Header Ads

ZOMBE:GODBLESS LEMA NI MBUMBUMBU WA SHERIA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi,(ACP), Abdallah Zombe amesema Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA) Godbles Lema ni mbumbumbu wa Sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Sambamba na hilo Zombe amemtaka Lema kufuata yale yote aliyotumwa na wapiga kura wake bungeni na siyo kumjadili yeye na kwamba wakati mbunge huyo alipokula kiapo cha utii wa kuitii Katiba na leo hii anatenda matendo yanakwenda kinyume na kanuni za bunge na katiba hiyo, hivyo mbunge huyo ni hatari kwa nchi na wapiga kura wake.

Zombe aliyasema hayo jana kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nje ya viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo alisema uamuzi huo baada ya Julai 28 mwaka huu, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha kuwasilisha bajeti yake na mbunge huyo ambaye ni waziri kivuli wa wizara hiyo kuhoji ni kwanini Zombe na wenzake waliachiliwa huru wakati nimiongoni mwa askari polisi walioua raia bila hatia.

“Mwalimu Julias Nyerere aliwahi kusema kuwa huru bila nidhamu ni sawa na wendawazi na nidhamu bila uhuru ni sawa na utumwa…sasa kwanukuu hiyo na ukiioanisha na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya wabunge akiwemo Lema nasema kabisa wabunge hao wanaofanya vitendo hivyo ni wendawazimu na hawastahili kuendelea kuwepo bungeni kwani wanaporomosha heshima ya bunge letu tukufu”alisema Zombe.

Alisema tangu mwaka 1992 vyama vingi viliporuhusiwa hapa nchini, vyama vya upinzani viliweza kushinda katika majimbo mbalimbali na kufanya wabunge wao kuingia ndani ya bunge ambao siku zote wabunge hao wa upinzani kama Freeman Mbowe Said Arif,Wilbroad Slaa, Habib Mnyaa wamekuwa wakiheshimu kanuni za bunge lakini cha kushangaza Lema na wenzake wamekuwa mstari kufanya vitendo vya kiwendawazimu bungeni hali inayopelekea kuidhalilisha CHADEMA.

Zombe alimtaka Lema akaisome Ibara ya 107A ya Katiba, ambayo inasema wazi mamlaka ya mwisho ya utoaji haki ni mahakama lakini anashangazwa na mbunge huyo kwenda kuhoji kesi ilikwishatolewa uamuzi na Mahakama Kuu na rufaa yake tayari imeshafunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka katika Mahakama ya Rufaa na kuongeza kuwa kitendo kilichofanywa na mbunge huyo dhidi yake ni dhahiri mbunge huyo hafamu kuwa majukumu yanayofanywa na mihili mitatu ya nchi ya Serikali,Bunge na Mahakama.

“Lema anasimama katika ya bunge ananizungumzia mimi wakati anajua wazi ananizungumzia mimi ambaye sinafursa ya kwenda kujieleza bungeni?Ninavyomfahamu mimi huyu Lema ni miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kuwa mwanamtandao wa wezi wa magari Arusha na taarifa hizo za Kiintelijensia zilinifikia ofisini kwangu wakati nipo RCO hapa jijini na wakati zikifanyiwa kazi ndiyo nikapatwa na matatizo ya kubambikiwa kesi na sina hakika kama amaeacha hiyo tabia ….na ninasisitiza naungana na kauli ya mbunge wa (CCM), Deo Filikunjombe utovu wa nidhamu unaoendelewa kufanywa na baadhi ya wabunge ni utoto”alisema Zombe.

Aidha alisema anashangazwa na Lema kuwa na jeuri ya kuhusu kesi mauji iliyokuwa ikimkabili yeye na wenzake lakini mbunge huyo anashindwa kutumia bunge hilo hilo kuhoji kesi ya maandamano haramu inayomkabili yeye na wanachama wengine wa CHADEMA katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha imefikia wapi na kuongeza kwa kuwataka wabunge wafuate kilichowapeleka bungeni na siyo kumaliza muda mwingi kuwajadili wananchi ambao siyo wabunge.

Wakati huo huo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, Upendo Msuya aliairisha kesi ya madai y ash bilioni 5.2 iliyofunguliwa na Zombe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba anaiarisha hadi Septemba 8 mwaka huu, kwaajili ya kuanza kusikilizwa.

Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwachilia huru Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Serikali ilikata rufaa Oktoba 7, 2009 katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachilia Zombe na wenzake.

Akisoma hukumu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, alibaini kuwa serikali ilishindwa kuthibitisha mashtaka na kuwa kamwe mahakama haiwezi kumtia hatiani mshtakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo.

Jaji huyo alihitimisha hukumu yake kwa kusema kuwa washtakiwa hao si wauaji na aliliagiza Jeshi la Polisi liwatafute wauaji halisi wa wafanyabiashara waliouawa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 2 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.