Header Ads

HAKIMU ATISHIA KUIFUTA KESI YA JERRY MURRO

Na Happiness Katabazi

HAKIMU Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Gabrile Milumbe, ameuchachamalia upande wa utetezi katika kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Muro, na wenzake kwamba kama haupo tayari kuendelea na kesi hiyo, ataifuta.
Mbali na Murro washtakiwa wengine ni Deogratius Mgasa na Edmund Kapama wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Pascal Kamala.


Hakimu huyo alitoa angalizo hilo baada ya wakili wa Serikali Zuberi Mkakatu, kuiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo iliyokuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka kwa madai kuwa wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, ambaye amekuwa akiendesha shauri hilo tangu awali, yuko likizo.

Baada ya wakili huyo kutoa maelezo hayo, Hakimu Milumbe alisema hayuko tayari kuahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo jana na kuongeza kuwa kama upande wa serikali hauko tayari kuendelea nayo, ataifuta kesi hiyo.

Hata hivyo hakimu huyo ambaye alionekana kukerwa na upande wa serikali kuahirisha kesi hiyo kila mara, aliamua kuiahirisha kwa nusu saa na baadaye kuamuru shahidi wa upande wa mashtaka aanze kutoa ushahidi wake.

Majira ya saa nne asubuhi, pande zote mbili ziliingia tena mahakamani, huku umati wa watu ukiwa umefurika kusikiliza kesi hiyo ambayo imekuwa ikivuta hisia za wengi.

Akitoa ushahidi wake, shahidi wa kwanza upande wa mashtaka, Staff Sajenti, Peter Jumamosi, alidai kuwa Februari Mosi mwaka huu wakati akiwa ofisini kwake katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati, bosi wake ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Charles Mkumbo, alikuja na watuhumiwa wawili wa kesi hiyo ili achuke maelezo yao.

“Siku hiyo, nikiwa ofisini pale katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati, ilipofika majira ya saa tisa, bosi wangu ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZDCO), Charles Mkumbo, alikuja na watuhumiwa wawili, akanipa mtuhumiwa wa pili, Deogratius Mgasa, nimhoji kuhusiana na madai ya kuomba rushwa,” alidai Peter Jumapili.

Wakati akitoa maelezo hayo, shahidi huyo alikatishwa na swali la Hakimu Milumbe ambaye alimuulizwa wakili wa serikali yalipo maelezo ya onyo ya mshtakiwa Mgassa na kujibiwa kwamba hawana maelezo hayo.

Wakili huyo wa serikali alidai kuwa maelezo hayo bado yako polisi, hali iliyosababisha hakimu kumtaka shahidi asitishe kutoa ushahidi kwa sababu mahakama haiwezi kusikiliza ushahidi wake bila kuwepo maelezo ya onyo.

“Lazima tufuate taratibu za kimahakama…mi’ sipendi kupoteza muda bure, awali tulikubaliana upande wa jamhuri mlete mashahidi watano kwa siku mkakubali …sasa hao mashahidi watano mliokubali kwamba mngewaleta leo (jana) wako wapi? Naairisha kesi hii hadi kesho (leo) na mashahidi watano hakikisheni wanafika bila kukosa,” alisema Hakimu Milumbe.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kula njama za kutaka kupokea rushwa kutoka kwa aliyekuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Agosti 11 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.