Header Ads

JERRY MURRO:POLISI WAMENIBAMBIKIZIA KESI


Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1), Jerry Murro(30), anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh milioni 10, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone hana hatia kwasababu kesi hiyo inayomkabili amebambikiwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.


Murro alitoa ombi hilo jana wakati anaongozwa na wakili wake Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi ambapo alidai kuwa uzalendo wake kwa jamii na uchapakazi wake katika habari za uchunguzi na kuibua ufisadi uliokuwa ukifanywa na askari wa polisi wa kikosi cha usalama barabarani ambao walikuwa wakila rushwa toka kwa madereva, na habari kuhusu ufisadi uliokuwa ukifanywa na raia mmoja wa korea katika halmashauri ya mji wa Bagamayo.

Mshtakiwa huyo kwanza alyakana mashtaka yanayomkabili ya yeye na washtakiwa wenzake Deo Muggasa na Kapama kuwa walikula njama na kisha kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Kaloli Wage kwa madai kuwa yeye hakuwa hakiwafahamu hao washtakiwa wala Wage na kwamba amekuja kuwafahamu kwa mara ya kwanza siku alipofikishwa mahakamani na Mahakao Mkuu ya Jeshi la Polisi.

Murro ambaye wakati akitoa utetezi wake alieleza mahakama kuwa yeye ni mwandishi wa mwanadamizi na mwenye shahada ya uandishi wa habari ya Chuo Kikuu lakini alipoulizwa swali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface kuwa elimu yake ya mwisho kabisa ni kiwango gani mshtakiwa huyo akajibu elimu yake ya mwisho ni ya kidato cha sita, alieleza kuwa yeye alikwenda katika Hoteli ya Sea Cliff ,Januari 28 mwaka 2010 kwaajili ya kuona na mtu ambaye hamfahamu na akafanya nae mazungumzo licha hakuweza kuieleza mahakama walifanya mazungumzo gani na mtu huyo.

Lakini hata hivyo akakanusha madai ya upande wa Jamhuri kuwa yeye alikwenda hotelini hapo Januari 29 mwaka 2010 na kukutana washtakiwa wenzake pamoja na Kaloli kama kilelezo cha picha za CCTV zinavyomuonyesha na pia akayakana maelezo aliyochukuliwa na Inspekta wa Polisi Issa Chabu na Koplo Lugano Mwansampeta aliyochukuliwa Januari 31 na Februali 2 mwaka jana licha mshtakiwa huyo akakiri saini zilizopo ndani ya maelezo hayo ni zake.

Alipohojiwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Boniface ni kwanini akubali kuweka saini yake kwenye maelezo ambayo siyo yake, Murro ambaye wakati anahojiwa na wakili huyo alionekana kuwa na jazba na kujifuta jasho, alidai siku zote polisi ni watu wa kutoa amri kwa watuhumiwa na kwamba yeye alipewa amri ya kusaini tu maelezo hayo ambayo yaliandikwa na Inspekta Issa na Koplo Mwansampeta.

“Mimi ni mtu maarufu kwenye jamii na kwasiku naweza kusalimiwa na watu zaidi ya elfu moja kutokana na kazi yangu ya kuandika habari za uchunguzi ambazo zilisababisha nipate zaidi ya tuzo tatu hapa nchini na wkaati napatwa na kesi hiyo mimi nilikuwa ndiyo Mkuu wa Dawati la Kipindi cha Usiku wa Habari TBC1, na habari zile za kulipua ufisadi wa polisi ndiyo zilizosababisha kila kukicha nipate vitisho, nijeruhiwe, gari langu ligongwe na taarifa za matukio hayo nimekuwa nikiyaripoti polisi lakini hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa.

“Hali iliyosababisha aliyekuwa bosi wangu kule kituo cha ITV, Reginald Mengi kuninunulia bastora yenye magazine mbili ambayo ilikuwa inaifadhi risasi 12 na bastora hiyo ilikuwa ni ya kipekee sana kwani ilikuwa ni nzito na nipia akaninunulia na pingu pale katika Duka la silaha Upanga kwaajili ya kujilinda na baada ya kununua vitu hivyo nilipewa kibali cha kumiliki naninarudia tena kutokana na umaarufu wangu kwenye jamii jeshi la polisi likanipatia maofisa wa juu wakanipeleka Makao Makuu ya FFU- Ukonga na wakanifundisha kulengaa silaha nikaweza hivyo kwenye kazi zangu zote nikawa natembea na bastora hiyo na pingu”alidai Murro ambaye hata hivyo hakutoa ushahidi kama ni kweli alikuwa akiyaripoti matukio hayo polisi na kupewa RB.

Akieleza siku ya Januari 31 mwaka 2010, ambayo ndiyo siku aliyokamatwa, kabla ya kukamatwa asubuhi alipigiwa simu na mtu asiyemhafamu akamtaka aifike katika mgahawa wa City Gargen mtaa wa Mkwepu kwani kutakuwa na mkutano na waandishi wa habari ambao utakuwa ukiwataja mafisadi hivyo mtu huyo akamtaka afike bila kukosa.

