana amempenda zaidi. Bwana ametoa na bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe. Amina.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Julai 18 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.