Header Ads

SERIKALI ISIFANYE PUPA KUWASHTAKIWA VIGOGO WA BP

Na Happiness Katabazi

KWA takribani wiki mbili sasa taifa lilijikuta likikabiliwa na uhaba wa mafuta kwasababu ya wafanyabiashara wa nishati hiyo kugoma kuuza nishati hiyo kwa bei elekezi iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji(EWURA) ambayo iliwataka wafanyabiashra hao kushusha bei.


Lakini wakati sekeseke hilo likitulia, Jumapili ya wiki hii EWURA ilijitokeza adharani na kusema kuwa wamepandisha bei ya mafuta ambayo bei hiyo mpya ilianza kutumikia tangu jumatatu wiki hii.

Wakati EWURA ambayo ipo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ikitangaza bei mpya,Jumatatu wiki hii naye waziri wa wizara hiyo William Ngeleja alizungumza bungeni akisema bei hiyo haipaswi kuanza kutumika sasa.Kauli hizo mbili siyo tu zimewakera wananchi bali pia zimewafanya wananchi kuendelea kuwadharau baadhi ya viongozi wa serikali ambao hivi sasa wamekuwa na utamaduni wa kutoa matamko yanayokinzana ilihali wapo kwenye serikali moja.

Ukiachulia mbali hayo pia vyombo vya vimekuwa vikiripoti Mwenyekiti wa Bodi ya BP, Philemon Felix amekuwa akihojiwa na jeshi la polisi ni kwanini BP ambayo Tanzania inahisa 50 nayo ilishiriki kugoma kuuza mafuta na wakati Felix akiendelea kuhojiwa gazeti hili lilifanikiwa kunasa barua waliyokuwa wamewaandikiwa wamiliki wa BP Tanzania ambaye ni Kaimu Msajili wa Hazina na PB Africa ya Afrika Kusini kueleza kuwa endapo BP itatekeleza agizo la EWURA kuuza mafuta kwa bei iliyopunguzwa ni wazi kampuni hiyo ingepata hasara zaidi ya sh bilioni 3.1.

Napenda ieleweke kuwa lengo la mtazamo huu si kutaka kuingilia kazi za wapelelezi wetu wala waendesha mashtaka bali lengo la mtazamo huu ni kutaka kutoa taadhari kwa wapelelezi wetu na waendesha mashtaka na serikali kwa ujumla kwamba wakati wanaendelea na mchakato huo wa kipelelezi wa kutaka kubaini ni kwanini nayo kampuni ya BP haikuuza mafuta, wasiwe na papara wala pupa ya kukukusanya vielelezo na kuandaa hati za mashtaka.

Nimelazimika kutoa taadhari hiyo kwasababu nina ushahidi wa baadhi ya kesi ambazo zilifunguliwa kwa papara, mashinikizo ya kisiasa na kelele za wananchi na matokeo yake upande wa Jamhuri katika kesi hiyo mara kadhaa ikajikuta inapigwa mweleka mahakamani.

Na mifano michache ya kesi zilizofunguliwa matokeo yake serikali ya awamu ya nne ikajikuta inakumbwa na aibu,kudaiwa ni serikali ya visasi ni kesi ya mauji ya wafanyabiashara wa nne iliyokuwa ikimkabili Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na wenzake, kesi ya kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LLC, iliyokuwa ikimkabili Naeem Gile, kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika benki ya NBC Ubungo, kesi mbili za kutoa rushwa katika wa CCM mwaka jana mkoani Iringa zilizokuwa zikimkabili aliyekuwa mgombea Ubunge wa jimbo la Iringa mjini, Fredrick Mwakalebela na mkewe na kesi nyingine ya kutoa rushwa iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa waziri wa zamani, Joseph Mungai.

