Header Ads

UJAMBAZI HUU TUUWEKEE MIKAKATI KUUTOKOMEZA

Happiness Katabazi

HIVI sasa kumeibuka aina mpya ya ujambazi ambapo mtu anapotoka kwenye mihangaiko yake ya kila siku hufuatiliwa kila anakokwenda na hatimaye kuuawa.

Uhalifu huu unalitia doa taifa letu ambalo kwa miaka mingi limekuwa na sifa ya amani na utulivu licha ya kuwapo kwa matukio ya kinyama yanayotokea mara moja moja.

Aina hii ya uhalifu inafanywa na watu ambao naweza kusema si wenye kuhitaji mali za wahusika bali roho zao, kwa kuwa kila wanapofanya uvamizi hawachukui chochote isipokuwa kuyakatisha maisha yao.

Watu wanaouawa ni tegemeo kubwa taifa na familia zao kwa hiyo vifo vyao husababisha huzuni na kusuasua kwa maendeleo yaliyokusudiwa.

Kadiri tunavyozidi kwenda mbele ndivyo jamii inavyozidi kuingiwa na roho za kikatili zilizojaa tamaa ya fedha na kisasi ambavyo ni kukiuka maagizo ya Mungu ya kupendana, kushirikiana.

Mwingiliano wa jamii tofauti katika nchi zinazotuzunguka na ukuaji wa teknolojia ya sayansi (utandawazi), umasikini na sababu nyinginezo ni miongoni mwa mambo yanayochangia kushamiri kwa uhalifu hapa nchini na duniani kwa ujumla.

Uanzishaji wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC) unaweza kuwa chachu ya kuongezeka kwa vitendo hivyo, kwa kuwa wananchi wa nchi wanachama wana uhuru wa kuingia na kutoka katika nchi zilizomo kwenye jumuiya hiyo bila ya kuwepo kwa vikwazo kama vilivyokuwapo awali.

Baadhi ya wananchi niliozungumza nao wameanza kuingiwa na wasiwasi kwamba kuzuka kwa aina hiyo mpya ya ujambazi ni matokeo ya nia njema ya viongozi wetu kuridhia kutekelezwa na Itifaki ya Soko la Pamoja la nchi za EAC?

Ujambazi wa kutumia mabomu ambayo mara kwa mara tumekuwa tukisikia yakitumika nchini Somalia na hivi karibuni ulijikita katika mji wa Kampala nchini Uganda na raia wa Uganda 75 waliuawa na bomu lililolipuka wakati wananchi hao wakitazama fainali ya Kombe la Dunia zilizomalizika Julai 11 mwaka huu.

Baadhi ya wananchi wa Somalia wanaanza kufaidika na utekelezaji wa Soko la Pamoja ambalo moja ya misingi ya soko hilo inatoa haki watu kuzagaa katika nchi za Afrika Mashariki bila vizuizi na kufanya kazi.

Sasa tunapofungua mipaka ya nchi yetu watu waingie kutoka Kenya,Uganda, Rwanda na Burundi waingine Tanzania kutafuta ajira na kuwapatia haki ya kuhamia (right of establishment).

Lakini aina ya ujambazi wenye ukatili na unyama wa kupindukia kwa wanapoenda kuua watu bila kupora hata kitambaa cha kujifutia jasho, ni mpya, hatujawahi kuusikia hapa nchini ndiyo maana tunapata woga wa kufanya shughuli zetu.

Uhalifu ambao mara kwa mara umekuwa ukitumika hapa nchini ni ule wa watu kuvunja nyumba za watu na kupora mali, kuiba benki na wakati mwingine ukisikia kuna vifo vimetokea kwenye tukio la uporaji ujue kulikuwa na ubishani kati ya mporaji na mporwaji.

Matukio ya kukatisha maisha ya watu pasi kuchukua chochote ni nadra kuyasikia lakini sasa yanaanza kushamiri kwa kasi ya aina yake huku yakiwahusisha zaidi watu wenye nyadhifa fulani au wafanyabiashara wakubwa.

Tanzania inapaswa kuwa makini zaidi hivi sasa ambapo tumeingia kwenye jumuiya ya ushirikiano wa Afrika Mashari kwani kuna majirani zetu ambao baadhi yao bado mikono yao inachuruzika damu za mauaji ya kimbari.

Mfano katika mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 , mauaji yote yaliyotokea kabla ya tarehe ile iliyowekwa na Umoja wa Mataifa(UN), yana sura ya kimbari vile vile.

Lakini ukiyachunguza mauaji hayo yatawanasa hawa ambao ni wahanga wa mauaji ya baadaye.

Kwa hiyo ina maana kama Wahutu waliua na Watutsi na wakalipiza kisasi. Unapotambua mauaji ya pili ya mwaka 1994 ambapo baadhi ya Watutsi waliuawa na Wahutu, bado haujagusa wala kuutoa mzizi wa fitina.

Sasa leo hii serikali iliyopo madarakani nchini Rwanda chini ya Rais Paul Kagame iliwahi kusikika ikilalamikia adhabu ndogo wanazopewa washitakiwa wa mauaji ya kimbari wanaoshtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari (ICTR) yenye makao yake makuu mjini Arusha.

Serikali hiyo inaona adhabu hizo ni sawa na kuwapa huduma bora wauaji ambao hawakujali utu wa wenzao wakati wakifanya au kuhamasisha ukatili.

Ndiyo maana sasa tutaona vituko vya mauaji kwa mtindo mpya yanaanza kutokea hapa nchini. Na katika kuhamishia mtindo huo mpya wa uuaji hapa kwetu, ndipo Watanzania hata wanataaluma wetu kama aliyekuwa Mhadhiri mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Juani Mwaikusa (58) aliuawa wiki iliyopita.

Wapangaji wa mauaji ya kimbari ni sawa kama watuhumiwa na washtakiwa wa kesi za mauaji hayo, ambayo kimsingi ni sawa na ujambazi.

Kwa hiyo kila tukio la mauaji yakitokea litakuwa na sura ya ujambazi kama tukio la mauji ya Profesa Mwaikusa.

Sisi Watanzania tungependa kuliasa Jeshi la Polisi kwamba wanachoweza kufanya ni kutambua kwamba mazingira ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yamebadilika. Ulinzi na usalama ni jambo gumu na nyeti.

Uwepo wa vitendo vya ujambazi vinavyolitikisa taifa letu hivi sasa visipojulikana chimbo lake ni nini, tutafikia hali ya mabomu kulipuana mitaani.

Sheria zetu za ulinzi na usalama nazo ni vema zikatupiwa jicho ili usalama wa raia na mali zao usiwe shakani kama ilivyoanza kujionyesha hivi sasa.

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jeshi la Polisi IGP), Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza ni vizuri yakafanya kazi pamoja ili kudhibiti hali hii.

Yaweke mikakati mipya ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji ambao baadhi yao wana hulka na kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

Vyombo hivyo vya ulinzi na usalama vijaribu kuzuia watu ambao wana historia ya uhalifu nchini mwao, kwa kuwazuia kuingia nchini kufanya chochote, iwe ni kutembea, kufanya kazi au kufanya biashara.

Kwahiyo, mabalozi wetu wa nchi za nje wafanye hiyo kazi, hatutaki watu wenye historia za kihalifu kuja hapa nchini kwetu. Na hilo likifanikiwa litakuwa limefanikiwa kuvunja minyororo ya wahalifu hapa nchini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili,Julai 25 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.