Header Ads

HAKIMU KESI YA JERRY MURRO ACHARUKA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema inachukizwa na tabia ya mawakili wa utetezi katika kesi ya kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1), Jerry Murro na wenzake ya kutofika mahakama siku ya kesi hiyo kwa maelezo kuwa wapo Mahakama Kuu kwaajili ya kuudhuria kesi nyingine.


Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi Frank Moshi muda mfupi baada ya Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface kuieleza mahakama kuwa kesi hiyo imekuja jana kwaajili ya washtakiwa kuanza kujitetea lakini mawakili wa utetezi Richard Rweyongeza na Majura Magafu wamemwarifu kuwa hawatakuwepo kwasababu wamekwenda Mahakama Kuu kuudhuria kesi mbalimbali na kwamba upande wa jamhuri upo tayari kwaajili ya kuendelea na kesi.

“Kwa zaidi ya mara nne sasa washtakiwa wanashindwa kupanda kizimbani kuanza kutoa utetezi wao kwasababu mawakili wao wamekuwa wakitoa udhuru kuwa hawatafika katika Mahakama ya Kisutu kwasababu wapo Mahakama Kuu kuudhuria kesi nyingine…sasa nasema sitaki tena kuona kesi hii inaarishwa kwasababu kama hizo,sote tumekuwa tukipanga tarehe za kuanza kusikilizwa na tunakubaliana lakini siku kesi inapokuja kesi haiendelei kwasababu eti mawakili wa utetezi wanakuwa mahakama za juu kwaajili ya kesi nyingine.

“ Hivyo leo nataka mjitambue nyie wote hapa ni mawakili na kila wakili ana dayari yake inayoonyesha ni lini atakuwa na kesi fulani katika mahakama hipi ….sasa leo pangeni tarehe ambayo nyie mnafahamu siyo mtafika hapa mahakamani bila kukosa ili mahakama hii ianze kupokea utetezi wa washtakiwa narudia tena hii tabia ya kutoa udhuru siku ya kesi hii inapokuja eti mawakili wa utetezi wapo mahakama kuu inakera sana” alisema Hakimu Moshi.

Hakimu Moshi aliarisha kesi hiyo hadi Agosti 18 mwaka huu, kwa kuendelea kusisitiza kwa kuwataka mawakili wa washtakiwa kufika siku hiyo bila kukosa ili washtakiwa waanze kupanda kizimbani kujitetea.

Mbali na Murro, washitakiwa wengine ni Edmund Kapama na Deogratius Mugasa ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 15 mwaka 2010.
Washitakiwa haop wanadaiwa kula njama, kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Kati ya mashitaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashitaka mawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Agosti 4 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.