Header Ads

KIZIMBANI KUJIFANYA POLISI

Na Happiness Katabazi

MSHTAKIWA wa tatu katika kesi ya kuomba rushwa ya Sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1),Jerry Murro, Deogratius Mgassa kwa mara nyingine tena jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na kesi mpya ya kujifanya ni Ofisa wa Jeshi la Polisi na kisha kujipatia sh milioni 19 kwa njia ya udanganyifu.


Mbele ya Hakimu Mkazi Devota Kisoka, Wakili wa serikali Zuberi Mkakatu alidai kuwa Mugassa anakabiliwa na mashtaka matatu.Shitaka la kwanza ni la kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwamba mshtakiwa huyo na wenzake ambao hawapo mahakamani.

Wakili Mkakatu alidai shtaka la pili ni la Mugassa kujifanya Ofisa wa Jeshi la Polisi kwamba Aprili 28 mwaka huu, katika Bar ya Rose Garden huko Mikocheni, yeye na wenzake walijitambulisha kwa Rose Azizi kuwa wao ni maofisa wa jeshi la polisi.

Mkakatu alidai shitaka la tatu ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwamba kati ya Mei na Aprili mwaka huu, katika Bar hiyo ya Rose Garden walijipatia sh milioni 19 kutoka kwa Rose Azizi baada ya kujifanya wao ni maofisa wa jeshi hilo na kwamba fedha hizo walizopewa watazitumia kuweka mtego wa kuwakamata wezi walioiba matofari mawili wa madini ya dhahabu wilayani Nzega.

Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana mashitaka yote matatu na wakili Mkakatu aliambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo anaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe ya kutajwa.

Aidha Hakimu Mkazi Kisoka alisema ili mshtakiwa huyo apatiwe dhamana ni lazima yeye mwenyewe ajidhamini fedha taslimu sh milioni 10 au kuwasilisha hati yenye thamani hiyo na pia awe na wadhamini wawili ambao wanasaini bondi ya sh milioni 10.Hata hivyo mshitakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo ya dhamana na amerudishwa rumande hadi Agosti 25 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja tena kwaajili ya kutajwa.

Hii ni kesi ya pili tofauti inayomkabili Mugassa mahakamani hapo.Kesi ya kwanza ni ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili yeye na Jerry Murro na Edmund Kapamba ambayo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Gabrile Mirumbe, ambapo wanakabiliwa na mashitaka matatu, likiwemo la kula njama za kutaka kupokea rushwa kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage ambapo pia wanadaiwa kujifanya wao ni maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU).

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 13 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.