Katika kesi hizo zote wapelelezi wa Takukuru na Jeshi la Polisi walivurunda vibaya katika kukukusanya vielelezo na kwakuwa wapelelezi walishavurunda nao mawakili wa serikali waliokuwa wakiendesha kesi hizo walikuwa wakishindwa kutamba mahakamani na mwisho wa siku mahakama ilikuja kuwaachiria huru washtakiwa wote.

Na ikumbukwe kesi hizo zote zilifunguliwa kwa mbwembwe na mikogo ya hali ya juu na mawakili wetu wa serikali na Takukuru katika serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete katika mahakama kadhaa hapa nchini.

Ni ukweli usiopingika kuwa katika awamu hii ya awamu ya nne, kesi za jinai ambazo zinawahusu waliokuwa viongozi serikalini ndani ya CCM, wafanyabiashara na watu wenye majina makubwa zimefunguliwa kwa kishindo na zinaendelea licha nyingine zinaendelea kwa kusuasua na kesi nyingine zimemalizika na serikali iliweza kushinda kesi hizo kwasababu ilikuwa imeandaa ushahidi mzuri na hatimaye mahakama ikawatia hatiani washtakiwa.

Kwa muktadha huo hapo juu ni wazi kabisa kama ni kweli serikali imedhamiria kumburuza mahakamani Mwenyekiti wa BP, Tanzania Limited, Philemon Felix na watendaji wengine wa bodi hiyo, sina pingamizi na hilo ila ushauri wangu kwa mamlaka za kipelelezi kwanza wasiwe na papara, waakikishe wanafanya upelelezi wao kikamilifu kwa kukusanya nyaraka vielelezo mbalimbali ambavyo vitakuja kuisaidia Jamhuri katika kesi hiyo kwani tayari kuna taarifa zinadai kuwa katika hilo la sakata la BP, BP walijaribu kuchukua hatua fulani fulani kutaka kupata ridhaa ya ushauri wa serikali bila mafanikio.

Nimelazimika kueleza wasiwasiwa wangu huo kwasababu hivi sasa kumezuka tabia chafu sana ambayo haina tija kwa taifa letu inayofanywa na baadhi ya viongozi wa baadhi ya taasisi zetu za serikali kwa kila mmoja wao kutaka kujifanya yeye ni mchapakazi hodari kwenye jamii kuliko kiongozi wa taasisi nyingine hali inayosababisha viongozi hao ambao wapo kwenye serikali moja kutoa matamko yanayokinza hali inayosababisha wananchi kuanza kuidharau serikali yao.

Na wananchi hao kuishia kuitolea matusi ya nguoni na kumtusi kiongozi wa nchi Rais Kikwete kuwa anaipeleka nchi kuzimu , pindi wananchi hao wawapo kwenye vijiwe vyao mitaani.Matusi ambayo hatuwezi kuyaandika kwenye vyombo vya habari.

Hakuna ubishi kuwa tangu aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, Gray Mgonja na Daniel Yona , aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Mkurugezi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba ambaye Mei 23 mwaka jana alihukumiwa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.Na vigogo hao wengine ambao wanakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi, kusababisha hasara na matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.

Ni wazi kabisa mashtaka hayo kwa asilimia kubwa yamechangia viongozi wengi wengi wa serikali ya awamu ya nne kuogopa kuchukua maamuzi ya mambo fulani fulani kwa maelezo kuwa mwisho wa siku nao wanaweza wakajikuta wanafikishwa mahakamani kwa makosa kama hayo.Na hali hiyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya viongozi tunaokutanaga nao faragha kubadilishana nao mawazo.

Umefika wakati sasa wa serikali ya Kikwete kuwa ni ya viongozi wanajiheshimu,wanaojitambua, wenye kutoa matamko yasiyokinzana kwa maslahi ya taifa letu na wafanyekazi kwa mtindo wa uwajibikaji wa pamoja siyo kusalitiana,kugeukana,kuchimbana, kuzuliana majungu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Ijumaa, Agosti 19 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.