Header Ads

POLISI WALINILAZIMISHA NITOE MAELEZO YA KUMKANDAMIZA JERRY MURRO-MUGGASA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji wa Taifa(TBC1),Jerry Murro na wenzake, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu , usipokee maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu(Deogratius Mugassa) kwa maelezo kama kielelezo kwa madai kwamba mshtakiwa aliteswa na polisi wakati akichukuliwa maelezo hayo.


Sambamba na hilo baadhi ya wananchi wakiwemo waandishi wa habari wamelalamikia hatua ya kesi hiyo ambayo inavuta hisia za watu wengi kuendeshewa chemba, kwani wananchi hao na waandishi wa habari wengi wanashindwa kuingia kusikiliza kesi hiyo kwasababu ya uhaba wa nafasi na kuongeza kuwa wanashangazwa na hatua hiyo kwani wakati mwingine mahakama za wazi za mahakama hiyo zinakuwa wazi lakini hakimu huyo anaendeshea kesi hiyo inaendeshewa chemba na kuuomba uongozi wa mahakama ufanye kila linalowezekana kesi hiyo iwe inasikilizwa katika mahakama ya wazi.

Ombi hilo liliwasilishwa kwa njia ya mdomo jana na wakili wa utetezi Majura Magafu mbele ya Hakimu Mkazi Gabrile Milumbe ikiwa ni sekunde chache baada ya shahidi wa kwanza wa upande mashitaka,Staff Sajenti Peter Jumamosi alikuwa akiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Stanslaus Boniface kutoa ushahidi wake na akaomba atoe maelezo hayo ya onyo ya Muggasa kama kielelezo.

Magafu alidai mteja wake(Muggasa) anaiomba isipokee maelezo hayo kama kielelezo kwasababu Februali 3 mwaka huu, wakati anachukuliwa maelezo hayo na shahidi huyo, aliteswa na alikuwa akishinikizwa na Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZDCO),Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Mkumbo na Kamishna Kasala ambao walimtaka mshtakiwa huyo atoe maelezo yatakayomgandamiza mshatiwa wa kwanza(Murro) ambaye jeshi la polisi limekuwa likimsaka muda mrefu kwasababu amekuwa akiwadhalilisha kwenye vyombo vya habari.

“Naomba mahakama isipokee kilelezo hiki kwani mteja wangu amenieleza alinyanyaswa wakati akichukuliwa maelezo na alilazimishwa na polisi akubaliane na maelezo wanayoyataka polisi..na manyanyaso aliyopata ni aliambiwa atoe maelezo yatakayomkandamiza Murro kwasababu polisi wanamtafuta muda mrefu kwani amekuwa akiwadhalilisha na wakati mteja wangu anachukuliwa maelezo hayo ZDCO-Mkumbo, Kamishna Kasala walikuwepo pembeni ambapo walikuwa wakimuamrisha shahidi huyo(Jumamosi) achukue maelezo ya mshtakiwa huyo ambayo yanamgandamiza Jerry Murro na kwamba hayo yalikuwa ni maelekezo maalum toka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi”alidai Magafu.

Baada ya Magafu kumaliza kuwasilisha pingamizi hilo la kupinga kielezo hicho kisipokelewe, Hakimu Milumbe alisema anatoa amri ya usikilizaji wa kesi ya msingi usimame na kuiairisha kesi hiyo hadi leo ambapo kesi ndani ya kesi(trial within a trial) itakapoanza kusikilizwa na kaumuru pande zote zilete mashahidi kama wanao.

Februali mwaka huu, Murro, Edmund Kapama na Muggasa walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa ya kushawishi na kuomba rushwa toka kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamayo Michael Wage.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Agosti 19 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.