Header Ads

TAO 'AKWAA KISIKI' KORTI KUU

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha (TLP) Hamad Tao dhidi ya Mbunge wa Ilala(CCM), Mussa Hassan ‘Zungu’lilokuwa linataka mahakama hiyo imsamehe asilipe dhamana ya kesi hiyo ya uchaguzi kwa maelezo ombi hilo liliwasilishwa kabla ya wakati wake.


Uamuzi wa kesi hiyo ya uchaguzi Na.104/2010 iliyofunguliwa na Tao ambaye hivi karibu alifukuzwa uanachama wa chama hicho, ulitolewa jana na Jaji Dk.Fauz Twaibu ambaye alisema amefikia uamuzi baada ya kubaini ombi hilo la Tao lakutaka asamehewe kulipa dhamana ya kesi hiyo kwasababu ombi hilo pia halikukidhi matakwa ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

Jaji Dk.Fauz alisema sheria ya uchaguzi imeweka kiwango cha juu cha shilingi milioni tano ambacho mlalamikaji anapaswa kuweka mahakamani kama dhamana kwa kila mlalamikiwa, lakini sheria hiyo inamtaka mlalamikaji afike mahakamani na kuieleza mahakama kuwa yeye anauwezo wa kulipa kiasi gani sasa baada ya mahakama kuamuru mdaiwa alipe kiwango gani cha dhamana bado sheria hiyo inamruhusu mlalamikaji kuwalisha ombi la kuiomba mahakama imsamehe kabisa kulipa fedha yoyote kama dhamana na mahakama inaweza kurithia kama inajiridhisha mlalamikaji huyo ni kweli hana huwezo wa kulipa dhamana.

“Sasa kwa mtiririko huo wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, ombi hilo la Tao halikufuata mtiririko huo matokeo yake Tao amewasilisha moja kwa moja ombi la kutaka asamehewe badala ya kwanza kuwasilisha ombi la kuomba apunguziwe dhamana ya sh milioni tano kwa kila mdaiwa ….kwahiyo mahakama hii inatupilia mbali ombi la Tao kwasababu liliwasilishwa kabla ya wakati wake na kwa sababu hiyo kesi ya msingi haitaweza kuendelea”alisema Jaji Fauz.

Katika kesi ya msingi ambayo Tao anamshtaki Zungu, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Ilala na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mlalamikaji huyo anadai kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jimbo la Ilala, mwaka 2010 yaliyomtangaza Zungu kuwa mshindi yafutwe kwasababu yeye alizuiliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro na Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo .

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Agosti 18 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.