Header Ads

JAJI MKUU ANUSURIKA AJALINI

Na Happiness Katabazi

JAJI Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, amepata ajali katika eneo la Simbo mkoani Tabora baada ya gari alilopanda kupinduka na kugonga kisiki.
Taarifa zilizolifikia Tanzania Daima jana asubuhi kutoka mkoani Tabora, zimedokeza kuwa Jaji Ramadhani alipatwa na ajali hiyo wakati akiendelea na ziara ya kukagua Tume ya Utumishi wa Mahakama.


Gari la Jaji Mkuu lilipinduka mara moja na kisha kuanza kuserereka lakini likazuiwa na kisiki; jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limezuia kutokea kwa maafa zaidi.

Tanzania Daima, iliwasiliana na Jaji Ramadhani na alithibitisha kupata ajali katika eneo la Nzega alipokuwa akitokea mkoani Singida kwa shughuli za kikazi.

Alisema walipofika eneo la Nzega ndipo gari lake lilipopata ajali; lakini hata hivyo alisema hali yake inaendelea vizuri kwa sababu hakupata majeraha.

“Eh! Yaani tayari gazeti lenu limeishapata habari kuhusu mimi kupata ajali? Ni kweli gari nililopanda aina Land Cruiser V8 limepata ajali lakini nashukuru tumetoka salama,” alisema.

Jaji Mkuu aliongeza kuwa mlinzi na dereva wake pia wametoka salama katika ajali hiyo na walibadilishiwa gari jingine baada ya mkasa huo na kuendelea na safari.

Jaji Ramadhani alibainisha kuwa katika ziara hiyo ameongozana na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, Jaji Ibrahim Juma, Wakurugenzi wa tume hiyo, na maofisa wengine wa mahakama.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 10 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.