Header Ads

PINGAMIZI LA AG KESI YA MPENDAZOE KUSIKILIZWA KWA MAANDISHI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam,jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililotaka kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Segerea iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Fred Mpendazoe(Chadema) ifutwe kwasababu hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho imekiuka amri ya mahakama hiyo, badala yake imezitaka pande zote kuwasilisha hoja zake kwa maandishi.


Wadaiwa katika kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wa Jimbo la Segerea ni Mwansheria Mkuu wa Serikali(AG), Mbunge wa jimbo hilo, Dk.Makongoro Mahanga (CCM) anayetetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.Mahanga anayapinga matokeo yaliyomtangaza mshindi Mahanga kwasababu kanuni na sheria ya Uchaguzi zilikiukwa.

Mawakili wa Serikali Patience Ntinwa na David Kakwaya mbele ya Jaji Profesa Ibrahim Juma waliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ya madai ilikuja jana kwaajili ya mahakama hiyo kuanza kusikiliza pingamizi hilo la mdaiwa ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya mlalamikaji Mpendazoe.

Jaji Profesa Juma alisema muda alikuwa na muda mchache ambao usingeweza kusikiliza pingamizi hilo na kwasababu hiyo anatoa amri ya pingamizi hilo kusikilizwa kwa njia ya maandishi hivyo akamtaka mwanasheria mkuu wa serikali kuwasilisha sababu za pingamizi lake kwa maandishi Agosti 10 na mlalamikaji (Mpendazoe) awasilishe majibu ya pingamizi hilo Agosti 24 na mdaiwa ajibu kama analakujibu kutokana na hoja zitakazokuwa zimewasilishwa na mlalamikaji Agosti 30 na kwamba uamuzi wa pingamizi hilo atautoa Septemba 15 mwaka huu.

Julai 5 mwaka huu, wadaiwa wawili AG, na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Segerea waliwasilishwa kwa maandishi mahakamani hapo mapingamizi mawili ambapo pingamizi la kwanza wanadai kuwa hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho na kuwasilishwa na mlalamikaji mahakamani ni batili kwasababu imekiuka amri ya mahakama iliyomtaka mlalamikaji huyo akaifanyie marekebisho tu hati hiyo ya madai lakini cha kustaajabisha mlalamikaji huyo amewasilisha hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho huku akiwa ameongeza dai jipya ambalo halikupaswa kuwekwa kwenye hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho akiwa ameongeza dai jipya ambalo halikupaswa kuwekwa kwenye hati hayo hivyo wakaomba hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho nayo itupwe.

Kuwasilishwa majibu hayo ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho pamoja na pingamizi hilo kulitokana na amri iliyotolewa na Jaji Juma, Juni 22 mwaka huu kwa wadai hao.

Kuwasilishwa mahakamani kwa hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho na Mpendazoe, kulitokana na utekelezaji wa amri iliyotolewa na Jaji Profesa Juma, Juni 6 mwaka huu, ambapo aliamuru hati ya madai ya awali ikafanyiwe marekebisho kwa kuviondoa vituo 10 vya kupigia kura ambavyo mlalamikaji hakuvitaja kwa majina.

Baada ya kufanyiwa marekebisho, Wakili wa mlalamikaji Peter Kibatala alieleza hivi sasa hati hiyo inasomeka kuwa wamebakiwa na vituo vya kupigia kura 249 ambapo vituo 120 ni vya Kata ya Kiwalani na vituo 129 ni vya Kata ya Vingunguti.

Novemba mwaka 2010 Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza mbunge wa sasa Dk. Mahanga kuwa ndiye mshindi kwa sababu uchaguzi huo ulikiuka matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Julai 28 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.