Header Ads

BP YAFICHUA SIRI YA MGOMO

Na Happiness Katabazi

KAMPUNI ya BP Tanzania Limited imefichua siri kwamba ingeendelea kuuza mafuta yake kwa bei elekezi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji(EWURA), ingeingia hasara ya sh. bilioni 3.1.


Mbali na hasara hiyo, BP Tanzania Limited ilieleza kuwa Benki isingewaruhusu kukopa zaidi ya dola milioni 30 (zaidi ya shilingi bilioni 40) kuingiza nishati hiyo, itashindwa pia kulipa mkopo wake benki na kushindwa kulipia gharama za mzigo wa mafuta waliouingiza nchini.

Kwa mujibu wa barua ya BP Tanzania limited ya Agosti 10 (Tanzania Daima inayo) iliyosainiwa na Mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo Philemon Felix kwenda kwa wnaahisa ambao ni serikali ya Tanzania iliyowakilishwa na Kaimu Msajili wa Hazina, Geoffrey Msella na mwana hisa mwingine Sipho Maseko/Richard King wa BP Afrika Pty wa Johannsburg, Afrika Kusini, mwenyekiti huyo aliwaeleezea wanahisa hao juu ya tatizo hilo.

Felix katika barua hiyo alisema kuwa kikao cha bodi ya BP kilichokutana siku hiyo kilitoa maamuzi kuwa kuna umuhimu wa haraka wa wanahisa hao kukutana kujadili mustakabali na hatma ya kampuni hiyo endapo watatekeleza agizo la Ewura la kupunguza bei ya mafuta.

Alisema kwa kipindi hicho kampuni ilikuwa na akiba ya mafuta ya petroli lita milioni mbili ambazo zingetumika kwa siku 10 na dizeli lita milioni 11 ambazo zingetumika kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mwenyekiti huyo wa bodi alieleza kuwa pia waliiandikia barua Ewura kuelezea mazingira hayo yanayoikabili kampuni.

Nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Kamishina msaidizi wa Nishati (petroli na gesi) wa wizara hiyo.

Uchunguzi umebaini kuwa Hazina iliipokea barua hiyo Agosti 11, mwaka huu wakati mwanahisa mwingine wa Afrika Kusini aliipokea barua hiyo siku hiyo hiyo aliyoandikiwa na kumwandikia mwanahisa mwenzake ambaye ni serikali ya Tanzania kupitia msajili wa hazina.

Katika barua hiyo ya mwanahisa wa Afrika Kusini, alimtaka mwanahisa mwenzake (Tanzania) kufanya jitihada za kukutana ili kujadili mazingira magumu yanayoikabili kampuni hiyo kwa Tanzania.

Katika barua hiyo, mwanahisa huyo aliitaka serikali ya Tanzania itakapofika kwenye mkutano huo kwanza iwe inafahamu kwa kina agizo la Ewura, athari zinazoweza kuikumba kampuni hiyo na nini hatma ya kampuni hiyo nchini Tanzania kwa wanahisa hao.

Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa serikali ilishindwa kujibu barua hiyo ya bodi na hata ile ya mwanahisa mwenzake juu ya kuandaa mkutano huo.

Habari kutoka ndani ya bodi ya BP Tanzania Limited zinaeleza kwamba vikao vya bodi viliendelea kujadili hali hiyo huku ikisubiri maelekezo kutoka serikalini, lakini serikali iliendelea kukaa kimya hadi Ewura ilipoamua kuiffungia BP kutofanya biashara hiyo kw akipindi cha miezi mitatu.

Chanzo chetu kutoka ndani ya bodi hiyo kiliwataka Watanzania kwanza kuelewa muundo wa bodi ya BP Afrika uko vipi ikiwa ni pamoja na mwenyekiti kutokuwa na kura ya veto.

“Hapa nataka Watanzania waelewe muundo wa kampuni ya BP ukoje. BP Afrika ina hisa 50 na Serikali ya Tanzania ina hisa 50 na Tanzania mwenye mali hiyo ni Msajili wa Hazina. Kwa mtiririko huo ndiyo tunapata BP Tanzania na katika BP Tanzania ndiyo tunaipata Bodi ya BP Tanzania.

