HUKUMU YA MAHALU YAWEKWA KIPORO
Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya Euro milioni mbili, inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin kwasababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo kuwa na majukumu mengi.
Hakimu Mkazi Alocye Katemana alisema kesi hiyo ilikuja jana kwaajili ya kutolewa hukumu na Hakimu Mfawidhi Ilvin Mugeta lakini hakimu Mugeta amemweleza kuwa na majukumu mengine ya kimahakama hivyo hataweza kuisoma hukumu hiyo jana .
Hakimu Katemana alisema kwa sababu hiyo Hakimu Mugeta amemweleza kuwa aiarishe kesi hiyo hadi Agosti 9 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya Hakimu Mugeta kusoma hukumu ya kesi hiyo.
Januari 22 mwaka 2007 kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ben Lincoln, Ponsia Lukosi na Vicent Haule walidai kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa sita ambayo ni kosa la kula njama, wizi wa Euro milioni mbili ,kugushi vocha za manunuzi ya jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia,kutumia risiti za manunuzi ya jengo hilo kuidanganya serikali na kuisababishia serikali hasara ya Euro milioni mbili. Ili kuithibisha kesi yao,upande wa Jamhuri ilileta jumla ya mashahidi saba na upande wa utetezi ulileta mashahidi wa tatu ambao ni Mahalu,Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na Grace Martin.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Julai 12 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment