Header Ads

WASHITAKIWA FEDHA HARAMU WABADILISHIWA MASHITAKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kula njama na kuhamisha fedha kwa njia haramu sh milioni 338.9 inayomkabili Ofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Justice Katiti na wenzake watano umebadilisha hati ya mashitaka.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Alocye Katemana, jana Wakili Kiongozi wa Serikali, Fredrick Manyanda, aliyekuwa akisaidiana na Mkuu wa Idara ya Sheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincoln, waliiambia mahakama kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili kubadilisha hati ya mashitaka.

Wakili Kiongozi wa Serikali Manyanda alisema kwa mujibu wa hati hiyo ya mashitaka ambayo mashitaka yote kumi yalikuwa yakiwakabili washitakiwa wote na kwa mujibu wa mashitaka hayo washitakiwa wote hawapaswi kupewa dhamana lakini kutokana na mabadiliko hayo, wameamua kumuondoa mshitakiwa wa sita, Joseph Rutto, katika shitaka la sita na saba ambayo ni mashitaka ya kuhamisha fedha kwa mtandao kwa njia ya haramu na badala yake mshitakiwa huyo atakabiliwa na shitaka la kwanza ambalo ni la kula njama ambalo kisheria linadhaminika.

Manyanda alieleza kuwa kwa mabadiliko hayo washitakiwa wengine watano wataendelea kukabiliwa na mashitaka yote.

Aidha, Hakimu Katemana alisema ili Rutto apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watatoa nusu ya kiasi hicho cha fedha au watawasilisha hati za mali zenye thamani ya nusu ya kiasi hicho cha fedha.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 9 mwaka huu, itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Fortunatus Muganzi, Robert Mbetwa, Gidion Otullo na Godwin Paulla ambao kwa pamoja wanadaiwa Septemba 29 mwaka 2008, jijini Dar es Salaam, walighushi maombi ya ujumbe wa kasi wa kuhamisha fedha Na. E.17 wa Benki ya Barclays na unaoonyesha kwamba Kampuni ya Tourism Promotion Services (Tanzania) Limited unaiomba benki hiyo uilipe Kampuni ya East Africa Procurement Services Limited Tanzania, sh milioni 338.9 kwa sababu ilifanya kazi ya kuuza maturubai na vifaa vya hoteli, huku wakijua si kweli.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 5 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.