Header Ads

NILIWAKAMATA WATUHUMIWA WAWILI-SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza wa upande wa Jamhuri Konstebo Shaha Mbengwa(31) katika kesi ndogo inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la (TBC1),Jerry Murro ya kuomba na kupokea rushwa ya sh milioni 10, ameieleza mahakama kuwa ni yeye ndiye aliyemkamata mshtakiwa wa pili na watatu Edmund Kapama na Deogratius Muggasa.


Mbengwa ambaye alikuwa akitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Milumbe huku akiongozwa kutoa ushahidi huo na Wakili Mkuu wa Serikali Stanslaus Boniface jana wakati kesi ndogo (trial within a trial) jana ilipoanza kusikilizwa ikiwa ni siku moja tu baada ya hakimu huyo kutoa amri ya kusimamisha usikilizwaji wa kesi ya msingi.

Mbengwa ambaye ni askari kanzu na anafanyakazi katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZDCO),Charles Mkumbo, alidai kuwa Januari 31 mwaka huu, Mkumbo alimpatia kazi ya kuwasaka washtakiwa hao wawili na kisha awapeleke ofisini kwake na akaeleza kuwa siku hiyo hakufanikiwa kuwakamata lakini ilipofika Februali mosi mwaka huu, alifanikiwa kuwakamata washtakiwa hao maeneo ya Kinondoni saa nne asubuhi.

Alieleza kuwa baada ya kuwakamata washtakiwa,wakati wanaanza safari ya kuwalete Kituo Kikuu cha Polisi Kati(Central) , njiani Muggasa alianza kutaka kugoma kupelekwa kituoni kwa maelezo kwamba siku hiyo ilikuwa ni siku yake anayotakiwa kwenda Makao Makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) kuripoti kwani nako huko alikuwa anakabiliwa na tuhuma zingine zinazomkabili.

“Kwasasabu nilikuwa na ofisa mwenzangu ,tulimkubalia hilo ombi lake na tukampeleka hadi TAKUKURU kweli akaripoti kisha akarudi nje tulipokuwa tukimsubiri tukaanza safari ya kuelekea ofisini kwa ZDCO ambapo tulifika ofisini kwa afande Mkumbo saa saba mchana”alidai Konstebo Shaha Mbengwa.

Baada ya kutoa maelezo hayo, karani mmoja wa mahakamani hapo alipenyesha karatasi iliyokuwa ikienda kwa hakimu Milumbe ambapo hakimu huyo aliisoma karatasi hiyo na kisha kutangaza ndani ya chemba kwamba amepata ujumbe kutoka uongozi wa juu wa mahakama unaomtaka atoke ndani ya chemba aende kuendeshea kesi hiyo inayofuta umati mkubwa wa watu kwenye mahakama ya wazi na akairisha kesi hiyo hadi saa saba mchana.

Lakini katika hali isiyotarajiwa ilipofika saa 6:10 mchana, Hakimu Milumbe aliwaita washitakiwa na mawakili wa utetezi Pascala Kamala,Majura Magafu na wakili Mkuu wa Serikali, Stanslaus Boniface ambaye awali alisema upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ndogo kwa jana umeleta mashahidi wa tano akiwemo ZDCO-Charles Mkumbo, kwamba hataweza kusikiliza kesi hiyo saa saba mchana kwasababu anajisikia vibaya hivyo akaiairisha hadi leo saa nne asubuhi.

Aidha tango hilo la kuamishwa kwa kesi hiyo toka chemba kupelekwa mahakama ya wazi, kuliwafurahisha umati wa watu wakiwemo waandishi wa habari za mahakama ,washtakiwa wenyewe, maaskari polisi, wanafunzi wa sheria ambao wanakuja mahakamani hapo kuudhulia mafunzo kwa vitendo na wananchi mbalimbali walisema wamefurahishwa sana na uamuzi huo wa uongozi wa mahakama kwani walikuwa wakisimama madirishani, na wengine kulazimika kusimama nje huku wasifahamu kinachoendelea ndani ya kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne Agosti 20 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.