Header Ads

JAJI KIONGOZI NAYE APATA AJALI

Na Happiness Katabazi

SIKU mbili tu baada ya Jaji Mkuu wa Tanzania Agustino Ramadhani anusurike kifo katika ajali mbaya ya gari, jana Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, Fakihi Jundu naye amenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kupata ajali mbaya ya gari.
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka ndani ya msafara wa Jaji Jundu, zinasema ajali hiyo ilitokea jana saa 7:45 mchana kilometa chache kufika Wilaya ya Kasuru mkoani Kigoma.


Msafara huo, ulikuwa ukitokea mkoani Shinyanga kuelekea mkoani Kigoma akitumia gari aina ya Toyota Land Cruser V8 akiwa na mlinzi wake, lilipinduka na kuingia porini.

Baada ya ajali hiyo, Jaji Jundu alikimbizwa kwenye hospitali ya Wilaya ya Kasuru kwa ajili ya matibabu.

Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Francis Mutungu, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema hali ya Jaji Jundu si nzuri kutokana na majereha aliyopata.

‘Ni kweli Jaji Jundu amepata ajali ya gari na hivi sasa ofisi yangu inafanya jitihada za kumrejesha Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu na kwamba hata Jaji Mkuu ambaye Jumatatu wiki hii naye alipata ajali ya gari akiwa kwenye msafara huo wa ziara ya kukakugua Tume ya Utumishi wa Mahakama nchini, tayari amerejeshwa Dar es Salaam kwa ajili ya kukaguliwa afya yake,” alisema Mutungi.

Jumatatu wiki hii, Jaji Mkuu Augustino Ramadhani, alipata ajali katika eneo la Simbo mkoani Tabora baada ya gari alilopanda kupinduka na kugonga kisiki.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Agosti 12 mwaka 2010





No comments:

Powered by Blogger.