“Kwa hiyo Tanzania inatoa Mwenyekiti wa Bodi na wajumbe wanne na upande wa BP Afrika nayo kwenye bodi inakuwa Katibu wa bodi na wajumbe wa nne na kwamba shughuli zote za utawala za wanahisa zinatawaliwa na BP Afrika na Mwenyekiti wa Bodi ambaye anatoka Tanzania anakuwa hana kura ya Veto ya kuamua jambo hata kama mwanahisa mwenzake halitaki.

“Sasa kwa mtindo huo mlitaka bodi ya BP ifanye nini? Ieleweke wazi kwamba sisi wajumbe tulichaguliwa kuwa wajumbe ili kwenda kuiendeleza BP kwa faida na siyo kuiletea hasara ambayo sisi wanataaluma wa mahesabu tulishapiga mahesabu kuwa endapo tutakubali kuuza mafuta kwa bei iliyokuwa imetangazwa na EWURA Agosti 2, mwaka huu, ni wazi BP Tanzania ingepata hasara ya Sh. bilioni 3.1.

“…sasa sisi kama bodi tulivyolitambua hilo ndiyo maana mapema kabisa tukawaandikia wamiliki ili wakae kwenye vikao na watupatie ufumbuzi lakini cha kushangaza hadi sasa mwenye mali mmoja ambaye ni Tanzania hajajibu barua ya bodi yetu,” kilieleza chanzo hicho.

Akizungumza na Tanzania Daima, mwenyekiti wa bodi hiyo, Felix alithibitisha kuwa bodi yake ilimuandikia barua Kaimu Msajili wa Hazina na BP Africa Limeted ili waweze kukutana na kulipatia ufumbuzi jambo hilo, lakini alisema hazina hawakuijibu hali iliyosababisha kuiweka bodi yake katika wakati mgumu.

Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Hazina Msella, alithibitisha kupokea barua hiyo Agosti 11 kutoka Bodi ya BP.

“BP wameniletea barua yao ya kuomba ushauri kwa serikali baada ya BP ambayo Tanzania nayo ina hisa 50 kugoma kuuza mafuta…sasa kama BP ilishajichukulia uamuzi wake ikaungana na kampuni nyingine za mafuta kugoma, sasa mimi nifanyeje?

“BP ilitaka mimi kwa niaba ya serikali niwashauri nini, wakati tayari ilikuwa imeshajichukulia maamuzi yake ya kugoma,” alisema Msella.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili imezipata kutoka ndani ya jeshi la polisi, Mwenyekiti wa Bodi amekuwa akiripoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi tangu Ijumaa wiki iliyopita kila siku hadi jana mchana.

Hata hivyo chanzo chetu cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilisema jeshi hilo linasubiri maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuhusu sheria gani itumike na kwa mashitaka gani yatakayo mkabili mwenyekiti huyo wa bodi.

Habari zaidi zinaeleza kuwa polisi walilazimika kumpa dhamana mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambapo ameacha hati yake ya kusafiria polisi kama dhamana.

Wiki iliyopita, taifa lilijikuta na wakati mgumu na vurugu za hapa na pale kufuatia wafanyabiashara wa mafuta kugoma kuuza mafuta kwa madai ya kukaidi agizo la EWURA lilowataka wafanyabiashara hao kupunguza bei.

Lakini hata hivyo juzi Meneja wa Biashara wa EWURA , Godwin Samuel aliibuka na kuzungumza na waandishi wa habari kuwa mamlaka hiyo inatangaza kupanda kwa bei za mafuta zote nchini ambazo zinaanza kutumika rasmi jana na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia sambamba na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani.

Akitangaza bei mpya, Samwel alisema petroli imepanda kwa sh 100.34 sawa na asilimia 5.51, dizeli sh 120.47 sawa na asilimia 6.30 huku mafuta ya taa yakipanda kwa sh 100.87 sawa na asilimia 5.30.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 17 mwaka 2011.





No comments:

Powered by Blogger.