Murro aliendelea kueleza kuwa alitii mualiko huo na alipofika kwenye maegesho ya mgahawa huo akaanza kuipiga ile namba ya mtu huyo aliyemuarika huku siku hiyo ikiwa inakatwa na sekunde chache baadaye akaona mtu anamgongea kwenye kioo chake cha gari akimtaka ateremke chini huku pembeni kuwa na gaina ya aina ya Defender la Polisi likiwa na askari polisi wakiwa wamebeba silaha aina ya SMG mabegani wakalizuia gari lake kwa gari mbele na kisha askari hao wakamuonyeshea Wage na ndipo askari mmoja akaingia kwenye gari la Murro na kuanza safari ya kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa maelezo zaidi.

“Nilipofika kituo hicho kikuu cha polisi nilikuta waandishi wa ha bari wengi sana na polisi wakinitazama wengine wakinikebei kuwa nimekamatika nikachukuliwa maelezo nikapewa dhamana lakini siku tatu baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo alinifuata ofisini TBC1, na kunieleza kuwa nimekwisha na akanionyesha picha za CCTV ambazo eti zinanionyesha nikiwa na hawa washtakiwa wenzangu na waziri huyo akanitaka nikaitishe mkutano na waandishi wa habari niwaeleze kuwa sikubambikiwa kesi na polisi bali nilitofautiana na polisi katika kazi, nikamweleza bosi wangu Tiddo Mhando kuhusu maelekezo hayo , Mhando akanikataza nisiitishe mkutano”alieleza Murro.

Aliendelea kueleza kuwa yeye alikuwa akifanyakazi kwa karibu na jeshi la polisi hasa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova lakini baada ya kubambikiziwa kesi hiyo alishangazwa kumuona Kova akishiriki kumgandamiza hali iliyosababisha yeye kushikwa na hasira na kuingia ofisini kwa Kova nikisha kumsema maneno ya ukali kwani ni Kova huyo huyo ambaye alikuwa akimpatiaga fedha kidogo ili aweze kumjenga katika habari alizokuwa akizurusha kwenye TBC1 ili Kova aonekane ni mchapakazi hodari.

Yafuatayo ni mahojiano baina ya wakili wa serikali Boniface na Murro;
Swali:Wakati unatoa utetezi wako umesema unaelimu ya Chuo Kikuu, ebu tueleze vizuri elimu yako ya mwisho yaani ya mwisho kabisa ni ya kiwango gani?Jibu:Kidato cha Sita.
Swali:Pia ulieleza kuwa tangu uanze kuandika habari za uchunguzi umekuwa ukipokea vitisho na umedai umekuwa ukitoa taaarifa polisi lakini hadi unamaliza kujitetea umeshindwa kutoa ushahidi wa hata RB moja kuonyesha uliokuwa ukitoa taarifa, sasa unaizungumziaje kesi hii hii inayokukabili?

Jibu:Kesi hii ni mwendelezo wa majanga ya vitisho nilivyokuwa nikivipata kutokana na mimi kuandika habari zilizokuwa zinaibua ufusadi.

Swali:Wage siyo polisi na wala hujawai kuandika habari za ufisadi wake kwasababu ufisadi Wage alishafukuzwa kazi na waziri Mkuu Mizengo Pinda na kwamba wewe hukuona ni habari kuandika ufisadi wake, sasa ni kwanini wakati unajijetea hapa umedai Wage na polisi ndiyo wamekubambikia kesi hii?
Jibu:Kimya!

Swali:Wewe umesema hapo awali ulikuwa humfahamu Wage wala washtakiwa wenzako, sasa inakuwaje huyu Wage umekutana naye wakati ulipokamatwa halafu ashiriki kukubambikizia kesi?
Jibu:Kimya.

Swali:Ulisema vitisho vyote ulivyokuwa ukipata vilikuwa vikikutaarifu kuwa mwisho wako ni kaburi, sasa ieleze mahakama kesi hii inayokukabiri ni kaburi?

Jibu:Ndiyo ni kaburi, maana naweza kupelekwa gerezani nikazibwa mdomo nikauwawa,kesi hii imesababisha nifukuzwe kazi, sina mshahara, Dola za Kimarekani nilizopata baada ya kushinda Tuzo ya Mwandishi Bora wa mwaka 2009, Katibu Mkuu wa Baraza wa Habari Kajubi Mkajanga ameniandikia barua ya kuniarifu kuwa hawataweza kunipatia fedha hizo hadi kesi itakapomalizika na kwamba hela hiyo ina kikomo cha mimi kuichukua ambayo ni Desemba mwaka huu, pia ile nyumba niliyopanga Kunduchi watu wameenda kwa mwenye nyumba wakamjaza maneno baba mwenye nyumba akasitisha mkataba na mimi akanitaka niondoke na hivi sasa nimerudi kuishi kwenye Mabibo.

Swali:Kama kesi hii ni kaburi kwahiyo wewe unayezungumza hapa mahakama ni mzimu maana kaburi analala marehemu ambaye hawezi kuzungumza?
Jibu:Kimya!watu wakacheka.

Swali:Taja kwa majina hao polisi unaodai wamekubambikizia kesi na wanaendelea kukuangamizia!
Jibu:Kimya! Mimi sio msemaji wa jeshi la polisi.

Mshtakiwa huyo alimaliza jana kutoa utetezi wake na Hakimu Moshi iliairishwa hadi Septemba 27 mwaka huu,ambapo shahidi mmoja wa Murro anapanda kizimbani kumtetea Murro.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.