VIGOGO SUMA -JKT KORTINI
Na Happiness Katabazi
MKURUGENZI wa Shirika Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) Kanali Ayoub Mwakang’ata na maofisa wenzake sita wa jeshi hilo jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka saba ya kula njama na matumizi mabaya ya madaraka.
Mbali na Kanali Mwakang’ta washitakiwa wengine ni Luteni kanali Mkohi Kichogo,Luteni Kanali Paul Mayavi,Meja Peter Lushika,Sajenti John lazier,Meja Yohana Nyichi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta wa SUMA JKT-Luteni Kanali Felex Samillan.
Mawakili toka ofisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa(TAKUKURU), Dominsian Kessy na Ben Lincoln walidai mbele ya Hakimu Mkazi Alocye Katemana na kuwa kosa la kwanza ni la matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, inayowakabili washitakiwa wote.
Wakili Kessy alidai kuwa Machi 5 mwaka 2009 katika chumba cha mikutano cha ofisi ya SUMA JKT Dar es salaam,wakiwa ni wajumbe wa bodi na Bodi ya Tenda ya SUMA JKT kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa maamuzi ya bodi hiyo ambayo yaliyoonyesha yametolewa na TAKOPA kwa madhumuni ya kununua magari na vifaa vya ujenzi bila kupata idhini ya kutoka Bodi ya ya Wakurugenzi ya TAKOPA.
Wakili Kessy alidai kosa la pili pia ni la matumuzi mabaya ya madaraka ambalo linawakabiliwa washitakiwa wote kuwa Machi 12 mwaka 2012 ,washitakiwa hao wakiwa ni wajumbe wa bodi ya Tenda ya SUMA JKT walitumia madaraka yao vibaya kwa kupitishia maazimio ya kununuliwa kwa magari na vifaa vya ujenzi ambavyo vilikuwa vimeishatumika kinyume na kifungu cha 58( 3) cha Sheria ya Mamunuzi ya Umma ya mwaka 2005.
Aidha alidai shitaka la tatu ni la matumizi mabaya ya madaraka linalomkabili mshitakiwa wa pili na wa saba( Kichogo, Samillan) ambapo Machi 16 mwaka 2009 wakiwa wajumbe wa bodi ya Tenda ya SUMA JKT waliamisha Sh 2,744,432,545 kupitia hundi Na.000010 kutoka akaunti ya TAKOPA Na.011103031753 kwa SUMA JKT akaunti Na.01110307094 ambazo akaunti hizo zote zipo katika katika Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) bila kufuata matakwa ya kifungu cha 156 cha Sheria ya Fedha ya Umma na Kanuni zake ya mwaka 2001.
Shitaka la nne alidai linawakabili washitakiwa hao wawili yaani mshitakiwa wa pili na watatu ambalo pia ni la matumuzi mabaya ya madaraka ambalo walilitenda Aprili 3 mwaka 2009,wakiwa wajumbe wa bodi hiyo ambapo waliamisha sh 489,677,879.30 kupitia hundi Na.000011 kutoka TAKOPA akaunti Na.011103031763 kwa akaunti Na. 011103017094 ya SUMA JKT ambazo zote zipo kwenye benki ya NBC bila kufuata kanuni na matakwa ya kifungu cha 156 cha Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001.
Shitaka la tano ambalo linawakabili tena washitakiwa hao wawili ni matamizi mabaya ya madaraka ambapo Aprili 4 mwaka 2009 wakiwa ni wajumbe wa bodi hiyo waliamisha Sh 269,519,093.60 kupitia hundi Na.000012 kutoka akaunti ya TAKOPA Na.011103031753 kwa SUMA JKT akaunti Na.011103017094 akaunti zote ambazo zipo benki ya NBC bila kuzingatia masharti ya kifungu cha 156 cha Sheria ya Fedha za umma na kanuni zake ya mwaka 2001.
Wakili Kessy alidai shitaka la sita linawakabili washitakiwa hao wawili tena ambapo nilamatumizi mabaya ya madaraka ambapo Mei 4 mwaka 2009 wakiwa ni wajumbe wa bodi hiyo,waliamisha shilingi 350,000,000,000 kupitia hundi Na.000015 kutoka akaunti ya TAKOPA Na.011103031753 kwa SUMA JKT akaunti Na. 011103017094 bila kufuata matakwa ya kifungu hicho cha sheria ya Fedha za umma.
Hata hivyo alidai shitaka la saba ni linawakabili washitakiwa wote ambalo ni la kula njama kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambapo kuwa kati ya Machi na Mei mwaka 2009 wakiwa wajumbe wa bodi hiyo jijini Dar es Salaam, walikula njama na kuamisha mradi kutoka akaunti ya TAKOPA Na. 011103017094 ambazo akaunti hiyo ipo NBC bila kufuata matakwa ya kifungu cha 156 cha Sheria ya Fedha ya umma na kanuni zake ya mwaka 2001 na kuongeza kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Hata hivyo washitakiwa wote walikana mashitaka hayo na Hakimu Katema alisema ili wapate dhamana ni lazima kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi ya shilingi milioni 25 kila mmoja, na washitakiwa hao walitimiza masharti hayo na wakapata dhamana, na akaiarisha kesi hiyo hadi Agosti Mosi huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 3 mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment